Mjadala kumulika fursa, changamoto sekta ya nishati safi

Dar es Salaam. Wadau nchini wamepanga kujadili mikakati ya kuongeza matumizi ya nishati safi ya kupikia katika kaya za Kitanzania ili kupunguza athari za kiafya na kimazingira zinazohusiana na matumizi ya kuni kwenye shughuli za kupikia.

Miongoni mwa dhumuni la majadiliano hayo ni kutimiza lengo la Serikali linalotaka asilimia 80 ya Watanzania watumie nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034.

Katika kutimiza hilo, Shirika la Umoja wa Mataifa la Mitaji na Uwekezaji (UNCDF) kwa kushirikiana na Mhadhiri Mkuu, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Innocent Pantaleo limeandaa warsha itakayokuja na mapendekezo yatakayowezesha jamii kutumia nishati hiyo katika matumizi yao.

Sambamba na hilo mjadala huo una lengo la kijadili vipengele muhimu ambavyo ni vikwazo vya soko, fursa za msaada wa kifedha, na marekebisho ya sera yanayohitajika pamoja na vifaa vya nishati safi ya kupikia.

“Warsha hii ya kujadili matumizi ya nishati safi ni hatua muhimu kuoanisha jitihada za mashirika ya umma na binafsi kufikia malengo ya pamoja katika sekta ya kupikia nishati safi,” amesema Mshauri Mkuu wa Kiufundi, UNCDF Tanzania, Peter Malika.

“Matokeo ya utafiti wetu yanakusudiwa kutoa mwongozo kwa CookFund kuhusu maeneo ya marekebisho ili kufikia malengo ya programu ambayo yanalingana na vipaumbele vya serikali kuhusu nishati safi,” ameongeza.

Pamoja na mada hizo warsha hiyo itajumuisha mikakati ya kuongeza uhamasishaji wa kutumia nishati safi ya kupikia, kuboresha upatikanaji wa vifaa vikiwemo majiko ili vipatikane kwa bei nafuu, na kuanzisha mifumo madhubuti ya sera kusaidia ukuaji endelevu wa sekta hii.

Kadhalika, warsha inatoa fursa ya kipekee ya kuboresha na kuoanisha jitihada za sekta nzima ili kuhakikisha mipango yote inaelekezwa kwenye kutoa matokeo ya kudumu.

Warsha hii itawakutanisha wadau muhimu kutoka katika sekta hiyo ikiwa ni pamoja na wawakilishi kutoka taasisi za umma, taasisi za kibinafsi, na washirika wa maendeleo.

Sambamba na hilo tukio hili litakuwa jukwaa la kubaini fursa za ushirikiano kati ya wadau ili kusukuma mbele ajenda ya nishati safi ya kupikia nchini Tanzania.

Kuelekea kwenye mikakati ya kitaifa ya nishati safi ya kupikia iliyowekwa na Serikali ya Tanzania, Programu ya CookFund inayosimamiwa na UNCDF na kufadhiliwa na Umoja wa Ulaya inalenga kuhakikisha kaya zinatumia nishati hiyo.

Lengo ni kupunguza athari za kimazingira na kiafya zinazohusiana na matumizi ya kuni kunakosababishwa na kukatwa miti, pamoja na kusaidia mabadiliko ya tabianchi.

Kupitia programu hii, UNCDF na washirika wake wanajitahidi kujenga soko imara na endelevu katika sekta ya nishati safi ili kusaidia kaya na kuboresha uchumi wa nchi.

Related Posts