Dodoma. Nchi 25 zinazolima kahawa barani Afrika zinakutana nchini Tanzania katika Mkutano Mkuu wa Tatu wa mwaka wa nchi zinazolima kahawa (IACO), kwa lengo la kujadili njia za kuongeza thamani ya zao hilo kwa miaka kumi ijayo kwenye soko la dunia.
Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe amesema hayo leo Jumanne Januari 14, 2025, jijini Dodoma alipozungumza na waandishi wa habari kuhusu mkutano huo utakaofanyika Februari 21 na 22 mwaka huu, Dar es Salaam.
Bashe amesema pamoja na nchi za Afrika kuzalisha asilimia 50 ya kahawa inayouzwa duniani, mapato yanayotokana na zao hilo bado ni madogo.
Amesema mapato ya jumla ya sekta ya kahawa duniani ni Dola 500 bilioni za Marekani kwa mwaka, lakini Afrika inachangia Dola 2.5 bilioni pekee.
“Asilimia 50 ya kahawa inayokwenda kwenye soko la dunia inatoka Afrika, lakini mapato yetu ni madogo kwa sababu tunazalisha na kuuza kahawa ghafi, tofauti na nchi nyingine zinazoongeza thamani kabla ya kuuza,” amesema Waziri Bashe.
Amesema licha ya mapato hayo duni, nchi za Afrika zinaagiza kahawa iliyoongezwa thamani kwa gharama ya Dola 6 bilioni za Marekani kwa mwaka, kiwango ambacho ni kikubwa kuliko mapato yanayotokana na kuuza kahawa ghafi.
Mojawapo ya ajenda kuu za mkutano huo ni kuweka mikakati ya kuongeza thamani ya kahawa inayozalishwa barani Afrika kwa miaka kumi ijayo ili kuongeza mapato na kunufaisha wakulima na nchi zinazolima kahawa.
Waziri Bashe amesema ushirikiano na sekta binafsi ni muhimu katika kufanikisha mabadiliko haya, kwa kuwashirikisha katika mnyororo wa thamani na kuwapa fursa za kuongeza thamani kwa kutumia masoko ya kimataifa.
“Serikali ya Tanzania, kwa upande wake inaendelea kuimarisha sekta ya kahawa kwa kuwasaidia wakulima,” amesema Bashe.
Amesema tayari miche milioni 20 ya kahawa imetolewa bure kwa wakulima kupitia ruzuku, ikiwa ni moja na mikakati ya kuongeza uzalishaji na ubora wa kahawa nchini.
Tanzania inapata Dola 200 milioni za Marekani kila mwaka kupitia sekta ya kahawa, lakini inafanya juhudi kushirikiana na sekta binafsi ili kuongeza thamani ya asilimia 50 ya kahawa inayozalishwa barani Afrika.
Mkutano huo unatarajiwa kuhudhuriwa na mawaziri wa kilimo, sekta binafsi, viongozi wa taasisi za kahawa, wakulima, na wadau wengine katika mnyororo wa thamani wa kahawa.
Kauli mbiu ya mkutano huo inasema: “Kufungua Fursa za Ajira kwa Vijana Kupitia Uboreshaji wa Sekta ya Kahawa Afrika.”
Bashe amesemamgeni rasmi katika mkutano huo atakuwa Rais Samia Suluhu Hassan.