Dar es Salaam. Mbwembwe na vituko vimegubika sera za wagombea wa nafasi za ujumbe wa Baraza Kuu Bara, Zanzibar na nafasi ya ujumbe wa mkutano mkuu kwa upande wa Zanzibar na Bara.
Mbwembwe hizo zilikuwa sehemu ya sera za wagombea wa nafasi hizo na kuibua vicheko kutoka kwa wajumbe waliokuwepo ndani ya Ukumbi wa Ubungo Plaza, Dar es Salaam usiku wa leo Jumanne Januari 14, 2025.
Vituko vilianza kushuhudiwa kutoka kwa mgombea wa ujumbe wa mkutano mkuu Bavicha – Zanzibar, Alawiya Shaibu Hussein ambaye hakuwa na muda wa kumwaga sera, kwani baada ya kujitambulisha aliishia kusema anaomba kura.
Kimbembe kilikuwa wakati wa kujibu maswali, aliulizwa iwapo atakusanya yote ndipo ajibu, alimwambia msimamizi wa uchaguzi “wewe endelea,” bila kujibu swali.
Kama ilivyokuwa kwa swali la kwanza, mgombea huyo alishindwa kujibu, licha ya kuomba lirudiwe.
Aliulizwa swali la tatu atakifanyia nini chama hicho iwapo atachaguliwa amejibu, “kuhamasisha na kuhamasisha vijana.”
Ulipofika wakati wa mgombea mwingine wa nafasi hiyo, Najma Hemed Ali ameanza kwa kujitambulisha jina na nafasi aliyonayo sasa, kisha akanyamaza kwa sekunde kadhaa, hivyo kusababisha minong’ono kutoka kwa wajumbe.
Msimamizi wa uchaguzi alipowataka wajumbe wawe watulivu, mgombea huyo alianza upya kujieleza kwa kusema, “Ni mjum…. Vijana naomba kura zenu.”
Ameendelea kwa kuwahoji wajumbe, “mmekubali au, kweli? Haya Asante.”
Hayo yalisababisha vicheko kutoka kwa wajumbe wa mkutano huo wa uchaguzi.
Alipoulizwa swali la kwanza, Najma alikaa kimya, vivyo hivyo kwa swali la pili na tatu.
Mbwembwe hizo hazikuishia kwenye kushindwa kuzungumza, bali hata aina ya maneno na mtindo wa uombaji kura.
Miongoni mwa wagombea waliotia mbwembwe katika kumwaga sera zake ni Pascal Mlapa anayeutaka ujumbe baraza kuu Bavicha, Bara.
Ameanza kwa kuitambulisha taaluma yake ya ujenzi wa maghorofa, akiihusisha na kile alichosema kama anajenga maghorofa atashindwa kujenga hoja.
“Kama najenga maghorofa nitashindwa kujenga hoja ndugu wajumbe?” amehoji Mlapa.
Sambamba na hilo, ameahidi kuhakikisha anaitibu kile alichokiita malaria iliyopo ndani ya chama hicho, kwa kusimamisha nguvu ya umma.
Atasimamisha nguvu ya umama kuchochea mabadiliko aliyodai yatatibu malaria iliyopo ndani ya chama hicho.
Amesema haiwezekani afike katika baraza kuu la chama hicho kikuu cha upinzni kisha aseme sawa bwana mkubwa, wakati akidai vijana wanatekwa na hatakubali kubariki jambo hilo.
Kwa upande wa Barnaba Samwel anayegombea nafasi hiyo, amejinadi kwa kutaja nyadhifa mbalimbali alizowahi kushika ikiwemo Mwenyekiti wa Chadema Tawi la Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM) jijini Dar es Salaam.
Amesema amewahi pia kuwa mhazini wa mtandao wa wanafunzi Mkoa wa Dar es Salaam, amewahi kugombea uenyekiti kanda ya Dar es Salaam na kwamba anaomba ridhaa.
Wingi wa nyadhifa alizowahi kushika, umesababisha swali kutoka kwa mmoja wa wajumbe aliyemuuliza amewahi kufanya nini katika nafasi hizo, amejibu “kwa sasa yeye ni mkunja ngumi kama wakunja ngumi wengine.”
Hata hivyo, mgombea huyo hakumaliza sera zake, alikatishwa na msimamizi wa uchaguzi kutokana na muda wake wa dakika mbili alizopewa kumalizika.
Mgombea mwingine wa nafasi hiyo ni Ezekiel Mollel aliyesema amewahi kuwa Spika wa Bunge la Wanafunzi IFM na sasa ni Katibu wa Baraza la Vijana Kigamboni.
Amesema ameomba nafasi hiyo kwa sababu ya matamanio ya kuwepo baraza litakaloaminika tena na kuwavutia vijana.
Kwa upande wa Atfat Hamad Ali anayeutaka ujumbe huo kutokea Zanzibar uombaji kura wake ulihusisha mikono na mbwembwe za kuvuta sauti.
Sambamba na hilo, mgombea huyo hakutumia hata dakika moja kati ya mbili alizopaswa kumwaga sera zake.
Kabla ya msimamizi wa uchaguzi hajaamrisha maswali kuulizwa, Atfat alishaomba wajumbe wamuulize.
Hilo liliibua vicheko kutoka kwa wajumbe, ambao wamezoea utaratibu wa maswali hutangazwa na msimamizi wa uchaguzi.
Katika moja ya maswali aliyoulizwa, mgombea huyo alimwamrisha mjumbe anayeuliza asimame ili amuone ndiyo amjibu.
Katika kuzimwaga sera zake, Halfan Abdallah Maalim anayeutaka ujumbe wa mkutano mkuu Bavicha taifa, ameshindwa kuitaja nafasi anayoiomba, huku akishindwa kuzungumza kwa ufasaha mbele ya kadamnasi
“Nimesimama hapa kugombea nafasi ya mjumbe mkuu… Mjumbe wa mkutano Mkuu Bavicha Taifa, naombeni kura zenu,” amesema.
Hata hivyo, ameshindwa kuendelea na sera, badala yake aliamua kuomba kura moja kwa moja.
Wakati wa maswali, mgombea huyo alitaka yaulizwe yote kisha ayajibu kwa pamoja na aliishia kujibu swali moja lililohusu uzoefu wake ndani ya chama hicho.
Endelea kufuatilia Mwananchi kwa taarifa zaidi kuhusu uchaguzi huu