DC Mgeni acharuka, atoa agizo kukamatwa waliowatia mimba wanafunzi

Same. Mkuu wa Wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro, Kasilda Mgeni ameagiza Jeshi la Polisi wilayani humo kuwasaka wanaume wanaodaiwa kuwapa ujauzito wanafunzi wanne katika kata za Kalemawe na Bendera.

Agizo hilo amelitoa leo Jumatano Januari 15, 2025 wakati wa ziara yake kwenye kata hiyo ya kusikiliza na kutatua kero mbalimbali za wananchi, sambamba na kuhamasisha wazazi kuhakikisha wanawapeleka watoto wao shuleni.

Mgeni amesema; “Serikali imejizatiti kutoa mazingira bora ya elimu kwa watoto wetu, lakini vitendo kama hivi havikubaliki, vinahatarisha maisha ya watoto na kuathiri maadili yetu. Wahusika wote waliowapa ujauzito wanafunzi wa Shule za Msingi na Sekondari watafutwe, wakamatwe na watawajibishwa kwa mujibu wa sheria.”

Mkuu huyo wa wilaya amesisitiza kuwa vitendo kama hivyo havikubaliki katika jamii na kwamba, vinaharibu ndoto za watoto hao wa kike, hivyo kufifisha juhudi za serikali za kumkomboa mwanamke.

Hivyo, ametoa ushauri kwa wazazi na walezi kuwalinda watoto wao dhidi ya vitendo vya ukatili na kuhakikisha wanawalea katika maadili na kumcha Mungu.

Mgeni pia ameagiza kukamatwa kwa wazazi wanaowaficha wanaume waliowapa ujauzito wanafunzi, akisema nao wanashiriki uhalifu huo.

“Endapo tukibaini wazazi walioshirikiana na wanaume waliowapa mimba wanafunzi kwa kupokea kitu kidogo, nao hawatapona. Nimeagiza nao watafutwe na washitakiwe kwa kosa la kuficha wahalifu wa ubakaji,” amesisitiza.

Akizungumza na Mwananchi Digital, Anna Mmbaga, mmoja wa wananchi wa Kata ya Bendera amemshukuru  mkuu wa wilaya kwa kuchukua hatua za haraka.

Hivyo ametoa shime kwa wazazi na walezi wenye watoto hao kutoa ushirikiano kwa serikali kwa lengo la kuhakikisha wahusika wanakamatwa na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.

“Tunamshukuru mkuu wetu wa Wilaya kwa kulivalia njuga jambo hili, linatuguza kama wazazi na tutatoa ushirikiano wa hali na mali,” amesema Mmbanga.

Related Posts