Unguja. Wakati ukizinduliwa mpango mkakati wa kisekta wa lishe Zanzibar wa miaka mitano, Makamu wa Pili wa Rais, Hemed Suleiman Abdulla amezitaka wizara na taasisi zinazohusika kujipanga kuutekeleza, iwapo wakishindwa wajihesabu hawana kazi.
Hemed amesema licha ya mafanikio na jitihada kubwa zinazochukuliwa, bado kuna kiwango kikubwa cha matatizo ya lishe duni.
Mpango mkakati huo wa kisekta wa lishe Zanzibar wa miaka mitano (2025 hadi 2029), umeandaliwa na Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (Unicef), umezinduliwa leo Januari 15, 2025 mjini Unguja, Hemed akiwa mgeni rasmi.
“Tutakuwa na tathmini kila baada ya miezi mitatu, nikiongoza vikao hivyo mwenyewe, tukihusisha mawaziri, makatibu wakuu na wataalamu wengine wanaohusika na lishe, taasisi au mtu yeyote inayehusika ajipange vizuri akishindwa kukamilisha mpango ajihesabu kwamba ameshindwa kazi ya aliyemteua (Rais),” amesema Hemed.
“Nitataka kuona kila wizara imejiandaa namna inavyotekeleza mpango huu wakati mwingine watu wanakwamisha mambo makusudi,” amesema.
Ameiagiza Wizara ya Afya kuona kitengo cha lishe kifanye kazi kwa kuwezeshwa vitendea kazi kwani mpango huo ni mkubwa.
“Ninasema haya ili tukae vizuri ili kwenye ufuatiliaji tusije kuonana wabaya, tusisimame hapa tukapoteza muda tunapaswa tutekeleze iwapo kuna changamoto naomba nijulishwe mapema.
Katika kusisitiza hilo, Hemed amesema; “Kuna kasumba moja fedha za safari kwenda Dodoma, Dar es Salaam, kwenda Pemba zinapatikana lakini fedha za kutembelea kwenye kitengo unaambiwa hazipatikani hili haliwezekeni, nasema haya ili tusije kuonana wabaya baadaye.”
Akitoa taarifa ya kitaalamu, Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Zanzibar, Dk Mngereza Miraji Mzee amesema lishe duni bado ni changamoto kubwa kwa afya ya jamii ya Zanzibar, hasa miongoni mwa watoto, vijana na wanawake wenye umri wa kuzaa.
Tatizo hilo ni pamoja na udumavu, uzito mkubwa na upungufu wa virutubishi mwilini, hususani upungufu wa damu na kuongezeka kwa magonjwa yasiyoambukiza kutokana na ulaji usio sahihi.
Kwa mfano, utafiti wa Demografia na Afya (DHS-MIS) wa mwaka 2022 umeonyesha kuwa, kwa upande wa Zanzibar, asilimia 17 ya watoto chini ya miaka mitano wanakabiliwa na udumavu, asilimia 8.2 wanakabiliwa na ukondefu, na asilimia 14.7 wanakabiliwa na uzito pungufu,” amesema.
Pia amesema zaidi ya asilimia 60 ya watoto chini ya miaka mitano wanakabiliwa na tatizo la upungufu wa damu, huku wanawake wenye umri wa kuzaa wakikabiliwa na kiwango kikubwa cha tatizo hili.
Kwa mujibu wa Dk Mngereza, utafiti wa STEP wa mwaka 2023 pia umeonyesha kuwa asilimia 43.4 ya watu Zanzibar wanakabiliwa na tatizo la uzito mkubwa, hali inayochangia kuongezeka kwa matatizo yasiyoambukiza kama shinikizo la damu.
Pia, utafiti wa Afya na lishe kwa vijana uliofanyika mwaka 2022 umeonyesha kuwa zaidi ya asilimia 45 ya vijana wenye umri wa kwenda shule wana upungufu wa damu, na zaidi ya asilimia 50 ya watoto wanakwenda shule bila kifungua kinywa.
Kiwango cha udumavu kwa watoto hao ni asilimia 13.9, kiwango cha ukondefu ni asilimia 15.6, na asilimia 8.4 wanakabiliwa na tatizo la uzito kupita kiasi.
Ametaja miongoni mwa sababu zinazochangia matatizo haya ya lishe ni ulaji usiofaa, ambapo takwimu zinaonyesha kuwa watu wengi wanatumia vyakula vya kukaanga na nafaka, hali inayohatarisha afya zao.
“Ili kushughulikia hali hii, Wizara ya Afya, kwa kushirikiana na wizara nyingine, ina uhitaji wa kutekeleza mpango wa pamoja ili kuhakikisha kwamba changamoto hizi za lishe zinapungua au kuondoka kabisa,” amesema Dk Mngereza.
Waziri wa Afya Zanzibar, Nassoro Ahmed Mazrui amesema wizara ya afya ina jukumu la kutekeleza na kuimarisha huduma za lishe ili kuboresha afya ya mama na mtoto, ikiwa ni hatua muhimu katika kupunguza vifo vya mama na mtoto Zanzibar.
Pamoja na jukumu hilo, Wizara inalenga pia kuboresha viashiria vya lishe kwa watoto chini ya miaka mitano kwa kupunguza ukondefu, uzito mdogo, na udumavu; pamoja na kupunguza tatizo la upungufu wa damu kwa wanawake wenye umri wa kuzaa (miaka 15-49) na watoto chini ya miaka mitano.
“Kupitia mpango mkakati huu, wizara inategemea kufanya kazi mbalimbali katika kuimarisha shughuli za lishe ikiwa ni pamoja na kutengeneza kamati za lishe katika ngazi za mikoa na wilaya,” amesema Mazrui.
Naye mwakilishi wa Unicef Tanzania, Elice Wisch amesema wataendelea kuisaidia Zanzibar katika kuboresha mifumo ya lishe.