Na Muhidin Amri,Songea
WAKALA wa barabara za vijijini na mijini Tanzania(TARURA)Mkoa wa Ruvuma,kwa mwaka wa fedha 2024/2025 umehidhinishiwa Sh.bilioni 38.394 kwa ajili ya kufanya matengenezo na ujenzi wa barabara zenye urefu wa kilometa 1,145,madaraja madogo 50 na makalavati 57.
Kati ya hizo Sh.bilioni 7.8 bajeti ya barabara kuu,Sh.bilioni 9.8 zinatokana na tozo ya mafuta,Sh.bilioni 4.5 fedha kutoka mfuko wa Jimbo na Sh.bilioni 16.2 ni fedha za mradi wa Agricconect chini ya Umoja wa Ulaya(EU).
Hayo yamesemwa na Meneja wa TARURA Mkoani hapa Mhandisi Silvester Chinengo,wakati akitambulisha barabara mpya mbili ya Muungano-Majengo na barabara ya Kilimo Mseto-Pm House zenye urefu wa kilometa 1.5 kwa gharama ya Sh.milioni 949 pamoja na barabara ya Mjimwema-Mkuzo yenye urefu wa kilometa 1.1 ambayo ujenzi wake umegharimu Sh.milioni 426.
“Barabara hizi zimejengwa kutokana na fedha za tozo ya mafuta na zimeleta mabadiliko makubwa kwenye mitaa kwa sababu wakati wa mvua wananchi waliathirika na mafuriko pamoja na matope, kwa sasa ni msaada mkubwa kwa wakazi wa mitaa hiyo na mali zao,pia zitarahisisha sana shughuli za usafiri na usafirisha kwa wananchi wa maeneo hayo.”alisema Chinengo.
Alisema,TARURA mkoa wa Ruvuma inahudumia mtandao wa barabara wa kilometa 71,146.21,madaraja 306,makalavati 531,drifti 14 na mitaro yenye urefu wa kilometa 6.91 ambapo kilometa 2,312 sawa na asilimia 32.36 ni za mjazio,kilometa 3,873.85 sawa na asilimia 54.12 ni za mkusanyo na kilometa 959.52 sawa na asilimia 13.43 ni za jamii.
Chinengo alieleza,katika barabara hizo kilometa 128.66 sawa na asilimia 1.8 ni za lami na zege,kilometa 1,429 sawa na asilimia 20 za changarawe na kilometa 5,588 sawa na asilimia 78.2 za udongo.
Akizungumzia miradi viporo alisema,kuna mradi mmoja wa kuondoa vikwazo vya usafirishaji(RISE)unaotekelezwa kwenye Halmashauri ya Madaba,Mbinga Mji,Halmashauri ya wilaya Mbinga,Nyasa,Namtumbo na Tunduru.
Aidha alisema,Serikali imetenga Sh.bilioni 2.28 kwa ajili ya kuondoa vikwazo barabarani ikiwemo kujenga madaraja na barabara za changarawe ambapo utekelezaji wake umefikia asilimia zaidi ya 70.
Chinengo,ameishukuru Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan,kuongeza bajeti ya barabara kwa kuingizwa vyanzo vipya vya mfuko wa Jimbo na Tozo,kwani awali walikuwa na bajeti moja kutoka Bodi ya Mfuko wa Barabara.
“vyanzo vipya vimewezesha kuongezeka kwa mtandao wa barabara ambapo zaidi ya asilimia 65 zinapitika majira yote ya mwaka,kuongeza mtandao wa barabara za lami na ufungaji wa taa katika makao makuu ya Halmashauri zote za mkoa wa Ruvuma”alisema.
Kwa upande wake Kaimu meneja wa Tarura wilaya ya Songea Godfrey Mngale alieleza kuwa,katika barabara ya Mjimwema-Mkuzo kazi zilizofanyika hadi sasa ni kuweka tabaka la lami,kujenga mitaro ya kupitisha maji kwa kutumia mawe pande zote mbili.
Alisema,ujenzi wa barabara hiyo umewezesha kubadilisha mazingira ya maeneo hayo pamoja na kupandisha thamani ya viwanja na vyumba na awali wananchi wa maeneo hayo walipata adha kubwa hasa wakati wa mvua kutokana na utelezi kwa kuwa eneo hilo lina mteremko mkali.
Amewataka wananchi waliopitiwa na barabara hiyo, kuhakikisha wanalinda miundombinu ili iweze kudumu kwa muda mrefu kwa kuwa waliteseka kwa muda mrefu kabla Serikali kupitia TARURA kuimarisha barabara kwa kiwango cha lami.
Denis Timoth Mkazi wa mtaa wa Matogoro,ameipongeza Serikali ya awamu ya sita kwa kuendelea kutekeleza miradi ya mingi ya barabara ili kuwaondolea wananchi kero ya kusafiri wanapotoka eneo moja kwenda lingine kwa ajili ya shughuli zao za kiuchumi.
Agnes Komba mkazi wa mtaa wa Makambi alisema,ujenzi wa barabara za lami umewasaidia wananchi kujikomboa na umaskini na kuimarika kwa uchumi wa mtu mmoja mmoja na wilaya ya Songea, kwani hivi sasa mitaa maeneo mengi hakuna adha ya usafiri na usafirishaji.
Muonekano wa barabara ya Muungano-PM House iliyojengwa katika Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma kama inavyoonekana.
Barabara ya Mjimwema-Mkuzo yenye urefu wa kilometa 1.1 ambayo imejengwa kwa kiwango cha lami kwa gharama ya Sh.milioni 426.`
Baadhi ya waendesha pikipiki na watumiaji wengine wakipita kwenye
barabara ya Mjimwema-Mkuzo yenye urefu wa kilometa 1.1 iliyojengwa kwa
kiwango cha lami kwa gharama ya Sh.milioni 426.