Lema ataja kiini cha tatizo Chadema, Mnyika azungumza

Dar es Salaam. Ni dhahiri Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kinapitia kwenye nyakati ngumu zinazotishia mustakabali wa chama hicho kikuu cha upinzani nchini.

Kwa zaidi ya miaka 20 Chadema kimejipambanua kama chama cha siasa chenye kuipa changamoto Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinachoongoza dola kwa sasa. Hata hivyo, kwa sasa Chadema kiko kwenye nyakati ngumu wakati ambao Mwenyekiti wake Freeman Mbowe na makamu wake- Bara, Tundu Lissu wako kwenye vita ya kuwania uongozi wa chama.

Lissu na Mbowe wote wanawania nafasi ya uenyekiti jambo ambalo limeibuka kambi mbili tofauti zote zikiwa na nguvu kutokana na wafuasi waliogawanyika.

Mbowe anaonekana kuungwa mkono na baadhi ya wajumbe wa Kamati Kuu huku Lissu naye akiungwa mkono na vigogo kama hao. Wachambuzi mbalimbali wa masuala ya siasa nchini, kwa nyakati tofauti wameonyesha hofu kuhusu hali ya mambo inavyoendelea ndani ya chama hicho na minyukano wa makada wake, kila upande ukirusha makombozi upande mwingine.

Hata hivyo, aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Kaskazini na Mjumbe wa Kamati Kuu, Godbless Lema amefichua kiini cha mgogoro huo ambao umekiweka chama hicho kwenye hatari.

Lema, ambaye kama ilivyo kwa viongozi wengine wa Chadema ambao wameshajipambanua upande waliopo kati ya Lissu na Mbowe, naye ameweka bayana kuwa anamuunga mkono Lissu kwenye uchaguzi huo, ameeleza kuwa mpasuko ulioanza muda mrefu kutokana na mambo yaliyokuwa yakianza kuonekana hayaendi inavyopaswa.

Licha ya mara kadhaa kudai kuwa amekuwa akijaribu kukabiliana na hatari hiyo ya mpasuko kwa kuwasiliana na Mbowe, lakini hakuna jitihada zilizochukuliwa hadi kufikia hatua ya mambo kuharibika.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Lema amesema alitumia muda mwingi kumshauri Mbowe kuhusu mpasuko huo, lakini kiongozi huyo hakuchukua hatua.

Mbowe alipotafutwa kwa njia ya mtandao hakupokea na hata alipoulizwa kuhusu kauli ya Lema, alijibu kwa ufupi kupitia ujumbe kuwa yuko kikaoni.

Lema aibua kiini cha tatizo

Lema ambaye alijiweka pembeni kwenye kinyang’anyiro cha uenyekiti Kanda ya Kaskazini, amefichua kuwa awali mkakati ulikuwa ni kumwachia Mbowe aendelee kugombea nafasi hiyo na Lissu aendelee kugombea umakamu mwenyekiti, huku yeye na wenzake wakiendelea kugombea uenyekiti kwenye kanda walizokuwepo.

“Wakati huo tumekubaliana kama brothers (ndugu) kwamba Heche kagombee Serengeti, wewe maintain (ubaki) nafasi yako, Lissu umakamu mwenyekiti, mwenyekiti aendelee na tukasema tutasaidiana,” amesema Lema. 

Hata hivyo, amedai kuwa baadaye walibaini kuwepo kwa mbinu chafu za baadhi yao kuenguliwa kwenye nafasi zao walizopanga kuendelea kugombea.

“Missions (mipango) ilianza kutuondoa kwenye uongozi, mimi (Lema), John Heche, (Tundu) Lissu, (Ezekia) Wenje pamoja na (Mchungaji Peter) Msigwa. 

“Ikaanza mission (mipango) ya kutuengua, nikaiona kwangu kila nikipanga kazi ya chama inakuwa ngumu, naambiwa huyu anajipanga kwa uongozi.  Nikamwambia mwenyekiti (Mbowe), naona kazi zangu zinakuwa ngumu kama kuna maelekezo umeyatoa hebu yaondoe, akasema tutakutana tuongee, haikufanikiwa,” amedai Lema huku akimshauri Mbowe kufuata ushauri wa familia wa kumtaka kujiweka pembeni badala ya kusikiliza wanachama waliomfuata nyumbani kwake kumuomba agombee.

Lema ameendelea kudai kuwa alikuwa akitumia muda mwingi kumshauri Mbowe kuhusu mwenendo wa chama kutokana na kuanza kuona sintofahamu, lakini ushauri wake haukutekelezwa.

“Nikamwambia mwenyekiti, napata mishale mingi, naomba tukutane na Lissu. Wakaja Arusha kwangu nikawaomba Mwenyekiti, Lissu, Wenje, Heche nao waje,” anabainisha moja ya kikao walichoketi jijini Arusha. 

“Lissu akasema baada ya kikao, Mwenyekiti tunaona una shida, rekebisha hizo shida, tunaona ulimi umekuwa soft (laini), rekebisha hiyo. Mwenyekiti kama unatuhakikishia kuwa uko genuine, fomu utakauyogusa sitagusa, hayo maneno alimwambia tunakula chakula.

