Wajasiriamali waeleza walivyonufaika na Tasaf

Unguja. Wajasiriamali waliopo kwenye mpango wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (Tasaf) wameeleza namna ulivyowaondoa kwenye umaskini.

Mpango wa kunusu kaya maskini kwa Zanzibar ulianza mwaka 2013 ukiwa katika afua tatu za ruzuku, ajira za muda na miundombinu.

Mpaka sasa kuna vikundi 3,372 vyenye wanachama 45,948.

Vikundi hivyo vimekusanya akiba ya zaidi ya Sh1.6 bilioni na vimeendelea kukopeshana kwa ajili ya kuanzisha na kutekeleza miradi ya kuwaongezea kipato.

Wakizungumza katika maonyesho ya biashara ya kimataifa Dimani Nyamanzi Januari 14, 2025, baadhi ya wajasiriamali wanaonufaika na mfuko huo wamesema hawakuwahi kufikiria kama wanaweza na kushiriki maonyesho ya biashara kama hayo.

Khadija Slaym Salim, mkazi wa Kianga amesema mwanzo walikuwa kaya maskini lakini kwasasa wanajivunia kunufaika wamenufaika kwenye vikundi vyao na kujiongezea vipato.

Khadija amesema mbali na kunufaika mmoja mmoja, wamenufaika kwenye huduma za kijamii kama shule, barabara na hospitali.

“Tofauti na mwanzo watoto walikuwa wanashindwa kwenda shule, mikoba ya daftari hawakuwa nayo, mtoto akienda shule tulikuwa tunakung’uta mifuko ya unga tunawapa lakini sasa hivi begi wanapata,” amesema Khadija.

Mnufaika mwingine, Naomba Bakari Hassan kutoka Kikundi cha Kutoa ni Moyo Chakechake Pemba,  amesema walikuwa na maisha magumu lakini sasa wanaendelea kuimarika kupitia kwenye vikundi vyao.

“Sasa hivi tunasomesha watoto tunapata fedha za huduma za nyumbani na kusomesha watoto tofauti na ilivyokuwa awali,” amesema Naomba.

Amesema kabla ya kuingia kwenye mradi alikuwa na maisha magumu lakini kwa sasa ni maisha bora, “familia yangu inakula, na mimi najitosheleza mahitaji yangu kupitia biashara ninayoifanya.”

Naomba anayefinyanga vitezo na kushona mikoba, anasema ndoto zake anataka awe mfanyabiashara mkubwa na kuwa na maisha bora zaidi.

Mtoto wa mnufaika, Raya Suleiman Hamad kutoka Kikundi Tushikamane cha Mgogoni Wete Pemba, amesema wazazi ndio wapo kwenye mpango huo, walipopata ruzuku wakatengeneza mafuta na bidhaa zingine kwa ajili ya kuuza.

Raya ambaye amesomeshwa na ruzuku ya Tasaf iliyokuwa ikitolewa kwa wazazi wake, amesema kwa sasa ameshakuwa mtaalamu kwenye ujasiriamali baada ya kufundishwa.

Mkurugenzi wa Mifumo na Mawasiliano ya Umma Tasaf, Japhet Boaz amesema kaya hizo zilikuwa hazikuwa na uwezo.

Boaz amesema baada ya kuzisaidia wanaziweka kwenye vikundi, kisha wanaweka akiba na wanaweza kukopeshana.

“Hata hawa tunaowaona hapa kwenye maonyesho wametoka kwenye vikundi, wakabuni miradi kulingana na mazingira waliyonayo kisha wameendelea kutengenza vitu mbalimbali na bidhaa nyingi zinazotokana na asili,” amesema.

Mratibu wa Tasaf Unguja, Makame Ali Haji amesema kwa taratibu za Tasaf kila kikundi kinakuwa na wanachama 15 wanaojiwekea na kuanzisha biashara ndogondogo.

“Tunashukuru wametumia rasimali za bahari kujiendeleza kiuchumi, wapo wanaolima mwani na wengine wameanzisha uzalishaji wa sabuni unaotokana na mwani, tunashukuru sana, wananchi hawa wameweza kujiimarisha kiuchumi na tunafahamu mpango huu unaendelea vizuri,” amesema Makame.

Related Posts