Yanga vs MC Algeria ni shoo ya kibabe sana CAFCL, utamu uko hapa

DAKIKA 90 za Jumamosi ya Januari 18, 2025 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa dhidi ya MC Alger, zimebeba hatma ya Wananchi msimu huu katika michuano ya kimataifa, ambapo watakuwa na kibarua kizito cha kupigania tiketi ya kwenda robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Wikiendi iliyopita Yanga imeonyesha ukubwa wake kwenye soka la Afrika kwa kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Al Hilal, lililofungwa na Stephane Aziz KI katika dakika ya saba tu ya mchezo huo uliochezwa kwenye Uwanja wa Cheikha Ould Boidiya, Mauritania.

Bao hilo liliifanya Yanga kwanza kulipiza kisasi kufuatia kupoteza mchezo wa kwanza jijini Dar es Salaam kwa mabao 2-0 ikiwa nyumbani dhidi ya vigogo hao wa Sudan, pili kuweka hai matumaini ya kutinga hatua ya robo fainali ya michuano hiyo kwa mara ya pili mfululizo.

Hesabu za Yanga kwa sasa ni pointi tatu za mchezo wa Jumamosi dhidi ya MC Alger, ikumbukwe katika mchezo wa kwanza ambao ulichezwa nchini Algeria Wananchi walipoteza kwa mabao 2-0, kikiwa kipigo cha pili mfululizo kukumbana nacho katika michuano hiyo kabla ya kuzindukia DR Congo na kuambulia sare ya 1-1 dhidi ya TP Mazembe.

Yanga yenye pointi saba katika nafasi ya tatu, inahitaji ushindi tu kwenye mchezo huo ambao ni kama fainali kutokana na wapinzani wao, MC Alger nao kuwa na uhitaji wa nafasi hiyo, Waalgeria hao wapo nafasi ya pili kwenye msimamo wa kundi A wakiwa na pointi nane, wao wanahitaji sare pekee kusonga mbele.

Licha ya Yanga kupoteza katika mchezo wa ugenini dhidi ya MC Alger, rekodi zinaonyesha kuwa Wananchi wamewahi kuifunga timu hiyo wakiwa nyumbani jijini Dar es Salaam. Walifanya hivyo 2017 na ilikuwa upande wa Kombe la Shirikisho Afrika, ulikuwa mchezo wa mkondo wa kwanza kwa bao 1-0 ambalo lilifungwa na Thabani Kamusoko.

Ni kundi A ambalo yupo Yanga na B ambalo bado hakijaeleweka timu ambazo zitaungana na Al Hilal na AS FAR ya Morocco ambazo zenyewe zilishajikatia tiketi mapema ya hatua ya robo fainali kabla ya mechi za raundi ya mwisho. Kundi A kuna vita kati ya Yanga na MC Alger kila mmoja ana nafasi ya kuungana na Al Hilal.

Kwa upande wa kundi B, ambalo AS FAR anayoichezea beki wa zamani wa Simba, Henock Inonga Baka imeshafuzu ikiwa na pointi tisa, vita imebakia kwa Mamelodi Sundowns yenye pointi nane na Raja Casablanca ya Morocco yenye pointi tano.

Katika mechi za raundi ya mwisho kwa timu za kundi hili, Mamelodi itamaliza kibarua chake dhidi ya AS FAR huku Raja Casablanca wakiwa nyumbani nao wakijaribu bahati yao kwa AS Maniema Union.

Orlando Pirates ya Afrika Kusini ikiwa na pointi 11 na Al Ahly yenye pointi 10, zimeshafuzu kwa hatua ya robo fainali zikitokea kundi C, ila zitakachopigania katika raundi ya mwisho zitakapokutana ni ufalme wa kundi hilo kwani wamepishana pointi moja tu.

Al Ahly atakuwa nyumbani kuikaribisha Orlando Pirates. Katika mchezo wa kwanza ambao ulichezwa Johannesburg, Afrika Kusini waligawana pointi baada ya kutoka suluhu. Nani kumaliza mbabe wa kundi hilo ni suala la kusubiri na kuona nini kitatokea huko Cairo.

Kama ilivyo kundi C, D nalo wanatafuta ufalme tu, nani kumaliza nafasi ya kwanza kama kufuzu  Esperance de Tunis na Pyramids anayoichezea mshambuliaji wa zamani wa Yanga, Fiston Mayele zote zimefuzu.

Tofauti na wababe wa kundi C ambao wanakutana katika raundi ya mwisho huku Esperance yenye pointi 10 sawa na Pyramids, wote watakuwa nyumbani, mmoja atacheza dhidi ya Sagrada Esperanca ya Angola, kina Mayele watacheza dhidi ya Djoliba ya Mali.

Emam Ashour wa Al Ahly anaongoza orodha ya wafungaji akiwa na mabao manne, akisaidia timu yake kutamba kwenye hatua za makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Ashour alianza taratibu, akifunga bao moja katika mechi ya tatu. Hata hivyo, aliibuka kuwa hatari zaidi katika mechi ya nne ambapo alitikisa nyavu mara tatu, wakati Al Ahly ikiibuka na ushindi wa mabao 6-1 dhidi ya CR Belouizdad. 

Wessam Abou Ali, pia kutoka Al Ahly, ana mabao matatu, aliyoyafunga yote katika mechi moja (MD3). Ibrahim Adel wa Pyramids na Elias Mokwana wa Esperance de Tunis nao wameonyesha ubora wao, kila mmoja akiwa na mabao matatu.

Clement Mzize wa Yanga naye ni miongoni mwa washambuliaji ambao wanawania ufungaji bora akiwa na mabao mawili ambayo alifunga dhidi ya TP Mazembe wakati Wananchi wakiibuka na ushindi wa mabao 3-1 kwa Mkapa na kuamisha matumaini ya kutinga robo fainali kwa mara ya tatu mfululizo.

Related Posts