“Akamwambia mwenyekiti, unataka Lema aondoke, Msigwa aondoke, Heche aondoke, mimi niondoke, nani akufanyie kampeni za urais? Lissu akasema, wewe na Msigwa mlinisaidia mimi kubeba damu kwenye ndege mpaka Nairobi, nawaheshimu,” anasimulia Lema. 

Amesema baada ya maelezo ya Lissu, yeye alimwita Mbowe nje akamshauri kwamba wakutane tena nyumbani kwa Mbowe kesho yake ili wakazie mazungumzo kwa kula nyama choma.

“Tukaenda kwa mwenyekiti. Lile wazo lilikuwa langu, tukala nyama kabisa kwamba mna commit covenant. Tukatawanyika,” amedai Lema.

Hata hivyo, amesema mambo hayakubadilika, kwani wakati huo uliibuka mvutano kati ya Mwenyekiti wa Kanda ya Nyasa, Joseph Mbilinyi maarufu Sugu na Mchungaji Msigwa.

Hapo napo, Lema amedai kuwa alimshauri Mbowe awapatanishe mapema kabla ya mambo kuharibika, akiwa Dar es Salaam, Tunduma na Sumbawanga.  

“Nikamwambia mwenyekiti, huu msuguano wa Sugu na Msigwa unakipasua chama, mwondoe Msigwa, mwambie hivi nitakuchagua kuwa mjumbe wa kamati kuu au tutafanya kazi pamoja, kwa sababu anaona una hasara naye na ana wasiwasi mpaka na kiti chake cha ubunge,” amedai Lema.

Hata hivyo, Lema amesema Mwenyekiti hakutilia maanani, jambo analodai kuwa chanzo cha Msigwa kutimkia CCM.

“Naweza kusema kwa sauti, uchaguzi wa Nyasa ulikuwa mbaya kuliko uchaguzi wa Tamisemi, Msigwa ameonewa, uchaguzi ule ulifanyika kihuni ili Msigwa ashindwe.

“Ndio maana nili-tweet, nikasema nimeumia kwa kitu ambacho Msigwa amefanyiwa na ataondoka siku sio nyingi,” amedai Lema huku akifuta jasho.

Licha ya kubainisha dalili za Mchungaji Msigwa kuondoka, Lema amesema aliumia kusikia rafiki yake huyo ametimkia CCM.

Lema amesema hakuishia hapo, bali eliendelea kumshauri Mbowe kupatana na viongozi wenzake, lakini ushauri wake uligonga mwamba.

“Wakati tukiwa kwenye operesheni Kanda ya Kaskazini, nilimpigia simu mwenyekiti nikakwambia muite Mchungaji Msigwa, muite Heche na Lissu, mimi nitashuka kwenye helkopta kwenye hiyo operesheni.

“Zunguka na Heche na Msigwa kujenga bond kuonyesha watu kwamba hatuna ugomvi. Mwenyekiti akanijibu kuwa Heche anaweza kuja, Lissu nimeshaongea naye, lakini Msigwa sitaki kumwona naomba umfikishie salamu na mimi kama mtumishi wa Bwana nikamwambia bro (kaka) hutakiwi kuonekana. Msigwa akasema haya,” amesema Lema huku akisisitiza kuwa kama uchaguzi utakuwa huru na haki, Mbowe hawezi kushinda.

Msigwa alipotafutwa kwa simu, alisema maelezo ya Lema ni sahihi. “Hayo mambo nimekuwa nikiyasema mara kwa mara. Kimsingi nilishayaona mapema, nikawashauri wenzangu tutoke hadharani tuyaseme, ila hawakukubali.”

Wakati hayo yakiendelea, Lema anasema alipokea simu kutoka kwa Heche akimwambia kuwa Mbowe amemwambia Bob Wangwe agombee uenyekiti wa Kanda ya Serengeti na atamuunga mkono.

Lema amesema alimpigia simu Bob Wangwe, ambaye alimthibitishia maneno hayo na ndipo alimpomtafuta Mbowe kuzungumzia suala hilo ambapo walikutana Dar es Salaam.

“Nikamwambia kwamba Heche amenipigia anasema amepigiwa na mdogo wake Bob Wangwe akisema umemtaka agombee uenyekiti Serengeti.

“Nikasema, kama ulikuwa unatafuta mgombea wa Serengeti mtu wa kwanza kufikiria angekuwa ni Bob Wangwe au Heche? Heche ni super brand, amekuwa mbunge, amekuwa diwani amekuwa mwenyekiti wa vijana, amekuwa mjumbe wa kamati kuu. Mwenyekiti unaondoaje brand zako zote ndani ya chama?” amehoji Lema.

Mwananchi lilipomtafuta Bob Wangwe kumuuliza kuhusu kauli ya Lema, alisema: “Ni kweli Mbowe aliniomba nigombee uenyekiti wa kanda.”

Hata hivyo, Wangwe amesema hakuona busara kushindana na kaka yake- Heche.

