TASAF YASHIRIKI MAONESHO YA KIMATAIFA YA BIASHARA ZANZIBAR (ZITF)

 

Mfuko wa Maendeleo ya Jamii – TASAF, umeshiriki kwenye maonesho ya Kimataifa ya Biashara Zanzibar ‘Zanzibar International Trade Fair’ ambapo umewawezesha wanufaika wa Mpango wa Kunusuru Kaya za Walengwa kutoka visiwa vya Pemba na Unguja kuonesha na kuuza bidhaa mbalimbali wanazozizalisha.

Pia katika maonesho hayo, wananchi kutoka maeneo mbalimbali wanapata fursa ya kujifunza namna TASAF inavyotekeleza afua za Mpango wa kunusuru kaya za walengwa na kukuza kipato cha kaya.

Maonesho haya yanayofanyika kwenye viwanja vya Nyamanzi kisiwani Unguja yanatoa fursa kwa wafanyabiashara na wajasiriamali mbalimbali kuonesha bidhaa zao na kupata masoko kutoka pande mbalimbali za nchi yetu.

Akizungumza wakati alipowatembelea wanufaika wa Mpango kwenye maonesho haya, Mkurugenzi wa Mifumo, Tathmini na Mawasiliano wa TASAF Bw. Japhet Boaz aliwapongeza wanufaika wa Mpango kwa kuwekeza sehemu ya ruzuku waliyopokea na kujikita kwenye shughuli za ujasirimali.

Mkurugenzi huyo pia aliwasihi wanufaika kuendelea kutumia vizuri rasilimali fedha wanazozipata kutoka kwenye biashara zao ili hali zao za maisha ziendelee kuimarika na kuondokana na umaskini kwenye kaya zao.

“Nawapongeza kwa kufanya shughuli hizi zinazowaingizia kipato, endeleeni kutumia vizuri fedha mnazozipata kwa lengo la kutokomeza hali duni kwenye kaya zetu,” alisema na kuongeza kuwa TASAF imekuwa ikishiriki kikamilifu katika ujenzi wa miundombinu ya utoaji huduma za kijamii.

Katika maadhimisho ya miaka 61 ya Mapinduzi ya Zanzibar, TASAF imeshiriki kikamilifu kwa kufanya ujenzi wa miradi ya elimu na afya katika visiwa vya Pemba na Unguja.

“Wakati wa shamrashamra za kuelekea kilele cha maadhimisho ya miaka 61 ya Mapinduzi ya Zanzibar, TASAF ilizindua Kituo cha Afya Upenja kilichopo katika Wilaya ya Kaskazini B Mkoa wa Kaskazini Unguja, Kituo cha Afya Kinyikani kilichopo Kisiwan Pemba sambamba na uwekaji wa Jiwe la Msingi la Skuli ya Dodo iliyopo kisiwani Pemba,” aliongeza.

Related Posts