Simulizi ajali iliyoua 11 wakiokoa majeruhi

Dar/Tanga. Ni siku zisizozidi 20 zikichukua maisha ya watu 30 kutokana na ajali za barabarani zilizotokea kati ya Desemba 24, 2024 na Januari 13, 2025, wilayani Handeni Mkoa wa Tanga.

Ajali tatu zilizotokea wilayani humo pia zimesababisha majeruhi zaidi ya 35.

Katika tukio la hivi karibuni, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Almachius Mchunguzi amesema ajali imetokea Januari 13, 2025 usiku na kusababisha vifo vya watu 11 na majeruhi 13 waliokuwa wakiwaokoa majeruhi wa ajali nyingine.

Rais Samia Suluhu Hassan, alipotoa salamu za Mwaka Mpya kwa Watanzania Desemba 31, 2024, alisema mwaka 2024 Tanzania ilikumbwa na jinamizi la ajali za barabarani, akieleza idadi ya watu waliofariki dunia ni 1,715.

 “Takwimu za Jeshi la Polisi Tanzania zinaonyesha kati ya Januari hadi Desemba mwaka huu, nchi yetu ilishuhudia jumla ya ajali 1,735. Ajali 1,198 kati ya hizo zilisababisha vifo vya ndugu zetu 1,715.”

“Hii ni idadi kubwa sana. Ndugu zetu wengine 2,719 walijeruhiwa katika ajali za barabarani. Asilimia 97 ya ajali hizi zimetokana na makosa ya kibinadamu, kubwa kabisa ikiwa uzembe wa madereva, uendeshaji hatari na mwendo kasi ambayo kwa pamoja ni asilimia 73.7 ya ajali zote,” alisema.

Aliagiza Wizara ya Mambo ya Ndani na Jeshi la Polisi kuongeza mikakati ya kuzuia ajali zinazosababishwa na makosa ya uzembe.

Katika ajali ya Januari 13, ilitokea katika Kijiji cha Chang’ombe, Kata ya Segera wilayani Handeni.

Desemba 24, 2024 watu wanane walifariki dunia na wengine kujeruhiwa katika ajali iliyohusisha lori na basi dogo la abiria aina ya Toyota Coaster lililokuwa likitokea Kijiji cha Michungwani, Kata ya Segera wilayani Handeni.

Ajali nyingine iliyosababisha vifo vya watu 11, huku 14 wakijeruhiwa ilihusisha gari aina ya Toyota Coaster na lori Desemba 25, 2024 eneo la Kwenkwale, Kata ya Kitumbi wilayani Handeni.

“Nilipata taarifa kuna ajali gari imedondoka tukafika pale na kuanza kuwapa majeruhi msaada na kulikuwa hakuna mtu aliyefariki, tulifanikiwa kuwaokoa ghafla lilitokea lori ikisemekana halina breki na kuvamia pale wenzangu wamefariki dunia mimi nimepata majeraha madogo mwilini.” Ni kauli Faraja Karata, mkazi wa Kijiji cha Chang’ombe, Kata ya Segera wilayani Handeni akisimulia jinsi wenzake 11 walivyofariki dunia wakiwa kwenye harakati za kuokoa majeruhi waliokuwa wakisafiri kutoka Dar es Salaam kwenda Arusha usiku wa kuamkia leo Januari 14, 2025.

Akizungumza akiwa wodini katika Hospitali ya Mji Korogwe amesema saa 2:30 usiku walisikia tukio la ajali, hivyo vijana kutoka Kijiji cha Mailikumi walijitokeza kutoa msaada. Anasema wakiendelea kutoa msaada lilitokea lori lililowagonga na wengine walikufa papo hapo.

Amesema katika ajali ya awali hakuna aliyefariki dunia ila walipata majeraha madogomadogo na walikuwa wamemaliza kutoa msaada, huku askari polisi wakiimarisha ulinzi.

Mkazi wa Kijiji cha Mailikumi, Aweso Twaha amesema wengi waliojitokeza kutoa msaada ni wananchi wa Kata ya Segera kutoka vijiji vya Mailikumi na Chang’ombe.

Kamanda Mchunguzi amesema wanamsaka dereva wa lori, Baraka Merkizedeck aliyewagonga watu waliokuwa pembeni mwa barabara.

Amewataja waliofariki dunia ambao wametambuliwa kuwa Hamisi, maarufu Saa Mbovu, Bugaja Rashid na Adam Maneno, wakazi wa Mailikumi. Mwingine ni Sawebu Juma, mkazi wa Dar es Salaam.

Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Balozi Batilda Burian amesema taarifa alizonazo ni kuwa vijana zaidi ya 40 walikuwepo eneo la tukio kusaidia majeruhi. Amesema wengine ni wafanyabiashara wanaofanya biashara zao barabarani.

Amesema kutokana na changamoto za ajali katika barabara ya Mkata kwenda Segera mpaka Korogwe, wanaangalia uwezekano wa kutengeneza njia pana zaidi ili kudhibiti ajali za mara kwa mara.

“Ajali ilikuwa mbaya, watu wamefariki kifo cha maumivu makali kutokana na ajali hiyo, Serikali imeliona hili tunaangalia uwezekano wa kutengeneza barabara kuwa pana zaidi ili kunusuru uwepo wa ajali hizi,” amesema.

Mganga Mkuu wa Hospitali ya Mji Korogwe, Miriam Cheche amesema walipokea miili 11 na majeruhi 13. Amesema waliofariki dunia wote ni wanaume.

Amesema baadhi ya majeruhi wamehamishiwa Hospitali ya Mkoa ya Bombo kwa matibabu zaidi, akieleza wengi wamevunjika viungo.

Nyongeza na Rajabu Athumani

Related Posts