Dk Biteko: Maandalizi mkutano wa M300 yafikia asilimia 95

Dar es Salaam. Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko amesema maandalizi kuelekea Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Afrika kuhusu Nishati yamefikia asilimia 95, huku taasisi za kimataifa nazo zikiomba kushiriki.

Maandalizi hayo kwa mujibu wa Dk Biteko, yanahusisha ukarabati wa Kituo cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC), maeneo mengine yatakayotumika na usajili wa wageni walioalikwa na kuomba kushiriki mkutano huo.

Mkutano huo, unatarajiwa kufanyika Januari 27 na 28 mwaka huu, ukiwakutanisha wakuu wa nchi 54 za Afrika, taasisi za kimataifa na viongozi wengine wakuu kutoka nje ya bara hilo.

Kuharakisha upatikanaji wa umeme kwa Waafrika milioni 300 ifikapo mwaka 2030 ndilo hasa jambo litakalojadiliwa katika mkutano huo, ambao Tanzania itakuwa mwenyeji wake.

Dk Biteko ameyasema hayo leo Jumatano Januari 15, 2025 alipokagua ukarabati wa JNICC ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya mkutano huo.

Amesema jambo lililoishangaza Serikali ni kuwepo taasisi nyingi za kimataifa zilizoomba kushiriki, mbali na wakuu wa nchi za Afrika na duniani wanaoendelea kuthibitisha ushiriki wao.

Kwa sababu ya idadi kubwa ya washiriki, amesema maandalizi yanaendelea kufanywa kuhakikisha wageni wote wanapokelewa na tayari yamefikia asilimia 95.

“Kazi nyingine zinazoendelea ni pamoja na usajili na uthibitisho wa wageni ambao watakuja kwa ajili ya ushiriki na ukarabati wa maeneo mengine yatakayotumika kwenye mkutano huu, nichukue nafasi hii kuupongeza uongozi wa Mkoa wa Dar es Salaam kwa hatua iliyofikiwa na kuliweka jiji kwenye mandhari ya kuvutia,” amesema.

Ametumia jukwaa hilo kueleza sababu ya Tanzania kuwa mwenyeji wa mkutano huo ni kuimarika kwa uhusiano wa nchi na mataifa mengine na mafanikio yaliyofikiwa katika sekta ya nishati, ikiwemo usambazaji wa huduma hiyo vijijini.

“Vijiji vyote 12,318 vimesambaziwa umeme na Vitongoji 34,000 kati ya 64,274  vilivyopo nchini,  tayari vimesambaziwa umeme,” amesema.

Amesema katika mkutano huo nchi zitasaini mikakati ya kuharakisha kusambaza umeme kwa wananchi itakayoeleza kwa kina hatua za kuchukuliwa chini ya mwavuli wa Benki ya Dunia na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB).

Faida nyingine, amesema ni kuongezeka kwa fursa za uwekezaji, kuimarisha biashara na kuongeza heshima ya nchi kimataifa.

Akizungumza katika tukio hilo, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila amesema baadhi ya barabara ikiwemo ya Nyerere itapunguziwa magari ili kupunguza msongamano kuanzia Januari 20, mwaka huu.

Amewataka wamiliki wa malori yaliyoegeshwa kando ya barabara hiyo kuyaondosha na watafute maeneo mengine ya maegesho ili kuleta taswira nzuri ya jiji.

Sambamba na hilo, amesema taa za barabarani zinaendelea kufungwa ili kunogesha Jiji na mazungumzo na hoteli mbalimbali yamefanyika ili ziboreshe huduma kwa wageni watakaowasili.

Chalamila amesema mbali na yatakayojadiliwa kwenye mkutano, ugeni huo utatumiwa fursa ya kutangaza utalii wa siasa, tiba na utalii wa vyakula na maeneo maalumu yameandaliwa kwa maonyesho hayo.

Related Posts