Maboresho mapya Sera ya Elimu kutatua changamoto za elimu?

Dar es Salaam. Ijumaa Januari 11, 2025 Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, alitangaza kuidhinishwa kwa Sera ya Elimu na Mafunzo ya 2014 toleo la 2023, inayotarajiwa kuzinduliwa rasmi mwishoni mwa Januari 2025.

Sera hiyo ambayo utekelezaji wake ulianza mwaka 2024, itazinduliwa na Rais Samia Suluhu Hassan.

“Mageuzi yaliyopo katika sera ni makubwa na yanatekelezwa kwa awamu, tutakuwa tunaona kila mwaka hatua ambazo zinachukuliwa. Haya ni mabadiliko yatakayogusa vizazi na vizazi,”alisema Profesa Mkenda.

Kwa mtafiti na mdau wa elimu, Dk Godfrey Telli hatua hii ni kubwa kwa elimu ya Tanzania, akieleza kuwa mabadiliko haya yalitakiwa yatokee mapema zaidi.

“Elimu yetu ilipokuwa imefikia ukienda mtaani ukiangalia wananchi wanafanya shughuli za ujasiriamali kama biashara, kutengeneza sumu na nyingine ambazo haziendani kabisa na vile watu hawa walifundishwa darasani” anasema.

Afafanua kuwa mara nyingi jamii ndio inatakiwa ifuate kile kilichopo kwenye elimu na sio elimu ifuate kilichopo mtaani, akisisitiza licha ya kuchelewa lakini ni hatua nzuri.

“Mtalaa umekuja kwa kuangalia uhalisia wa kinachohitajika mtaani. Ilitakiwa iwe kinyume chake lakini hatujachelewa” alifafanua.

Wakati waziri akitangaza uzinduzi wa sera hiyo, awali Januari mwaka 2024, aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dk Franklin Rwezimula alisema jumla ya shule 96 za sekondari teule zingeanza utekelezaji wa kutoa masomo ya amali, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa mitalaa mipya ya elimu iliyoboreshwa.

Changamoto masomo ya amali, biashara

Licha ya kwamba mtalaa ndio unaanza zipo shule ambazo tayari zilikuwa zinafundisha masomo haya. Hata hivyo uchunguzi wa gazeti hili kwenye matokeo ya mitihani yaliyotoka hivi karibuni yameonyesha wanafunzi wengi kuanguka kwenye masomo hayo.

Jambo hili linawaibua wadau wa elimu wakitaka Serikali kuhakikisha kuna wataalamu wa kutosha watakao fundisha masomo haya ili wanafunzi wapate ujuzi unaokusudiwa.

Mfano matokeo ya mtihani wa upimaji kidato cha pili 2024 yaliyotolewa na Baraza la Mitihani la Taifa (Necta) yameonyesha kuwapo kwa ufaulu hafifu katika baadhi ya masomo, ikiwemo kilimo ambapo asilimia 65.5 ya watahiniwa wanaosoma somo hili walipata daraja F.

Masomo mengine ambayo wanafunzi walipata F kwa wingi ni mazoezi ya viungo asilimia 74.76, uhandisi wa barabara asilimia 40.10, useremala na upakaji rangi asilimia 40.8. Pia uchumi asilimia 37.03, sayansi ya uhandisi asilimia 48.54.

Mbali na masomo haya ambayo huenda ndiyo mara ya kwanza kwa baadhi ya wanafunzi kujifunza, kwa yale ya biashara ambayo ni Commerce na Book-keeping ufaulu wake ulikuwa kwa asilimia 56.23 na asilimia 48.49 mtawalia.

Akizungumzia ufaulu huo, mdau wa elimu, Muhanyi Nkoronko anasema kufeli kwa wanafunzi katika masomo haya kunasababishwa na kukosekana kwa walimu.

Anasema ukosefu wa walimu unatokana na jambo linalofundishwa huenda kuwa jipya au walimu waliokuwapo hawakuwa wengi kutosheleza kutoa maarifa stahiki kwa ajili ya kuwapa wanafunzi.

“Tunashindwa kuzalisha watu watakaoweza kujitegemea huko baadaye, kuwe na mpango wa kuongeza walimu watakaokuwa na uwezo kwa kufundisha masomo hayo baadaye. Huenda waliopo wanamudu lakini ni wachache hivyo kushindwa kumfikia mwanafunzi mmoja mmoja, anasema Nkoronko.

Anasema ili kufanikisha hilo ni vyema Serikali ikaangalia namna ya kushirikiana na vyuo vya ualimu ili kuzalisha walimu wanaotakiwa kwa ajili ya kufundisha masomo yaliyopo.

“Pia kuangalia namna ya kuongeza vitabu vya kiada na ziada, ambavyo vinaweza kuwasidia wanafunzi kusoma ili waweze kupata maarifa mbalimbali,” anaeleza.

Mdau mwingine, Nicodemus Shauri anataja ugeni wa masomo haya kwa wanafunzi inaweza pia kuwa kikwazo. Akizungumzia mapokeo ya wanafunzi katika masomo haya, anasema wanasimama kama wanafunzi wa majaribio kwa kuanza kujifunza kitu kipya.

“Unajua katika ujifunzaji wanafunzi huwa wanatumia mitihani iliyopita kujifunza, sasa hawa kwa sababu ndiyo wa kwanza hakuna kitu cha nyuma wanachoweza kukisoma ili kuongeza uelewa wao na sidhani kama kuna vifaa vya kufundishia toshelezi,” anasema.

Katika kuboresha ufundishaji wa masomo haya, Shauri anasema katika kila kitakachofanyika, ni bora wanafunzi wapate ufaulu wa alama D kuliko F.

