Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imepanga Februari 12, 2025 kuanza kusikiliza ushahidi wa kesi ya kuchapisha taarifa za uongo kwa lengo la kupotosha umma, inayomkabili Meya wa zamani wa Manispaa ya Ubungo, Boniface Jacob maarufu Boni Yai.
Jacob (42), ambaye ni Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Pwani na Godlisten Malisa (38), mkazi wa Moshi mkoani Kilimanjaro, wanakabiliwa na kesi ya jinai namba 11805/2024.
Jacob, mkazi wa Mbezi Msakuzi na Malisa wanakabiliwa na mashtaka matatu, mawili kati ya hayo yanamkabili Jacob pekee.
Kesi hiyo ilipangwa leo Januari 15, 2025 kwa ajili ya kuanza kusikilizwa lakini imeshindikana kutokana na hakimu anayeisikiliza, Ushindi Swallo, kupangiwa kazi nyingine.
Wakili wa Serikali, Cuthbert Mbilingi mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Beda Nyaki amesema upande wa mashtaka una shahidi mmoja, Denis Basiyagire.
“Kesi ilikuja kwa ajili ya kuanza usikilizwaji na tayari upande wake mashtaka tunaye shahidi mmoja ambaye yupo mbele ya mahakama yako, lakini hakimu anayesikiliza kesi hii amepangiwa majukumu mengine ya kikazi, hivyo tunaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa,” amesema.
Mshtakiwa Jacob alipoulizwa na hakimu Nyaki, kuhusu mawakili wake kutokuwepo mahakamani alijibu wamepata udhuru.
Baada ya kusikiliza maelezo hayo, hakimu Nyaki alikubaliana na upande wa mashtaka na kuahirisha kesi hiyo hadi Februari 12, 2025 itakapoanza kusikilizwa. Washtakiwa wapo nje kwa dhamana.
Katika kesi nyingine, washtakiwa hao wanashtakiwa chini ya kifungu cha 16 cha Sheria ya Makosa ya Kimtandao namba 14 ya mwaka 2015.
Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, Jacob anadaiwa kuchapisha taarifa za uongo mtandaoni kinyume cha kifungu cha 16 cha sheria ya mtandao.
Jacob anadaiwa kutenda kosa hilo Aprili 22, 2024 ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa lengo la kupotosha umma, alichapisha taarifa za uongo katika mfumo wa kompyuta kupitia mtandao wa kijamii wa X (twitter) wenye jina la Boniface Jocob@ExMayor Ubungo.
Shtaka la pili ni kuchapisha taarifa za uongo mtandaoni kwa lengo la kuipotosha jamii linalomkabili Jacob pekee yake, akidaiwa kutenda kosa hilo Machi 19, 2024 katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Anadaiwa kuchapisha taarifa za uongo katika mfumo wa kompyuta kupitia mtandao wake wa kijamii wa X wenye jina la Boniface Jacob @ExMayor Ubungo kwa kuandika:
“MAUAJI ARUSHA, Mwananchi mwenzetu na aliyekuwa dereva wa magari ya watalii, Omari Msamo ameuawa na askari wa Jeshi la Polisi Wilaya ya Karatu mkoani Arusha.”
Shtaka la tatu ni kutoa taarifa za uongo, linalomkabili Malisa pekee anayedaiwa kulitenda Aprili 22, 2024 katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Malisa anadaiwa kwa nia ovu na kwa lengo la kuupotosha umma na jamii, alichapisha taarifa ya uongo katika mfumo wa kompyuta kupitia mtandao wake wa kijamii wa Instagram wenye jina la Malisa_gj, kwa kuandika ujumbe uliosomeka: “Tarehe 13 Aprili meya mstaafu wa Manispaa ya Ubungo @Exmyor_bonifacejacob alitoa taarifa ya kupotelewa na ndugu yake Bw. Robert Mushi maarufu kama Babu G, ambaye alipotea mapema mwezi Aprili 2024.”
Kwa mara ya kwanza Jacob na Malisa walifikishwa mahakamani Mei 6, 2024 kujibu mashtaka hayo.
Wakati huohuo, upelelezi katika kesi nyingine ya kusambaza taarifa za uongo inayomkabili Jacob, haujakamilika.
Jacob anakabiliwa na mashtaka mawili ya kuchapishaji taarifa za uongo kwenye mtandao wake wa X. Wakili wa Serikali, Mbilingi amedai kesi iliitwa mahakamani kwa ajili ya kutajwa.
Mbilingi ameeleza hayo mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Franco Kiswaga anayesikiliza shauri hilo.
Mshtakiwa alidai mawakili wake wamepata udhuru na bado hawajarudi kutoka likizo.
Hakimu Kiswaga aliahirisha kesi hiyo hadi Februari 12, 2025 kwa ajili ya kutajwa.
Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, Jacob anakabiliwa na mashtaka mawili ya kuchapisha taarifa za uongo katika mfumo wa kompyuta katika akaunti yake ya X kwa nia ya kupotosha umma kinyume cha kifungu cha 16 cha Sheria ya Makosa ya Kimtandao namba 14 ya mwaka 2015.
Katika shtaka la kwanza, anadaiwa Septemba 12, 2024 jijini Dar alichapisha taarifa za uongo zikimhusisha Mkuu wa Upelelezi wa Kanda (ZCO) ya Dar es Salaam, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) taarifa zinasomeka kuwa:
“Mafwele anatuhumiwa na familia nyingi kama mtu ambaye ameshiriki mauaji kwa moja katika kuwapoteza ndugu wa baadhi ya familia zao, kupotea kwa mfanyabiashara Mussa Mziba, kupotea kwa Deo Mugasa, kupotea kwa Adinani Hussein Mbezi, kupotea kwa vijana watano wa Aggrey.”.
Katika shtaka la pili, anadaiwa Septemba 14, 2024 jijini Dar es Salaam alichapisha taarifa za uongo zinazowahusisha wakuu wa upelelezi wa mikoa na utekaji na mauaji ya watu na kutupa miili yao.
Kwa mara ya kwanza alifikishwa mahakamani hapo Septemba 19, 2024 kujibu mashtaka yanayomkabili.