ACT Wazalendo na usemi aungurumapo papa baharini na wengine wapo

Dar es Salaam. Aungurumaye baharini papa, lakini na wengine wapo. Hivyo ndivyo unavyoweza kukielezea Chama cha ACT Wazalendo, ambacho mwaka 2024 kilitimiza miaka 10 tangu kuanzishwa kwake, kikitumia muda huo kufurukuta na kupambana na miamba ya vyama vya upinzani vilivyotangulia.

Katika mahojiano maalumu na Mwananchi wiki hii, Makamu Mwenyekiti wa ACT Wazalendo Bara, Issihaka Mchinjita anaeleza mikakati ya chama hicho kushindwa chaguzi na hatimaye kushika Dola.

Swali: Tumemaliza uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwishoni mwa 2024 ambayo vyama vya upinzani vimeshindwa vibaya, nini mikakati ya ACT Wazalendo baada ya hapo?

Jibu: Uchaguzi wa Serikali za Mitaa na kwa jinsi ulivyokuwa, umeacha malalamiko mengi na ndiyo maana sisi tumefungua kesi 51 na zimeanza kutajwa katika mahakama mbalimbali nchini.

Kwa upande wa Zanzibar wao hawana uchaguzi wa Serikali za Mitaa, hivyo chama kimejipanga kufuatilia programu ya uandikishwaji wa wapigakura katika Daftari la Kudumu la Wapigakura, kwa sababu uchakachuaji wa uchaguzi huwa unaanzia katika hatua hiyo.

Hivyo tunatarajia viongozi wote wa ACT Wazalendo watakuwa na uhamasishaji katika ziara zinazoanza hivi karibuni na pia kusukuma ajenda za kitaifa zinazohusu mabadiliko ya uendeshaji wa uchaguzi nchini.

Swali: Kwa muda mrefu vyama vya upinzani vimekuwa vikikata tamaa ya kufungua kesi za uchaguzi kwa madai ya kutokuwa na imani na Mahakama, nini kimewasukuma safari hii kufungua kesi zote hizo?

Jibu: Ni kweli, kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2019, ambao zaidi ya asilimia 80 ya wagombea walienguliwa, hatukuona kwa namna gani Mahakama zinaweza kurejesha wagombea wetu.

Mwaka 2020 tulishiriki kwenye uchaguzi ambao ulikuwa na mazonge mengi, tulishuhudia hali ya kidemokrasia iliyokuwa ikikua kuanzia mwaka 1995 hadi mwaka 2015, lakini ilikuja kushuka mwaka 2020 hadi wabunge wanne wa upinzani waliochaguliwa.

Hapo pia hatukuona kama Mahakama ingesaidia kushughulikia kesi zetu.

Lakini baada ya kuingia kwa Rais Samia Suluhu Hassan aliyetangaza kwamba anataka tuanze upya na sisi ACT Wazalendo tulichora barabara ya mambo gani tunataka yafanyiwe kazi, kwa hiyo tulishiriki kwenye kufanya mabadiliko makubwa ya kisheria na usimamizi wa haki hapa nchini.

Pili, tunakwenda kujenga msingi, kwani kuna mambo yameanza kujitokeza kuanzia mwaka 2020 ambayo kwa kweli yanakatisha tamaa.

Tumeanza kuona dalili za kuvurugwa kwa uchaguzi, zikiwemo za makaratasi ya kupigia kura yakisambaa mitaani kabla ya uchaguzi na ndio zilikuwa kura feki. Tuliyaona hayo mwaka 2020 na katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa tumeyaona hayo.

Tukishinda hizi kesi, tutakwenda Mahakama Kuu kutaka uchapishaji wa makaratasi ya kura urudishwe kwenye misingi ya asili, ambako huko nyuma mchakato ulikuwa ukishirikisha wadau.

Swali: Umezungumzia matumaini baada ya Rais Samia kuingia madarakani na kuanzisha kikosi kazi. Mbona bado mnaulalamikia uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa mwaka jana?

Jibu: Ni kweli hakuna mabadiliko makubwa yaliyofanyika, badala yake kumekuwa na hadaa kubwa.

Rais Samia alipoingia madarakani alikuja na falsafa ya 4R (Maridhiano-Reconciliation), Ustahimilivu (Resilience), Mageuzi (Reforms), na Kujenga upya Taifa (Rebuilding).

