Mrithi wa Kinana CCM huyu hapa

Dar/Dodoma. Wakati Chama Cha Mapinduzi (CCM) kikijipanga kufanya mkutano mkuu maalumu kuanzia Januari 18 hadi 19, 2025, Waziri Mkuu mstaafu, Mizengo Pinda, anatajwa zaidi kumrithi Abdulrahman Kinana katika nafasi ya Makamu Mwenyekiti – Bara, Mwananchi limedokezwa.

Mbali na Pinda, wengine wanaotajwa kukalia kiti hicho cha juu kwenye chama hicho tawala ni mwanasiasa mkongwe Stephen Wasira na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Tanga, Rajab Abdallah.

Nafasi hiyo ya makamu mwenyekiti imekuwa wazi tangu Julai 28, 2024, baada ya Kinana kuandika barua ya kuomba kujiuzulu wadhifa huo kwenda kwa mwenyekiti wake, Rais Samia Suluhu Hassan.

Kinana, aliyewahi kuwa Katibu Mkuu wa chama hicho, alirejea kwenye nafasi ya makamu mwenyekiti Aprili mosi, 2022, alipochaguliwa na wajumbe wa mkutano mkuu kwa kura za “ndiyo” 1,875 sawa na asilimia 100.

Alichaguliwa akichukua nafasi ya Philip Mangula, aliyeandika barua ya kung’atuka kwa Mwenyekiti wa CCM, Rais Samia, ambaye aliridhia.

Tangu Kinana alipojiuzulu, nafasi hiyo imebaki wazi kwa kipindi cha takriban miezi mitano, jambo ambalo ni la kipekee katika historia ya chama hicho.

Kwa mujibu wa Katiba ya CCM, nafasi ya makamu mwenyekiti ni muhimu katika kumsaidia mwenyekiti wa chama kutekeleza majukumu yake.

Kwa mujibu wa Katiba ya CCM, makamu mwenyekiti ni wasaidizi wakuu wa mwenyekiti na watafanya kazi zote za chama watakazopewa na mwenyekiti.

Taarifa ambazo Mwananchi limezipata kutoka vyanzo mbalimbali serikalini na CCM, jina la Pinda ndilo linatajwa zaidi kwenda kumrithi Kinana katika nafasi hiyo ya juu ndani ya chama tawala na mshauri mkuu wa mwenyekiti.

“Hatuhitaji kwenda kwenye mkutano mkuu na majina mengi, litakwenda moja tu la mzee Pinda. Anatosha kabisa kwa uzoefu wake; anakijua chama, na ni mtulivu asiyekuwa na mawaa,” amesema mmoja wa viongozi waandamizi wa CCM.

Kiongozi huyo, aliyeomba hifadhi ya jina lake, amesema Pinda mwenye miaka 76, kwa nyadhifa alizoshika, anastahili hususan kipindi hiki kuelekea uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 2025.

“Unajua huu mwaka ni wa uchaguzi, ni uchaguzi ambao tunatarajia utakuwa na vuta nikuvute, hasa ukizingatia mazingira ya mwaka 2020, kwa hiyo tunapaswa kuwa na makamu mwenyekiti ambaye ndiye mwenyekiti wa maadili asimamie mchakato vizuri.

“Huyu mzee hana cha kupoteza, hana makundi, hana makando kando yaani unaweza kusema ni mtu ‘smart’ asiyetiliwa shaka na uadilifu wake. Kwa hiyo wacha mtoto wa mkulima tumpe jukumu hili,” amesema.

Pinda, maarufu kama “Mtoto wa Mkulima,” alizaliwa Agosti 12, 1948, mkoani Rukwa. Alianza kazi serikalini kabla ya kuchaguliwa kuwa mbunge wa Mpanda Mashariki mwaka 2000.

Mwaka 2005 hadi 2008, alihudumu kama Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi). Februari 2008, baada ya sakata la Richmond, aliteuliwa kuwa Waziri Mkuu wa Tanzania, nafasi aliyohudumu hadi Novemba 2015.

Baada ya kustaafu, Pinda amebaki kuwa mmoja wa makada wakongwe wa CCM, akijulikana kwa busara na weledi wake katika siasa za Tanzania.

Katika korido za CCM, Wasira ambaye ni waziri mwandamizi mstaafu mwenye uzoefu ndani ya Serikali na chama anatajwa tajwa kukalia kiti hicho.

Wasira amehudumu kama waziri enzi za utawala wa awamu ya kwanza ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, awamu ya pili ya Ali Hassan Mwinyi, awamu ya tatu ya Benjamin Mkapa na awamu ya nne ya Jakaya Kikwete.

Pia, Abdallah ambaye ni Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Tanga ambaye miezi ya karibuni aliteuliwa kuwa Mjumbe wa Kamati Kuu kutokana na aina zake za siasa, naye anatajwa huenda akawa mrithi wa Kinana.

Mitazamo wachambuzi wa siasa

Wachambuzi wa siasa wametofautiana kuhusu nani anayefaa kuwa mrithi wa nafasi hiyo ya Makamu Mwenyekiti – Bara.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Dk Conrad Masabo, amesema makada kama Pinda na Wasira ni vyema wakapumzishwa na kuendelea kutoa ushauri wa masuala mbalimbali.

“Kwa maoni yangu, si sahihi kuwarudisha kwenye kashikashi kina Pinda na Wasira kwa sababu walifanya kazi kubwa. CCM ina watu wengi; wawatumie wengine, ikiwemo huyo (Rajab). Sioni haja ya kuwarudisha hawa wazee kuwarudisha tena kwenye umakamu,” amesema.

Dk Masabo amependekeza vijana wenye uwezo mkubwa wa kushika nafasi hiyo wapewe nafasi, akitaja umuhimu wa kuheshimu taratibu za chama kuelekea uchaguzi mkuu.

Kwa upande wake, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Aviti Mushi, amesema Pinda ndiye anayefaa zaidi kwa sababu ya uzoefu wake wa uongozi.

Leo, Jumatano Januari 15, 2025, Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Amos Makalla, amesema vikao vya Kamati Kuu na Halmashauri Kuu vitafanyika Ijumaa Januari 17, 2025, jijini Dodoma.

Makalla amesema vikao hivyo ni sehemu ya maandalizi kuelekea mkutano mkuu maalumu utakaofanyika kuazia Januari 18 hadi -19, 2025.

Katika mkutano wake wa Januari 7, 2025, akizungumza na waandishi wa habari, Makalla amefafanua utaratibu wa kumpata makamu mwenyekiti, akisema: “Nafasi ya makamu mwenyekiti haigombewi; haujazi fomu. Ni mapendekezo ya Kamati Kuu na Halmashauri Kuu.”

Alisema jina la makamu mwenyekiti likipatikana kutoka kwa vikao hivyo litapelekwa mkutano mkuu kwa ajili ya kupigiwa kura.

Related Posts