Lema asimama na Lissu, ampa neno Mbowe

Dar es Salaam. Aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Kanda ya Kaskazini, Godbless Lema amemshauri mwenyekiti wa chama hicho Taifa, Freeman Mbowe kusikiliza ushauri wa familia yake wa kumtaka kutogombea tena nafasi hiyo.
Lema amesema Mbowe mara kadhaa amekuwa na nia ya kupumzika na kuwaachia nguvu mpya vijana kuendeleza mapambano, lakini watu wanaoitwa wanachama wamekuwa wakimshauri kuendelea kuwa mwenyekiti.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo Jumanne, Januari 14, 2025 Lema amesema anamheshimu Mbowe kutokana na kazi kubwa ya kukijenga Chadema aliyoifanya, lakini kwa sasa asikilize zaidi ushauri wa familia yake.
“Mara kadhaa Mbowe amekuwa akiniambia kuwa anahitaji kupumzika ili atuachie chama tuendeleze mapambano. Lakini, wakati anataka kutekeleza azma yake hiyo wanachama wakaandamana kwenda kwake kumtaka agombee. Akasema nitatafakari kisha akasema nitagombea. Kwangu nadhani ni muhimu akasikiliza ushauri wa familia yake zaidi,” amesema Lema.

Asimama na Tundu Lissu
Lema ameweka bayana msimamo wake kuwa atamuunga na kumpigia kampeni Tundu Lissu ili awe mwenyekiti wa chama hicho.
Lissu ambaye ni makamu mwenyekiti wa Chadema-Bara, anachuana na mwenyekiti wake wa sasa Freeman Mbowe kwenye uchaguzi unaotarajiwa kufanyika Januari 21, 2025.

Lema pia, ametoa msimamo wake kuwa iwapo Mbowe atashinda nafasi hiyo, basi yeye hatagombea ubunge Arusha Mjini kwenye uchaguzi utakaofanyika baadaye mwaka huu.
“Niko hapa kuweka bayana kwamba, ninamuunga mkono Lissu. Najua nitakuwa kwenye wakati mgumu sana mbele ya kaka yangu (Mbowe), lakini niweke wazi kuwa ninamuunga mkono Lissu na nitampigania kwenye harakati hizi za kuwa mwenyekiti.
“Nishafuatwa na watu wakinitaka nisimuache kaka yangu kwenye hii vita, wengine wamekwenda hadi kwa mama yangu kijijini kunishtakia kuwa kama sitamuunga mkono Mbowe akishinda nitakosa nafasi ya kugombea ubunge. Niseme wazi, ninasimama na Lissu na kama mwenyekiti (Mbowe) atashinda basi sitagombea ubunge Arusha Mjini,” amesema Lema.

Endelea kufuatilia Mwananchi.

Related Posts