Tumemaliza msimu wa sherehe za Krismasi na Mwaka Mpya, lakini wazazi bado hawajasahau makovu ya gharama za mahafali ya wahitimu, huku suala la majoho kwa wahitimu likizidi kuchukua sura mpya katika mitandao ya kijamii.
Badala ya kutumia majoho kwenye mahafali, taasisi nyingine mbali na vyuo vikuu zilienda mbali zaidi kuhamasisha watoto kushona suti, ambazo zilikuwa ni za gharama kubwa.
“Mimi nashangaa majoho haya yalitoka wapi na mzazi unalazimika kulinunua bila kuuliza, maana mtoto asipofanana na wenzake wakati umegharamia miaka yote ada na michango kedekede, unaona ngoja hata hili liishe, joho kulikodi ni Sh50, 000 pengine ukilazimika ushone ni laki moja,” anasema Devotha Paul ambaye mtoto wake amehitimu kidato cha nne mkoani Shinyanga.
Uvaaji wa majoho ya kitaaluma ni utamaduni wa kihistoria wenye mizizi mirefu inayotokana na mfumo wa elimu ya juu katika ulimwengu wa Kiislamu.
Mwaka 841, chuo kikuu cha kwanza barani Ulaya kilianzishwa na Waislamu katika mji wa Salerno, Italia.
Chuo hiki kilikuwa mwendelezo wa vyuo vikuu vya Kiislamu vilivyokuwa Mashariki ya Kati, ambavyo vilijulikana kwa ubora wake wa elimu na sayansi.
Baadaye, vyuo vya Toledo, Seville, na Granada vilifuata, vikichukua nafasi muhimu kama vituo vya maarifa.
Wakati wanafunzi wa Ulaya (wasio Waislamu) waliposoma katika vyuo hivi, walichukua si tu maarifa ya kitaaluma bali pia tamaduni mbalimbali, ikiwa ni pamoja na mavazi.
Waliporudi katika nchi zao, walihifadhi desturi ya kuvaa mavazi yaliyofanana na ya Waarabu/Waislamu, kama vile thawb au qamees, mavazi mapana na yenye heshima. Mavazi haya yaliwakilisha hadhi ya kielimu na mafanikio ya kitaaluma.
Tamaduni hii baadaye iliingizwa katika vyuo vya Ulaya, hasa wakati wa kuhitimu na hafla za kitaaluma, ambapo mavazi ya joho yalionekana kama alama ya mafanikio na heshima ya kitaaluma.
Kitabu ‘Islam in Europe’ cha Goodwin kinaeleza kuwa mavazi ya Kiarabu yalibaki kuwa ishara safi ya uadilifu wa kielimu, hasa wakati wa matukio muhimu kama midahalo ya kitaaluma na mahafali.
Historia inaeleza wazi kupitia mwanafalsafa Placid Tempes kwamba, katika karne ya 12 na 13, vyuo vikuu vya Ulaya kama Oxford, Cambridge, na Bologna vilianza kutumia majoho kwa lengo la kubainisha hadhi za kitaaluma na kijamii.
Vyuo hivi viliongozwa na misingi ya kidini, na hivyo mavazi hayo yalichukua nafasi kama alama za heshima na dini. Kadri muda ulivyopita, rangi, mapambo, na mitindo tofauti ya majoho yalianza kutumiwa kutofautisha ngazi mbalimbali za kitaaluma, hivyo kuimarisha dhana ya matabaka ya kielimu.
Desturi ya uvaaji wa majoho iliingizwa barani Afrika kupitia ukoloni, ambapo ilionekana kama sehemu ya mfumo wa elimu ulioletwa na wageni.
Majoho yalipewa nafasi ya kuwa alama ya maendeleo na ustaarabu. Hata hivyo, utamaduni huu ulipokelewa kwa maoni mseto. Wengi walihoji sababu ya kuiga tamaduni za kigeni ambazo hazikujikita katika mizizi ya Kiafrika.
Marufuku ya mojoho shuleni
Novemba 2016, aliyekuwa Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako, alitangaza marufuku ya matumizi ya majoho katika sherehe za mahafali kwa ngazi za chini za elimu.
Kauli hiyo iliwashangaza wengi, hasa ikizingatiwa kuwa haikufuatwa na waraka wowote rasmi kutoka serikalini.
Kwa mtazamo wa wengi, ilikuwa ni tangazo la kisiasa lililofanana na kauli yake nyingine ya mwaka huo huo aliposema masomo ya sayansi yatakuwa ya lazima katika ngazi zote za elimu, ingawa hakukuwa na miongozo ya utekelezaji.
Profesa Ndalichako alieleza kuwa majoho yanapaswa kuvaliwa kuanzia ngazi ya shahada ya kwanza, ambapo yanakuwa na maana halisi ya mafanikio ya kitaaluma.
Alibainisha kuwa utamaduni wa kutumia majoho katika ngazi za chini, ulikuwa unachochea mgawanyiko wa kitabaka kwa sababu familia zenye kipato kidogo, zilikuwa zikilazimishwa kugharamia mavazi hayo, mzigo ambao mara nyingi haukuwa wa lazima.