ACT Wazalendo tulimpa ushirikiano kuhakikisha kwamba tunapata kikosi kazi na tutapata hiyo sheria.

Lakini kituko cha kwanza ni kwenye Tume ya Uchaguzi, badala ya kuundwa kwa Tume Huru ya Uchaguzi kama tulivyotarajia, ikachukuliwa iliyokuwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi ikabatizwa kuwa ndio Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi.

Kwa kweli ile ilikuwa ni kuwakatisha tamaa waliofanya jitihada, vikiwemo vyama vya siasa, asasi za kiraia na watu wenye heshima walioshiriki kwenye michakato ile.

Kingine ni kwenye Sheria ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi ambayo inataja kwamba uchaguzi wa Serikali za Mitaa usisimamiwe na Wizara ya Tamisemi, lakini bahati mbaya sana ikaweka kifungu kinachoweka mkwamo kinachosema Bunge litunge Sheria nyingine itakayowezesha kufanya kazi.

Lakini kwa sababu sheria haikutungwa, Tamisemi imefanya vilevile ilivyofanya mwaka 2019, tofauti yake ni kwamba imekuja na hadaa.

Awali tulidhani wana nia njema, kila tulipolalamika Tamisemi walikuja kusikiliza, tumefanya vikao zaidi ya vitano, tangu walipotoa kanuni zao tulikutana nao na TCD (Kituo cha Demokrasia Tanzania).

Tamisemi wakakubali kurekebisha na hata baada ya mchakato kuanza tukakutana na Baraza la Vyama vya siasa, wakaja wakatusikiliza wakakubali na wakaenda kufanya marekebisho.

Tulipoingia kwenye uchaguzi, wagombea wetu walipoenguliwa, Waziri wa Tamisemi (Mohamed Mchengerwa) akasema hilo ni kinyume na utaratibu atalishughulikia, akasema kwa kuwa mchakato wa kuwarejesha wagombea wetu, tukate rufaa wagombea wote watarejeshwa.

Tukaona mwanga tukawaelekeza watu wetu wakate rufaa, lakini hayakutekelezwa.

Lakini usiku uleule tulishuhudia makaratasi ya kupigia kura yakiwa yamesambazwa na ndiyo maana uchaguzi ule ulivurugwa.

Swali: Kwa sasa ACT Wazalendo inajipimaje kisiasa?

Jibu: Kwanza inafahamika kuwa hali siasa ya nchi yetu imeipa nafasi kubwa ACT Wazalendo kwenye kanda tofauti, kwanza Kanda ya Magharibi ambayo chama chetu kina nguvu kubwa.

Kwa mfano ukienda Kanda ya Magharibi kwenye majimbo yake zaidi ya sita ACT Wazalendo ina uhakika wa kushindwa, kwa mfano Kigoma Mjini, Kigoma Kaskazini, Kigoma Kusini.

Halafu Tabora kuna majimbo kama Kaliua, Urambo chama kinaweza kushinda.

Pia tuna Kanda ya Pwani kwenye majimbo ya Mafia, Mkuranga, Rufiji kote tuna uhakika. Ukija Dar es Salaam jimbo la Mbagala, Temeke, Kinondoni tuna uhakika nayo.

Kwa upande wa Kaskazini kuna majimbo kama Tanga Mjini, Pangani huko nako tuna uhakika wa kushinda.

Ukiacha hayo, pia ukienda Lindi, kuna majimbo sita tuna uhakika nayo ambayo ni Kilwa Kaskazini, Kilwa Kusini, Nchinga, Lindi Vijijini, Liwale na Ruangwa la Waziri Mkuu (Kassim Majaliwa), pia ACT ina uhakika wa kushinda.

Ukienda Ruvuma kuna Mkoa wa Selous wenye majimbo matatu ambayo ni Namtumbo, Tunduru Kaskazini, Tunduru Kusini, haya ni majimbo, chini ya uchaguzi wa haki tutashinda.

Kama uchaguzi utakuwa huru na wa haki tuna uhakika wa kupata majimbo 50 upande wa Bara.

Kwa upande wa Zanzibar ambako kuna majimbo 50, tuna uhakika wa majimbo 30 kama uchaguzi ukiwa huru na wa haki.

Pia ACT Wazalendo tofauti na vyama vingine, imerithi wanachama kutoka CUF na wengine Chadema.

