Kocha Stand aukubali mziki wa Geita Gold, ajipanga upya

BAADA ya kumaliza mzunguko wa kwanza Ligi ya Championship kinyonge kwa kuchapwa mabao 3-1 na Geita Gold, Kocha Msaidizi wa Stand United, Feisal Hau amekubali kiwango cha wapinzani wake huku akiwatupia lawama mabeki kwa kukosa umakini.

Timu hiyo ilikubali kichapo hicho mwishoni mwa wiki iliyopita katika Uwanja wa Nyankumbu, mjini Geita na kuhitimisha mechi 15 za mzunguko wa kwanza ikivuna alama 29 na kukamata nafasi ya nne kwenye msimamo wa Championship, huku ikishinda michezo tisa, sare mbili na kupoteza tatu.

Hau alisema mabeki wake walikosa umakini katika mipira ya kutengwa iliyokuwa inatumiwa na Geita Gold na kuruhusu mabao yanayofanana, huku akiahidi kuanza maandalizi ya mzunguko wa pili kwa kurekebisha mapungufu hayo.

Chama la Wana litaanza mzunguko wa pili nyumbani katika Uwanja wa Kambarage, Shinyanga ikiikaribisha Kiluvya United Januari 26, mwaka huu ikihitaji ushindi ili kuendelea kuwania nafasi mbili za juu ikimaliza hapo itarejea Ligi Kuu moja kwa moja.

“Tulienda na mpango kazi wetu tukiamini Geita Gold ni timu inayocheza sana mpira, nikawaambia wachezaji wangu tucheze lakini tuangalie kama watabadilika itakuwa ni timu inayopiga kutokea mbali nasi tubadilike,” alisema Hau na kuongeza.

“Geita Gold walitumia mipira mirefu na kutegemea mipira ya kurusha kwa sababu wana warushaji wazuri wanafikisha mipira golini, nikawaelekeza kipa na mabeki nini cha kufanya lakini ni mapungufu yaleyale niliyowaambia ndiyo yalitudhuru.”

Kocha huyo wa zamani wa Copco FC, aliongeza. “Mabeki wetu hawakuchangamka na kujikuta wakifungwa mabao ya aina moja, tulichokiona hapa tunakwenda kusahihisha isitokee tukakutana na timu aina ya Geita Gold na tukapoteza mchezo kwa mtindo huu.”

Related Posts