Farida Mangube, Morogoro
Jeshi la Polisi Mkoa wa Morogoro limemkamata dereva Daniel Benaya Mwiluli, mwenye umri wa miaka 39, mkazi wa Makambako, mkoa wa Njombe, kwa tuhuma za uzembe uliosababisha ajali ya gari lililokuwa limebeba mafuta aina ya diesel.
Dereva huyo alikamatwa Januari 15, 2025, katika eneo la Mzambarauni, kata ya Mafisa, wilaya ya Morogoro, baada ya gari lenye namba za usajili T257 EAU/T620 ABG aina ya HOWO kupinduka kutokana na uzembe wa dereva hiyo ambapo hakuna taarifa za vifo vilivyoripotiwa
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro ameendelea kuwakumbusha madereva wa magari ya masafa marefu kuchukua muda wa kupumzika kabla ya safari ili kuzuia ajali zinazosababishwa na uchovu, ulevi, msongo wa mawazo, au usingizi.
Katika tukio hilo, Mrakibu Msaidizi wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji wa Mkoa wa Morogoro, Daniel Ibrahim Mnyara, pia alitoa wito kwa wananchi kuepuka kufika kwenye maeneo ya ajali za mafuta kwa lengo la kuchota mafuta. Alisema vitendo hivyo ni hatarishi kwa maisha yao, mali zao, na vinaweza kuchukuliwa kama wizi.
Jeshi la Polisi limeahidi kuendelea kusimamia sheria na kuchukua hatua stahiki dhidi ya madereva wazembe kwa lengo la kudhibiti ajali barabarani.