“Tuhakikishe walimu wanaajiriwa wa masomo hayo, vitabu vya kufundishia na kujifunzia vipatikane shuleni na kama ni masomo ya amali tuhakikishe wanafunzi wanajifunza kwa vitendo,” anasema.

Changamoto zitatatuliwa na muda

Akifafanua kuhusu changamoto za wataalamu na miundombinu Telli, anasema: ”Hatuwezi kuanza kitu bila changamoto, mfano shule za msingi pekee zina wanafunzi zaidi ya milioni 10 kama nusu wataenda kwenye mtaala wa amali that’s huge (hiyo ni kubwa sana), kuna mahitaji mengi kama madarasa, vifaa na wataalamu sio rahisi kuvimaliza kwa haraka lakini ni mwanzo mzuri”.

Telli anaongeza kuwa nchi ilikuwa inakosa mwitikio wa kisiasa kwenye kubadilisha mfumo wa elimu lakini sasa hilo halipo.

“…Sasa tunaona political will (utashi wa kisiasa) na wizara tunaona imekuja na taratibu nyingi za kuwapata wataalamu, sasahivi watu wanafuatwa Veta.Kumewekwa taratibu wataalamu wale hat walio mtaani wanaendelezwa na kupatiwa vyeti ili waje kufundisha. Naamini kabisa mpaka 2027 mambo yataanza kubadilika” anafafanua.

Ajira walimu, wataalamu masomo ya amali

Kuhusu suala la kuajiri walimu, Serikali imeendelea kufanya jitihada mbalimbali katika kushughulikia suala hilo ambapo imekuwa ikitangaza nafasi za kutafuta walimu wa masomo haya kwa nyakati tofauti.

Kwa mfano, Desemba 13, 2024 Serikali ilitangaza nafasi 3,633 za ajira za ualimu huku nyingi zikiwa za masomo ya amali. Ajira hizo zinarandana na mabadiliko ya sera, ambayo imetoa kipaumbele katika elimu ya amali kama mbinu mojawapo ya kukabiliana na tatizo la ajira kwa wahitimu

Nafasi hizo zilitangazwa kupitia Sekretarieti ya Ajira huku walimu waliokuwa wakihitajika kupitia tangazo hilo ni wale wa masomo ya biashara, ushonaji, uashi, umeme, ufundi magari, uchomeleaji na uundaji vyuma, sanaa, useremala, ufundi bomba, afya ya wanyama na uzalishaji chakula.

Wengine ni wa masomo ya kilimo na bustani, huduma ya chakula, upakaji rangi, umeme wa magari, jokofu na vipoza hewa, nishati ya jua, tehama, uvuvi, usindikaji mbao na mazoezi ya viungo.

Wadau na utekelezaji wa mtalaa

Akizungumza na Mwananchi, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), Dk Paul Loisilie anasema mabadiliko yaliyofanyika katika sekta ya elimu ni makubwa na hivyo yanahitaji watu kujitolea kwa hali ya juu kuliko hivi sasa katika kufanikisha utekelezaji wake.

Anasema jambo la kwanza linalotakiwa kufanyika ni wadau kuwa na nia, kwa sababu hiyo ndiyo itakayowawezesha kushinda changamoto zilizopo kwenye hatua mbalimbali za utekelezaji.

“Jambo la pili ni hamasa, Serikali ilete hamasa kwa walimu hasa mshuleni na sio vitisho, walimu waonyeshwe wana uwezo na wanaungwa mkono na Serikali katika kutekeleza mtalaa mpya. Bila hamasa yatakuwa ni mambo ya kawaida,”anasema.

Dk Loisulie anasema jambo jingine linalotakiwa kufanyika ni kutenga raslimali za kutosha katika utekelezaji wa sera na mtaala kwa kuwa kuna baadhi ya maeneo yanahitaji vifaa.

“Jamii nzima pia ione kuwa jambo hili lina faida, isionekane kuwa ni kitu kilicholetwa tu bali iwe tayari kupokea na kutumia kwa mtazamo chanya,”anasema.

Naye, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha St John, Dk Shadidu Ndossa anasema miundombinu na watalaamu, ni muhimu katika utekelezaji wa mtaala, kwani tawaasaidia wanafunzi kupata maarifa kwenye mageuzi hayo.

“Matumizi ya teknolojia ni jambo la muhimu, hata kama hatuwezi kupata walimu wa kutosha kufundisha, kuna baadhi ya mambo ambayo hata kama hatuna vifaa vya kufundishia lakini teknolojia inaweza kurahisisha sana,”anaeleza. Anaongeza; “Tunategemea shule nyingi ambazo zimeunganishwa na umeme, pamoja na intaneti ili hata kama kuna mwalimu mmoja aweze kufundisha shule 15 hadi 20.”

Kwa upande wake, Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Bakari Mtembo anasema iwapo watu watakaosimamia utekelezaji wa mabadiliko hayo makubwa ya elimu watakuwa na nia kama waasisi basi sekta hiyo, itapiga hatua kubwa.

“Tunatekeleza hiki kitu lakini walimu wamepewa uwezo? Hapa kwenye kujaza uwezo wa walimu kuna changamoto, walimu wengi wanafundisha kwa nadharia. Ukimwambia mwalimu akifundishe kwa vitendo inaweza kuwa mtihani mkubwa kwake,”anasema.

Hata hivyo, anasema kwa upande miundombinu Serikali imejitahidi, huku akitoa ushauri wa kuwapo kwa nyumba za walimu kama miongoni mwa vigezo vinavyotakiwa kutekelezwa kabla ya usajili wa shule mpya.

Related Posts