Dar es Salaam. Wakati wagombea wa uenyekiti wa Baraza la Vijana la Chadema (Bavicha) wakinadi sera zao, mmoja wao, Shija Shibeshi ametangazwa kujitoa na kumuunga mkono Deogratius Mahinyila.
Hatua ya Shibeshi kutangaza kujiondoa, inapigia msumari uamuzi wake alioutangaza tangu Januari 11, 2025 katika mdahalo uliowakutanisha wagombea wote wa nafasi hiyo, ambapo alisema atajiengua lakini mpaka uchaguzi unaanza kufanyika hakuwa amefanya hivyo.
Kujiondoa kwa Shibeshi, kunafanya wagombea wa uenyekiti wa Bavicha wabaki wawili, ambao ni Deogratius Mahinyila na Masoud Mambo.
Hata hivyo tangu awali, wawili hao ndiyo waliokuwa wanatajwa kuchuana katika kinyang’anyiro hicho,huku wakijipambanua mapema kwa kila mmoja kuunga mkono kambi yake kati ya Freeman Mbowe na Tundu Lissu.
Tayari tangu jana Jumatatu, kambi ya Lissu imekuwa ikimpigia kampeni hadharani Mahinyila akiwemo Lissu mwenyewe aliyetumia ukurasa wa kijamii wa X (zamani Twitter) kuwaeleza wajumbe wa mkutano mkuu kumchagua kwani anastahili.
Kambi la Mbowe nayo inapiga kampeni chini kwa chini dhidi ya Mambo.
Mkutano mkuu huo wa Bavicha ulianza jana asubuhi Jumatatu, Januari 13, 2025 na unaendelea leo asubuhi kwa wagombea kujinadi na kupigiwa kura.
Akizungumzia uamuzi wa kujitoa, Shibeshi amesema kiu yake ilikuwa kugombea ili kuleta mabadiliko ndani ya chama hicho na kuongeza msukumo wa mapambano.
Amesema maono yake ilikuwa ni kuliongoza baraza kwenye mapambano ya kudai Katiba mpya, kusukuma ajenda za baraza ikiwemo mabadiliko ya katiba ya Chadema.
“Sasa nilitamani kuwashawishi ninyi tukubaliane tutengeneze mfumo wa katiba yenye shirikisho la serikali tatu yaani Serikali ya Tanganyika, Zanzibar na Jamhuri ya Muungano,” amesema.
Amegusia pia vijana wengine ambao kwa sasa hawajulikani walipo na alikuwa tayari kuyaongoza mapambano ya kuwatafuta popote walipo.
“Nasema nilitamani kwa sababu, katika mdahalo tulioufanya, niliutangazia umma kwamba niliamua kujiondoa kwenye kinyang’anyiro cha kugombea.
“Naomba kutamka mbele yenu kuwa ninaamua kumuunga mkono Deogratius Mahinyila kwa sababu…,” amesema
Baada ya kauli hiyo, Mwenyekiti wa uchaguzi huo, Elisha Chonya alimwambia mgombea aishie kutangaza kujitoa na si kumpigia debe mgombea mwingine.
Hata hivyo, Shibeshi hakukubaliana na hilo hadi aliposema: “Mjumbe yeyote aliyetaka kunipigia kura, aache badala yake ampigie Deogratius Mahinyila.”
Ulipofika wakati wa Mahinyila kujinadi ameana kwa kusema kuwa amekuwa mtetezi wa chama hicho kisheria katika masuala mbalimbali.
Amesema atakapochaguliwa analenga kuifanya Bavicha kuwa baraza huru na litakalowasemea vijana.
Pia amesema ataifanya Bavicha kuwasemea vijana na kuwa na kitengo maalumu cha kuhakikisha hakuna kijana anayekamatwa, kupelekwa mahakamani kwa masuala ya kisiasa na akakosa wakili.
“Chama chetu kimejengwa katika misingi ya hoja, lazima tuwe na Bavicha yenye mafunzo na semina na yenye uhuru wa kiuchumi,” amesema.
Amesema atahakikisha baraza hilo linasimama kiuchumi kwa kuhakikisha kila pato linaloingia kwenye chama Bavicha inapata.
Ameeleza katika mikoa ya kusini ndiko atakakoanza ziara yake baada ya kuchaguliwa.
Amesema uchaguzi huo ndio utakaoamua hatima ya Chadema na kuipa uhai, hivyo vijana wanapaswa kuzingatia hilo.
“Mimi ni jasiri, mimi sio chawa, ni kijana ninayejitambua siwezi nikakubali jambo lolote hata ukiwa nani,” amesema.
Amesema atakaposhinda atatoa nafasi sawa kwa wanachama wote hata kama wapo wenye mitazamo tofauti.
Kwa upande wa Masoud Mambo amesema akichaguliwa analenga kuifanya Bavicha kuwa ya kimkakati yenye mpango A na B.
“Bavicha inapaswa kusimama barabarani na kuanzisha maandamano pasipo kusubiri tamko la viongozi wa juu, watakuja kutuzuia tukiwa tayari barabarani,” amesema.
Kwa mujibu wa Mambo, vijana wa Chadema wanakabiliwa na changamoto lukuki, atakachokifanya ni kuendeleza harakati za kudai Katiba Mpya na Tume Huru ya Uchaguzi.
Mambo amesema Bavicha imekosa uchumi na iwapo atachaguliwa atajenga uchumi imara ndani ya baraza hilo.
Amesema atalitekeleza hilo kwa kutumia fursa zilizopo katika mikoa mbalimbali, zitafanyika tafiti na kuona mradi gani ufanyike kuzalishwa chanzo cha mapato.
Mgombea huyo amesema ataandaa utaratibu utakaowezesha wajumbe wawe tayari wamesharatibiwa mapema kabla hata hawajafika eneo la mkutano.
Endelea kufuatilia Mwananchi kujua kinachoendelea.