Kauli hiyo ilizua hisia mseto kutoka kwa wazazi, walimu, na wananchi kwa ujumla. Wapo waliounga mkono hatua hiyo, wakisema kuwa ingehamasisha wanafunzi wa ngazi za chini kujitahidi zaidi kufikia elimu ya juu.
Wengine walihisi kuwa hatua hiyo ilikuwa ya kukandamiza furaha ya wanafunzi na wazazi ambao walikuwa wamezoea kusherehekea mafanikio ya kielimu ya watoto wao kupitia mavazi ya majoho.
Kwa upande mwingine, baadhi ya wachambuzi wa masuala ya elimu waliona kuwa tatizo halikuwa mavazi ya majoho pekee, bali pia wingi wa shule na taasisi zilizokuwa zikiiga tamaduni hizo bila kuelewa historia na muktadha wake. Wengi walikubaliana kuwa desturi hiyo ilikuwa ikipoteza maana yake ya asili na kuwa burudani isiyo na tija ya kielimu.
Aliyekuwa mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Tumaini Makumira, Dr Eliawony Meena, aliwahi kusema enzi za mkoloni walipomaliza shahada ya kwanza walilazimika kuanza kufundisha darasani wakiwa wamevalia majoho (academic regalia) kama wako bado kwenye mahafali kama ishara ya kujitofautisha na wafanyakazi wengine ambao hawakufikia ngazi hiyo ya elimu.
Alisema elimu ya chuo kikuu kwa wakati huo ilikuwa ni ya fahari kubwa tofauti na sasa.
“Aaaaah bwana mdogo…, unajua enzi zetu wakati wa mkoloni ilikuwa ukiingia darasani kama mnavyoniona sasa ilibidi nivae joho la mahafali na wakati huo vitabu vya riwaya kama vya kina Chinua Achebe, tulikuwa tukiviningi’niza kwenye mikanda ya suruali ndani ya mabasi ya umma watu watufahamu tulivyo wasomi.Elimu ilikuwa kitu cha thamani sana kiasi kwamba usingeweza kuvaa joho kiholela. Sasa hivi…mmm majoho hadi chekechea wanavaa pasipo kufahamu misingi yake, japo ni ukoloni ndio uliotufikisha hapa na kutupelekea kuthamini kazi za mishahara,” alisema Dk Meena.
Marufuku iliyokosa uhalali
Ukweli ni kwamba hakukuwa na waraka wa utekelezaji wa kauli ya Profesa Ndalichako, na hivyo kufanya marufuku hiyo kubaki kama tangazo la kisiasa lisilo na nguvu ya kisheria. Shule nyingi, hasa za binafsi, bado zinaendeleza utamaduni wa kutumia majoho katika mahafali ya wanafunzi wa shule za awali na msingi, huku baadhi ya wazazi wakilalamikia mzigo wa gharama.
Lakini wanafunzi wanalipokea hilo suala kama namna bora ya kuthamini kila ngazi ya elimu waliyofikia, huku wakitanabaisha kwamba majoho huwafanya watamani kufikia huko juu walipo wengine.
“Unajua mzee, mimi sioni tabu kuvaa joho, kwanza ni utambulisho kwamba hata kwenye familia yetu wasomi wapo… naona wanaotukataza kuvaa majoho kama huyo Profesa ni ukiritimba usiokuwa na maana,” anasema Denis Daudi, mhitimu wa kidato cha nne wilayani Kahama.
Chacha Mwita, mwanafunzi wa mwaka wa tatu katika Chuo Kikuu cha Sokoine mkoani Morogoro, anasema kuwa uvaaji wa majoho kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari umepoteza maana halisi ya mafanikio ya kitaaluma.
“Majoho yanapaswa kuwa alama ya mafanikio makubwa, hasa katika ngazi za juu kama shahada ya kwanza. Kuwavalisha watoto wa chekechea na shule za msingi ni kama kudhihaki maana ya elimu. Hili linaondoa motisha ya kujitahidi kufika ngazi ya juu,” anasema Chacha kwa msisitizo.
Naye Esther Mwakalinga, mwanafunzi wa mwaka wa pili wa sheria katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, anahisi kuwa gharama zinazohusiana na mavazi haya ni mzigo usio wa lazima kwa wazazi.
“Familia nyingi zinahangaika kupata mahitaji ya msingi, halafu wanatakiwa kugharamia mavazi ya majoho kwa sherehe ambazo hazina tija kielimu. Hii inakuwa mzigo usio wa lazima na inawafanya baadhi ya wazazi kuhisi aibu ikiwa hawawezi kumudu,” anasema Esther kwa huzuni.
Mjadala wa uvaaji wa majoho unaonyesha haja ya kutafakari upya thamani ya tamaduni za kielimu barani Afrika.
Ingawa ni muhimu kusherehekea mafanikio ya kielimu, ni lazima kuhakikisha kuwa sherehe hizo haziathiri familia kwa gharama zisizo za lazima au kuchochea matabaka ya kijamii
Taifa linapaswa kufikiria njia za kuimarisha elimu kwa njia inayothamini utambulisho wa Kiafrika, huku ikipunguza kasumba ya kigeni ambayo mara nyingi haina maana halisi katika muktadha wa Kiafrika.