MBUNGE ABOOD ATOA WITO WA KUTATUA CHANGAMOTO ZA WENYEVITI WA SERIKALI ZA MITAA

Farida Mangube, Morogoro 

Mbunge wa Jimbo la Morogoro Mjini, Abdul Azizi Abood, ameiomba Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro kuchukua hatua madhubuti katika kutatua changamoto zinazowakumba wenyeviti wa serikali za mitaa, akisema baadhi yao wamekuwa wakihusishwa na migogoro inayokwamisha maendeleo ya jamii.

Abood alitoa wito huo wakati wa hitimisho la mafunzo maalum kwa viongozi wa serikali za mitaa yaliyofanyika mjini Morogoro. Mafunzo hayo yalilenga kuwajengea uwezo viongozi hao katika kusimamia fedha za miradi, kujiepusha na rushwa, kuimarisha utawala bora, na kuboresha usimamizi wa ardhi ili kukuza demokrasia na maendeleo endelevu.

“Ni muhimu kuwa na viongozi waaminifu, wenye maadili, na wenye uwezo wa kusimamia maendeleo ya wananchi. Changamoto zinazowakabili wenyeviti wa mitaa lazima zitatuliwe ili kupunguza migogoro ambayo inarudisha nyuma juhudi za maendeleo,” alisema Abood.

Kwa upande wake, Afisa Mipango Miji wa Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro, Yonah Mtawa, alisema mafunzo hayo ni hatua muhimu katika kumaliza migogoro ya ardhi na kuimarisha usalama wa nchi.

“Migogoro mingi ya ardhi inayojitokeza katika jamii inaweza kudhibitiwa kwa kutoa elimu na kujenga uwezo kwa viongozi wa mitaa. Mafunzo haya ni chachu ya kuboresha mahusiano na utulivu wa jamii,” alisema Mtawa.

Priscar Kimako, balozi wa mtaa wa Nguzo, alisema: “Tumepata elimu ya kutosha kuhusu utawala bora na usimamizi wa ardhi. Hii itatusaidia kutatua migogoro ya wananchi kwa ufanisi.”

Naye Justun Mkoba, mwenyekiti wa mtaa wa Bingwa Sokoni, alieleza: “Ni muhimu kwa viongozi wa serikali za mitaa kupewa mafunzo kama haya mara kwa mara. Yanatufanya tuwe na uelewa wa masuala ya kisheria na kiutawala.”

Abood amesisitiza kuwa serikali itaendelea kushirikiana na Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro kuhakikisha viongozi wa mitaa wanapata nyenzo stahiki za kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.

Related Posts