KIKOSI cha Simba kimefuzu hatua ya robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika baada ya juzi kutoka sare ya kufungana bao 1-1 na Bravos do Maquis ya Angola, huku kikiweka rekodi ya kipekee ambayo haijawahi kutokea tangu msimu wa 2018-2019.
Mchezo huo wa makundi uliopigwa kwenye Uwanja wa Taifa wa Novemba 11 jijini Luanda nchini Angola, uliifanya Simba kuandika rekodi ya kufunga bao katika kila mechi ya ugenini ya CAF, ikiwa ni kwa mara ya kwanza kwani haijawahi kutokea.
Katika mchezo huo ilishuhudiwa wenyeji wakipata bao la utangulizi katika dakika ya 13, kupitia kwa Abednego Mosiatlhaga, huku la kuchomoa kwa upande wa Simba lililowapeleka robo fainali likifungwa na mshambuliaji, Leonel Ateba katika dakika ya 69.
Iko hivi, Simba imefuzu robo fainali ya sita kati ya saba ilizowania CAF tangu msimu wa 2018-19, na haijawahi kucheza michezo mitatu ya ugenini yote ikifunga bao, lakini msimu huu imetokea chini ya kocha, Fadlu Davids kuandika rekodi ya kipekee Msimbazi.
Msimu wa 2018-2019 ikishiriki Ligi ya Mabingwa Afrika, ilipangwa kundi D ambapo ilimaliza nafasi ya pili na pointi tisa nyuma vinara Al Ahly ya Misri iliyokuwa na pointi 10. Mechi za ugenini Simba ilichapwa na AS Vita 5-0, ikachapwa tena 5-0 na Al Ahly, kisha ikapoteza 2-0 kwa JS Saoura.
Msimu wa 2020-2021 ikacheza tena Ligi ya Mabingwa na kuangukia kundi A, ikamaliza kinara na pointi 13, ikifuatiwa na Al Ahly iliyomaliza na pointi 11. Simba ugenini ilichapwa na AS Vita 1-0, ikatoka 0-0 na Al Merrikh, kisha kwenda Misri kuchapwa na Al Ahly bao 1-0.
Msimu wa 2021-2022, ilikuwa Kombe la Shirikisho na kumaliza nafasi ya pili na pointi 10, nyuma ya vinara RS Berkane ya Morocco iliyomaliza sawa na pointi 10 pia. Hapa Simba mechi za ugenini ilianza na sare ya 1-1 dhidi ya US Gendarmerie, ikachapwa 2-0 na RS Berkane, ikapoteza 3-0 kwa ASEC Mimosas.
Msimu wa 2022-2023, ilikuwa Ligi ya Mabingwa Afrika na kumaliza nafasi ya pili kundi C na pointi tisa, nyuma ya Raja Casablanca ya Morocco iliyomaliza na pointi 16. Mechi za ugenini ilianza kufungwa 1-0 na Horoya AC, ikaifunga Vipers 1-0, ikachapwa na Raja Casablanca 3-1.
Msimu wa 2023-2024 ikiwa Ligi ya Mabingwa ilimaliza nafasi ya pili kundi B na pointi tisa, nyuma ya vinara ASEC Mimosas ya Ivory Coast iliyomaliza na pointi 11. Ugenini ilianza na matokeo ya 0-0 dhidi ya Jwaneng Galaxy, ikaenda Morocco kwa Wydad na kuchapwa 1-0, kisha kwenda Ivory Coast na kutoka 0-0 na ASEC.
Msimu huu wa 2024-2025 ikiwa Kombe la Shirikisho Afrika ndipo ikaandika rekodi ya kufunga bao katika kila mchezo wake wa ugenini ikiwa ni rekodi mpya kwao, ikishika nafasi ya pili kundi A na pointi 10, nyuma ya CS Constantine ya Algeria yenye pointi 12. Simba msimu huu ilianza ugenini kwa kichapo cha mabao 2-1 dhidi ya CS Constantine, ikashinda 1-0 mbele ya CS Sfaxien na sare ya 1-1 kwa Bravos do Maquis.
Kitendo hicho cha kufunga bao katika kila mchezo ndicho kilichoifanya timu hiyo kuandika rekodi mpya kwani kabla ya hapo haikuwahi kutokea, jambo lililomfanya kocha mkuu wa timu hiyo, Fadlu Davids kuwapongeza wachezaji wote kwa juhudi zao.
“Kimahesabu malengo yetu tumeyafikia lakini hatubweteki na kilichotokea kwa sababu moja ya mikakati yetu ni kuhakikisha mchezo wa mwisho tunaishinda CS Constantine, tunahitaji kuongoza kundi letu japo sio rahisi ila inawezekana,” alisema.