Dar es Salaam. Aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Kanda ya Kaskazini, Godbless Lema amesema kama uchaguzi wa mwenyekiti ndani ya chama hicho utafanyika kwa uhuru, uwazi na haki basi Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe hawezi kushinda.
Lema ambaye ametangaza msimamo wake wa kumuunga mkono makamu mwenyekiti wa Chadema-Bara, Tundu Lissu kwenye kuwania nafasi ya mwenyekiti Taifa, amesema wanachama wengi waliopo kwenye ngazi za maamuzi wanamuunga mkono Lissu.
“Ninachowaambia ni kuwa kama uchaguzi utakuwa huru na haki, mwenyekiti (Mbowe) hawezi kushinda take my word. Yaani mwenyekiti ana watu wachache sana wanaomuunga mkono,” amesema Lema wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, leo Januari 14, 2025.
Desemba 22, 2024, Mbowe akizungumza baada ya kurejesha fomu makao makuu ya chama Mikocheni kuwania nafasi hiyo, aliziagiza mamlaka zinazosimamia uchaguzi wa chama hicho, kutenda haki ili ipatikane safu bora, yenye sifa na inayokubalika kuongeza.
“Naziagiza mamlaka za chama zinazohusika kusimamia mchakato mzima wa uchaguzi huu, zihakikishe uchaguzi wetu unafanyika vizuri na usiwe na doa, uwe wa uwazi, kila mtu aone, dunia ione, Chadema tunaweza kuchaguana bila kufanya wizi wa kura.
“Wizi wa kura si asili ya Chadema, ili yeyote atakayepatikana akawe halali si tu mbele ya wana Chadema, bali hata kwa Mungu,” alisema.
Tayari kamati kuu ya Chadema imekwishateua Kamati ya Wazee Wastaafu wa chama hicho watakaosimamia uchaguzi.
Walioteuliwa ni Ahmed Rashid, Alfred Kinyondo, Profesa Azaveli Lwaitama, Wakili Edson Mbogoro, Francis Mushi, Lumuli Kasyupa, Profesa Raymond Mosha na Ruth Mollel aliyewahi kuwa Katibu Mkuu Utumishi.
Endelea kufuatilia Mwananchi.