BEKI kisiki wa zamani wa Coastal Union, Simba na Mtibwa Sugar, Abdi Banda amejiunga na Dodoma Jiji kama mchezaji huru baada ya kuvunja mkataba na Baroka FC ya Afrika Kusini.
Banda alivunja mkataba na Baroka miezi mitatu tangu ajiunge na timu hiyo inayoshiriki Ligi ya Championship.
Beki huyo alivunja mkataba na timu hiyo baada ya kupita wiki mbili tangu Fifa ilipoiamuru Richards Bay – klabu aliyoichezea awali kumlipa mamilioni ya fedha ya mshahara aliyokuwa anaidai.
Akizungumza na Mwanaspoti, Msimamizi wa mchezaji huyo, Fadhili Omary alisema Banda ameshamalizana na Dodoma Jiji na tayari yuko mjini humo akijiandaa na mechi za Ligi Kuu Bara.
“Amesaini mkataba wa miezi sita ya mzunguko wa pili. Yuko Bongo muda kidogo kilichobaki ni upande wa timu kumtambulisha,” alisema Sizya.
Timu hiyo iko nafasi ya tisa kwenye msimamo wa Ligi Kuu ikikusanya pointi 19 kwenye michezo 16, ushindi tano, sare nne na kupoteza michezo saba.
Nyota huyo mwenye uwezo wa kumudu kucheza kama beki wa kati, kushoto na kiungo mkabaji kabla ya Baroka alizitumikia Richards Bay, Chippa United, Highlands Park na TS Galaxy za Afrika Kusini huku Tanzania akiichezea Simba na Coastal Union.