Mauwasa yaongeza muda wa upatikanaji wa maji, sasa ni saa 18

Maswa. Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira mjini Maswa (Mauwasa) katika kuboresha huduma za maji kwa wakazi wa Maswa mkoani Simiyu, imeongeza muda wa upatikanaji wa maji kutoka saa 12 hadi 18 kutokana na kukamilika ujenzi la tenki la maji lenye ujazo wa lita milioni moja.

Mkurugenzi mtendaji wa Mamlaka hiyo, Nandi Mathias ameyasema hayo leo Jumatano Januari 15, 2025 wakati akizungumza na Mwananchi Digital baada ya kutembelea eneo linalojengwa tenki hilo.

Amesema kukamilika kwa tenki hilo kwa gharama ya zaidi ya Sh900 milioni, ni moja ya maboresho ya mfumo wa usambazaji maji wa mamlaka hiyo kwa wananchi wanaowahudumia.

 “Kukamilika kwa ujenzi wa tenki hili la maji lililopo kwenye kilima cha Nyalikungu mjini Maswa limetusaidia katika usambazaji maji na kuongeza muda wa upatikanaji wa maji kutoka masaa 12 hadi 18 kwa siku,” amesena.

Mathias amesema hiyo kwa upande wao ni hatua muhimu katika kuhakikisha upatikanaji wa huduma bora kwa wananchi zaidi ya 200,000 ambao wanawahudumia. 

Pia Mathias amesema hatua hiyo itasaidia kupunguza changamoto za upatikanaji wa maji safi na salama sambamba na kuimarisha maisha ya wakazi wa eneo hilo na vijiji 14 vinavyohudumiwa na mamlaka hiyo.

“Ongezeko hili la saa sita linatarajiwa kuwa na manufaa makubwa kwa jamii, hasa katika shughuli za kila siku zinazohitaji matumizi ya maji,” amesema.

Hata hivyo, amesema bado wanaendelea na ukamilishaji wa tenki la kuhifadhi maji linalojengwa katika Kijiji cha Hinduki ambalo litakuwa na uwezo wa kujaza lita milioni mbili  litakapokamilika na watatoa huduma ya maji kwa saa 24.

Caroline Shayo mkazi wa Mtaa wa Uzunguni anasema licha ya mamlaka hiyo kuongeza muda wa upatikanaji wa maji kwa zaidi ya saa sita, hitaji lao ni kupata maji kwa saa 24.

“Pamoja na jitihada hizi zinazofanywa na Mauwasa kuongeza muda wa upatikanaji wa maji zaidi ya masaa sita, ni vizuri wakaongeza muda ukafika masaa 24 ili yapatikane kwa siku nzima kutokana na umuhimu wake,” amesema.

Related Posts