Kwa hiyo tunazo ngome zilizokuwa za Chadema na sasa zimekuwa za ACT, kwa mfano Nkasi (Rukwa), maeneo ya Ludewa (Njombe) tuna madiwani kule.

Mwaka jana ACT Wazalendo tumezunguka majimbo yote 214 nchini na tumepata viongozi kwenye majimbo hayo katika uchaguzi wetu wa ndani.

Kumbuka ACT imetimiza miaka 10 tangu ilipoanzishwa mwaka 2014, kwa hiyo kuna hatua kubwa tumepiga.

Swali: Kwa hiyo mnaelekea kuwa chama kikuu cha upinzani?

Jibu: Chama kikuu cha upinzani kitajulikana tukienda kwenye uchaguzi kwa sababu sasa uchaguzi wa 2020 uliharibiwa, lakini ACT Wazalendo ina wabunge wengi kuliko vyote vya upinzani.

Tulikuwa tunaamini kuwa uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa 2024 ungekuwa huru na wa haki ungetupa kipimo kizuri cha kujua hali yetu.

Swali: Kwani ACT Wazalendo ina wanachama wangapi mpaka sasa?

Jibu: Mpaka sasa tumeshasajili wanachama milioni moja kidijitali na tuna mpango wa kusajili wanachama milioni 10 ifikapo Mei mwaka huu.

Hata hivyo, tulikuwa na wanachama milioni 3.5 ambao hawajaingizwa kwenye mfumo wa kidijitali, bali walipewa kadi za karatasi.

Tutaanza tena usajili ifikapo Februari

Swali: Mmekuwa mkizungumzia kero za wananchi katika ajenda zenu, ni kero gani kubwa inayotesa Watanzania.

Jibu: Changamoto kubwa iliyopo nchini ni ukosefu wa ajira. Tumefika mahali ambapo Serikali ya CCM imeshindwa kuwahakikishia mustakabali vijana.

Kwa mujibu wa utafiti wa Repoa (Taasisi ya Utafiti wa Kuondoa Umasikini), kila mwaka tunaingiza kwenye soko la ajira watu milioni moja, lakini uwezo wetu wa kutoa ajira ni watu 70,000 kwa mwaka, kwa hiyo vijana wanaotarajia kuajiriwa zaidi ya 900,000 wanakosa ajira hizo.

Kuna sekta muhimu kama afya, elimu ambazo kwa uhitaji wake usingetegemea kuwe na wataalamu waliosomeshwa kwa kodi za Watanzania wakose ajira.

Januari mwaka huu, Serikali imetangaza ajira zaidi ya 14,000 na vijana zaidi ya 200,000 wameomba. Sasa utaona hapo, wakati shuleni kukiwa na uhaba wa zaidi ya walimu 270,000 wanaohitajika, lakini Serikali ina uwezo wa kuajiri vijana zaidi ya 14,000 tu.

Unaposhindwa kuajiri walimu, maana yake unashindwa kumwandalia Mtanzania maisha yake ya baadaye.

Leo tunapoandaa Dira ya Taifa ya maendeleo ya 2050, lakini pia tunaandaa vijana wasio na elimu.

Kwa upande wa afya tuna uhaba wa wahudumu wa afya zaidi ya 120,000, lakini mwaka huu 2024/25 bajeti iliyopitishwa ni kuajiri vijana 13,000 tu.

Hata ukiangalia Dira ya Taifa ya Maendeleo, CCM inafikiria kutatua ajira kwa asilimia 50 ifikapo 2050.

Swali: Kwa nini tumefika hapa? Je, ACT Wazalendo mtafanyaje kutatua tatizo hili?

Jibu: Ukisoma ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG) ya 2023 iliyosomwa Machi 2024, CAG amezua hoja ya mahesabu ya fedha kutojulikana zilivyotumika ni Sh3.2 trilioni. Kama fedha hivi zingeweza kuajiri walimu 130,000,

Ikiwa utasoma ripoti za CAG kwa miaka 10 na kuangalia kiwango cha fedha zinazopotea, utagundua tumepoteza zaidi ya Sh50 trilioni, maana yake kama zingepatikana zingetatua tatizo la ajira lililopo. Sisi siyo nchi inayoshindwa kuzalisha ajira.

Related Posts