WAKATI dirisha la usajili likitarajiwa kufungwa usiku wa leo inaelezwa kuna vita kubwa kati ya vigogo vya Simba na Yanga vikipigana vikumbo kuwania saini ya beki Lameck Lawi.
Iko hivi. Baada ya Simba kukwama kumsajili Lawi katika dirisha lililopita kisha beki huyo kukwama kuuzwa Ubelgiji, Kamati ya Sheria na Hadhi za wachezaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), ilizitaka pande hizo Coastal Union na Wekundu hao kukaa mezani na kumalizana kwa maridhiano.
Wakati timu hizo mbili zikijivuta kwa kikao hicho Yanga ikaingilia ugomvi huo kwa siri ikitaka kumsajili kimafia Lawi kwa kumpandisha bei na kufikia sehemu nzuri.
Yanga inataka kuipiga bao Simba kwa kumpa Lawi Sh150 Milioni kwa mkataba wa miaka mitatu wakati Wekundu hao wako tayari kumpa Sh130 Milioni.
Ofa hiyo ya Yanga ilimchanganya beki huyo na akili yake kubadilika fasta na klabu ya Coastal Union ikitangaziwa udhamini mnono na moja ya wadhamini wa watetezi wa Ligi Kuu Bara.
Ghafla, Simba ikapata taarifa hiyo na kuliamsha upya faili la mazungumzo na Coastal kuhusu Lawi.
“Hatuna shida ya kumuuza Lawi kwa Simba, lakini kila mmoja anataka kufanya biashara sehemu ambayo anaona maslahi ni mazuri, ukizipima ofa hizi mbili unaona namna ilivyo ngumu kukimbia kile wanachotaka kufanya Yanga,” alisema bosi mmoja wa Coastal Union.
“Bado mvutano unaendelea na kama unavyojua leo dirisha linafungwa tutaona nani atakuwa amefanikiwa kumalizana na Coastal Union.”
Timu zote zina uhitaji wa beki wa kati, huku Simba inataka kumsajili beki huyo ili akamuongezee presha Fondoh Che Malone, ambaye wanadai amekuwa na makosa mengi kwenye mechi za siku za hivi karibuni.
Yanga wanataka beki wa kati kufuatia kocha Sead Ramovic kuhitaji beki wa maana atakayekuja kuwasaidia Ibrahim Bacca na Dickson Job.
Timu hizo zinazoshiriki michuano ya kimataifa, Yanga ikiwa Ligi ya Mabingwa na Simba Kombe la Shirikisho Afrika, wikiendi hii zitacheza michezo ya mwisho nyumbani dhidi ya timu kutoka Algeria.
Simba itacheza Jumapili na CS Constantine katika mechi ya kuamua timu ipi imalize nafasi ya kwanza na ya pili katika Kundi A, huku Yanga itaumana na MC Alger katika Ligi ya Mabingwa, ikisaka tiketi ya kucheza robo fainali kutoka Kundi A, huku wageni wote walishinda nyumbani dhidi ya vigogo hivyo.
Yanga ilicharazwa mabao 2-0 na MC Alger yenye pointi nane kwa sasa, moja zaidi na ilizonazo Yanga yenye saba, wakati Simba ililala kwa mabao 2-1 kwa Constantine yenye pointi 12 kileleleni katika Kundi A, mbili zaidi ya walizonazo Wekundu hao ambao wote wawili kwa sasa wameshafuzu robo fainali.