TMA yatangaza uwepo wa Kimbunga Dikeledi

Dar es Salaam. Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa taarifa ya uwepo wa Kimbunga Dikeledi katika Bahari ya Hindi mwambao wa pwani ya Msumbiji.

Katika taarifa yake, iliyotoa leo Jumanne Januari 14, 2025 mamlaka hiyo inaeleza kuwa, mifumo ya hali ya hewa inaonesha kimbunga hicho kwa sasa kipo mwambao wa pwani ya Msumbiji na kinatarajiwa kurejea katika Rasi ya Msumbiji leo alasiri.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, kimbunga hicho hakiashirii uwezekano wa kusababisha athari za moja kwa moja hapa nchini.

“Hata hivyo, kutokana na ukaribu wa maeneo ambayo Kimbunga Dikeledi kipo sambamba na maeneo ya kusini mwa nchi yetu, upo uwezekano mdogo wa matukio ya vipindi vifupi vya mvua kubwa katika maeneo ya pwani ya kusini hususan katika mikoa ya Lindi na Mtwara kwa siku ya leo Januari 14, 2025,”inaeleza sehemu ya taarifa hiyo.

Kwa upande mwingine, TMA inaeleza kuwa, vipindi vya upepo mkali na mawimbi makubwa ya Bahari vinatarajiwa kwa maeneo ya ukanda wote wa pwani ya Bahari ya Hindi na maeneo jirani kati ya Januari 14 na15, 2025.

“Aidha, taarifa ya tahadhari ya uwepo wa vipindi vya upepo mkali na mawimbi makubwa, mamlaka ilianza kutoa kuanzia tarehe 11 Januari, 2025 na hali ya upepo inatarajiwa kuwa shwari kuanzia tarehe 16 Januari, 2025,”inaeleza taarifa hiyo.

Mamlaka hiyo inashauri watumiaji wa bahari na wananchi kwa jumla kuendelea kufuatilia na kuzingatia taarifa za utabiri kutoka TMA pamoja na kupata ushauri na miongozo ya wataalam wa kisekta.

Pia, inasema inaendelea kufuatilia mwenendo wa kimbunga hicho na athari zake kwa mifumo ya hali ya hewa hapa nchini na itaendelea kutoa taarifa kila inapobidi

Related Posts