DC Mbozi afariki dunia, akumbukwa kwa uchapakazi

Mbeya/Manyara. Mkuu wa Wilaya ya Mbozi, Ester Mahawe amefariki dunia, viongozi wa Serikali na Chama cha Mapinduzi (CCM), wakimkumbuka kwa uchapakazi.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa), Mohamed Mchengerwa kwa niaba ya Rais, Samia Suluhu Hassan ametangaza kifo cha mkuu huyo wa wilaya kilichotokea leo Januari 14, 2025 katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kaskazini (KCMC) mkoani Kilimanjaro alikokuwa akipatiwa matibabu.

Katika taarifa iliyotolewa na Nteghenjwa Hosseah, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Ofisi ya Rais (Tamisemi), Mchengerwa ametoa pole kwa familia, mkuu wa Mkoa wa Songwe, wafanyakazi na wananchi wote wa wilaya ya Mbozi, ndugu, jamaa na marafiki.

“Ofisi ya Rais Tamisemi kwa kushirikiana na familia inaendelea kuratibu shughuli za mazishi na taarifa zaidi zitaendelea kutolewa,” inaeleza taarifa hiyo.

Rais Samia kupitia mitandao ya kijamii ameomboleza kifo cha Mahawe akisema kimemsikitisha.

“Nawapa pole familia ya marehemu, Mkuu wa Mkoa wa Songwe, ndugu, jamaa na wote walioguswa na msiba huu. Tunamshukuru Mwenyezi Mungu kwa maisha ya Esther na utumishi wake kwa umma ambao uliongozwa na uchapakazi hodari, ukweli na msimamo thabiti katika utendaji,” amesema.

Mahawe amewahi kuwa mbunge wa viti maalumu kupitia CCM mwaka 2015 hadi 2020.

Aliteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Kigoma mwaka 2021 na baadaye mwaka 2023 Rais Samia alimhamishia Wilaya ya Mbozi.

Katika utendaji wake alikuwa mstari wa mbele kuhakikisha wasichana wanapata elimu bora.

Mahawe pia alikuwa mjumbe wa mkutano mkuu wa CCM Taifa. Mwaka 2020 aligombea ubunge jimbo la Babati Mjini na kwenye kura za maoni aliongoza, ila akapitishwa Pauline Gekul kugombea nafasi hiyo.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi mkoani Songwe, George Musyani amesema kifo cha mkuu huyo wa wilaya ni pigo kubwa.

Amesema alikuwa mtumishi aliyekuwa mstari wa mbele kuipigania wilaya hiyo.

“Leo saa 4:00 asubuhi tumepata taarifa za kifo chake akiwa anaendelea na matibabu KCMC, ni pigo kubwa kwa kuwa alikuwa kiongozi aliyejali kazi na kuwathamini wananchi wake bila kubagua,” amesema.

Amesema suala la mazishi wanasubiri mamlaka na familia yake, akisema wataendelea kumkumbuka kwa kuwa alijipambanua katika kusimamia ulinzi na usalama.

Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) mkoani Songwe, Radwel Mwampashi amesema anawasiliana na mamlaka husika kujua taratibu za mazishi.

“Sijajua zaidi kwa kuwa tumepata taarifa leo, lakini alikuwa anaumwa kwa muda mrefu, hivyo tunasubiri mipango mingine zaidi ikiwamo ya mazishi,” amesema Mwampashi.

Mkazi wa mjini Babati, Wilbroad Bayo amesema hakuna maneno yanayotosha kumzungumzia Mahawe.

Mkazi wa mjini Bahati, Sweet Dominick amesema Mahawe ameondoka kipindi ambacho bado anategemewa katika uongozi.

Amesema atakumbukwa kwa kuibua vipaji vya vijana akieleza mwaka 2019 kupitia Manyara Talent Search alimuibua msanii Prisca Getu.

Related Posts

en English sw Swahili