Wakati taarifa za kuhimiza amani, utulivu na upendo zikisikika Zanzibar katika nyumba za ibada na kwingineko matukio ya vifo, baadhi vya watu waliokuwa mikononi mwa vyombo vya dola zimeshitua watu na kuuliza visiwa hivi naelekea wapi?
Jamaa wa marehemu wawili walioiaga dunia karibuni katika Kijiji cha Kiiungoni, Kusini Pemba, walikataa kupokea maiti hadi sababu ya kifo ichunguzwe na daktari na waione ripoti ya uchunguzi.
Wanafamilia wa hizo maiti mbili walidai kuwekewa shinikizo za kutakiwa kuzika maiti haraka na askari wa Jeshi la Kujenga Uchumi (JKU), ndiyo walisafirisha miili na kuchimba makaburi, jambo ambalo lilionekana kuwa sio la kawaida.
Kwa kawaida, tangu zama za utawala wa kisultani hadi miaka ya karibuni, vinapotokea vifo vya aina hii, kumekuwepo uchunguzi rasmi wa kisheria (inquest) ambao maelezo yake hutolewa mahakamani.
Madhumuni ya uchunguzi ni kumtambua aliyekufa na wakati alioaga dunia, alifia wapi na mazingira yaliyosababisha kifo hicho.
Baadaye ripoti ya daktari aliyeichunguza maiti huwasilishwa mahakamani na hakimu hutoa uamuzi juu ya kifo hicho kuthibitisha kilikuwa ni cha kawaida au mkono wa mtu ulihusika au haukuhusika.
Kwa bahati mbaya, kama alivyoelezea Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Othman Masoud Othman, alipokwenda Pemba vilipotokea vifo vya Othman Hamad Othman (75) na Amour Salim Khamis (28) utaratibu huu wa kisheria haujaonekana kufanyika ipasavyo.
Makamu wa Rais ambaye ni mwanasheria mbobezi na aliwahi kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Mkurugenzi wa Mshitaka, alipofungua jengo la Mahakama ya Mkoa wa Kaskazini Pemba lililopo Kinyasini, Wilaya ya Wete, alitaka ufanyike uchunguzi wa kisheria ili ukweli wa suala hili ujulikane na haki kuonekana inatendeka.
Othman aliitaka Mahakama, Polisi na Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka kuhakikisha unafanyika uchunguzi wa kisheria kwa vifo vyenye utata kama hivyo ambavyo polisi wamekiri kuwakamata watu hao wawili kwa madai ya kuhusika na biashara ya dawa za kulevya.
Lakini yanapotolewa maelezo ya kilichosababisha watu hao kupoteza maisha yao na kwa nini kulikuwa na utata jamaa zao walipokabidhiwa maiti au kuelezwa kwa nini makaburi yalichimbwa na askari wa JKU, jambo ambalo siyo la kawaida.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kusini Pemba, Kamishna Msaidizi Mwandamizi, Abdullah Musa anasema watalichunguza suala hilo na kutoa maelezo.
Hapa inafaa kukumbusha hata katika tukio la vifo vya watu wawili na wengine kujeruhiwa miezi mwili iliyopita katika Kijiji cha Kidoti, kaskazini Unguja, ilidaiwa polisi waliwafyatulia risasi watu waliokuwa katika lori ikielezwa kwamba uchunguzi ungelifanyika. Lakini hadi sasa hakuna taarifa iliyotolewa.
Katika hivi vifo vya Pemba, yapo maelezo yenye utata na imekuwa tabu kujua ukweli ni upi. Jambo lililokuwa halina ubishi ni kwamba watu hao wawili walikufa wakiwa mikononi mwa vyombo vya dola baada ya kuchukuliwa usiku majumbani mwao.
Mwakilishi wa Pandani, Pemba, Profesa Omar Faki na wanafamilia ya marehemu wamevishutumu vyombo vya dola kuhusika na mauaji.
Faki na wanafamilia wanasema miili yote miwili imeonyesha watu hao walipigwa na picha zilizosambazwa zinaonyesha majeraha ya mwili.
Lakini sheha wa eneo hilo, Omar Fakih anadai aliiona miili ya marehemu na ilikuwa safi na haina hata mikwaruzo. Suala ni nani mkweli?
Ni vizuri masuala ya watu kuuawa, iwe mikononi mwa vyombo vya ulinzi au katika matukio ambayo vyombo vya ulinzi vinadaiwa kuhusika na mauaji yakashughulikiwa kwa mujibu wa sheria na siyo utaratibu usioeleweka.
Ni vizuri masuala haya yashughulikiwe kama sheria inavyoelekeza kwa kufunguliwa mahakamani majalada ya uchunguzi wa kisheria.
Polisi wanasema wanachunguza, lakini kwa vile ni askari polisi na wengine wa vyombo vingine vya ulinzi kudaiwa kuwa na mkono katika hivi vifo, siyo vema na siyo sahihi kwa uchunguzi huo kufanywa na polisi peke yao.
Ni vizuri katika uchunguzi huo wakawemo wanasheria huru na masuala haya yakashughulikiwa kisheria na siyo kisiasa au utaratibu unaopangwa na mtu au kikundi cha watu.
Nimesikitika kusikia baadhi ya wanasiasa kutaka Polisi wasiulizwe kuhusu vifo kama hivi vyenye utata kwa madai kwamba kufanya hivyo ni kuingilia kazi ya Jeshi la Polisi.
Ni vizuri wanasiasa wakaelewa kila mwananchi anayo haki ya kutoa maoni anapoona sheria inakandamizwa na haki haitendeki, kwani matukio ya vifo vya watu wakiwa mikononi mwa vyombo vya dola siyo mambo anayostahili kufumbiwa macho na masikio.
Kinachohitajika ni kuona haki inatendeka na kama utafanyika uchunguzi huru na kuonyesha hakuna mkono wa askari, itasaidia kulisafisha Jeshi la Polisi na kurejesha imani ya wananchi kwa walinzi wa usalama wa raia na mali zao.