Kwa upande wa Heche alipotafutwa na Mwananchi kuhusu kauli ya Lema amesema, “Yote aliyosema Lema ni kweli. Tumekaa vikao kadhaa hadi tukaunda kundi la Washauri.”

Wenje na tuhuma za kujiengua

Kwa mujibu wa Lema wakati wakiendelea na vikao vya usuluhishi, walishangaa kuona Wenje hahudhurii ikiwemo kikao kimoja ambacho kilidaiwa kuitishwa na Wenje mwenyewe.

Katika kikao hicho, Lema amedai kuwa akiwa na Lissu alilalamika kuwa amebaini kuwepo mpango wa kumhujumu kisiasa.

Wakati wakiwa wameshakubaliana kuwa Lissu ataendelea kugombea umakamu mwenyekiti, wakashangaa kuona Wenje akitangaza kugombea nafasi hiyo.

“Kuna siku Lissu akanipigia simu akasema Wenje anachukua fomu ya kugombea umakamu mwenyekiti, hebu mshauri Wenje asifanye hiyo press (mkutano na waandishi) anayotaka kufanya,” amesema Lema.

Hata hivyo, Lema amesema kuwa alichukua jukumu la kumshauri Mbowe kuzungumza na Wenje ili kumzuia kutoa tangazo hilo, lakini haikufanyika hivyo na mkutano wa kutangaza nia ukafanyika.

“Kabla Wenje hajafanya press (mkutano na wanahabari), nikamwambia mwenyekiti Wenje anachukua fomu, mzuie asifanye kitu. Mwenyekiti akaniambia mpigie wewe, nikampigia Wenje, tuliambiana, nikamwambia acha huo upuuzi, akasema ni demokrasia. Nikasema ni sawa kwa chama cha harakati, acha hicho kitu anachotaka kufanya,” ameongeza Leman a kuongeza: Nikamrudia Mbowe kumweleza alichojibu Wenje, lakini hakuchukua hatua na akatangaza nia yake.

Akizungumza na Mwananchi kuhusu kauli za Lema, Wenje ametetea uamuzi wake wa kugombea umakamu mwenyekiti, akisema ndio demokrasia.

“Hivi mimi kugombea umakamu mwenyekiti ni dhambi? Hao wanaopinga ni madikteta wakati wanahubiri demokrasia,” amesema Wenje.

Amesema kuwa Lema anatoa kauli hizo kwa kuwa ameshapoteza umaarufu na ameona hakubaliki tena na ndio maana ametoa matamko ya kutogombea.

“Nimemsikia Lema akisema Mbowe akishinda uwenyekiti hagombei ubunge, kwani alipokuwa mbunge kwa miaka 10 alikuwa chini ya mwenyekiti gani?. Kwanza Lema ni mwanachama tu, mamlaka yake ya nidhamu ni tawi, mimi ni mjumbe wa kamati kuu sioni hata kwa nini nimjibu,” amesema Wenje.

Alipoulizwa kuhusu vikao walivyokuwa wakikaa kwa ajili ya usuluhishi, Wenje amedai kuwa Lema na wenzake walitaka kumpindua Mbowe kwenye nafasi ya uenyekiti.

“Kama kuna watu walitakiwa kuchukuliwa hatua za kinidhamu ni Lema na genge lake. Kwa sababu walianzisha kitu kinachoitwa Join the Chain na walilenga kumpindua mwenyekiti wakati yuko gerezani,” amedai na kuongeza, “Mimi nilishtuka nikajiondoa.”

Wenje amekosoa pia mapendekezo ya Lema aliyetaka Katibu Mkuu wa zamani wa chama hicho, Dk Wilbrod Slaa kurejeshwa kwenye chama.

“Huyo Dk Slaa ndiye aliyeandika kitabu cha kuikashifu Chadema, halafu leo ndio arudishwe kwenye chama?”

Sababu za Lissu kugombea uenyekiti

Kwa mujibu wa Lema, baada ya Wenje kutangaza nia kugombea umakamu mwenyekiti, ndipo Lissu naye akaamua kugombea uenyekiti, jambo ambalo aliliona tangu awali kuwa litaleta mvutano.

Amesema alimshauri Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika kuhusu suala hilo akimtaka aitishe kikao cha dharura cha Kamati Kuu, lakini alijibiwa kuwa chama hakina fedha.

Mnyika alipoulizwa suala hilo, alijibu kupitia WhatsApp akisema: “Katika kipindi hiki ambacho katibu mkuu pamoja na kuwa mtendaji mkuu wa chama ni msimamizi wa uchaguzi hivyo, kauli yangu kujibu baadhi ya madai yanayotolewa na wagombea au wanaowaunga mkono ya kweli au ya uongo inaweza kuwa na athari, taathira au madhara katika mchakato wa uchaguzi.

“Hivyo, yapo nitakayoyajibu iwapo nitaulizwa kwenye Baraza Kuu na Mkutano Mkuu kama sehemu ya mjadala wa Taarifa ya Utendaji ya Miaka Mitano na mengine msubiri mniulize nitayajibu katika wakati muafaka.” amesema

Related Posts