Arusha. Maambukizi kwenye mapafu yaliyosababisha matatizo ya kupumua ndicho kinachotajwa kuwa chanzo cha kifo cha aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Mbozi mkoani Songwe, Ester Mahawe.
Ester amefariki dunia jana Januari 14, 2025 katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kaskazini (KCMC) Moshi, mkoani Kilimanjaro alikokuwa akipatiwa matibabu ya msaada wa hewa ya Oksijeni kwa ajili ya kumwezesha kupumua.
Hayo yameelezwa leo Jumatano, Januari 15, 2025 na mume wa marehemu, Alexander Samson alipozungumza na gazeti hili, nyumbani kwake Ngaramtoni jijini Arusha.
Amesema mkewe (Ester) aligundulika kuwa na maambukizi ya mapafu Januari mosi mwaka huu.
“Awali Agosti 2024 aliwahi kuugua ugonjwa wa kansa ya ziwa la kulia na alipata matibabu nchini India ikiwemo kukatwa ziwa na kutumia dawa hadi baadaye ulipoonekana ugonjwa umetoweka na kurudi nyumbani kuendelea na majukumu yake,” amesema.
Baada ya kurejea kazini, amesema mkewe alianza na jukumu la kuzunguka katika maeneo mbalimbali kufanya kampeni za wenyeviti wa serikali za mitaa.
“Alivyomaliza tu kampeni akaanza kusumbuliwa na shida ya kupumua na tulihudhuria hospitali ya Ocean Road, Dar es Salaam na alikutwa na maambukizi kwenye mapafu na akaanza matibabu,” amesema Samson.
Baadaye Desemba 17, 2024 amesema mkewe alihamia katika Hospitali ya Lugalo kwa ajili ya matibabu yakiwemo ya kuwekewa mashine ya oksijeni ya kumwezesha kupumua, alipopata nafuu walirudi Arusha kwa sharti ya kuhudhuria hospitali baada ya wiki mbili.
“Asubuhi ya January 13, 2025 alitakiwa kurudi kliniki lakini usiku wa kuamkia siku hiyo, alionyesha kuzidiwa zaidi na tukazungumza na daktari wake aliyeko Lugalo ambae alituma gari la wagonjwa (Ambulance) kwa ajili ya kuja kumchukua na saa tano alifika nyumbani hapa na tukaanza safari” amesema na kuongeza;
“Tulipofika ‘Kwa Sadala’ alionyesha kuzidiwa na kusema anataka huduma ya dharura hivyo tuliamua kukatisha na kumuwahisha katika hospitali ya karibu ambayo ni Hospitali ya Rufaa ya KCMC na kueleza shida kisha akaanza kupatiwa huduma lakini hali ilizidi kuwa mbaya ikalazimu aingizwe chumba cha wagonjwa mahututi kupatiwa huduma ya oksijeni,” amesema.
Amesema ilipofika saa 7 usiku, Daktari Mkuu wa KCMC aliwaamuru waahirishe safari, hivyo gari la wagonjwa lilirudishwa.
“Bahati mbaya saa 5 asubuhi ya Januari 14, 2025 muda uleule tuliompandisha gari ndio akakata roho akipambania uhai wake,” amesimulia mume huyo wa Ester.
Samson amesema mara ya mwisho kuongeza na mkewe ilikuwa siku aliyoingizwa kwenye chumba cha wagonjwa mahututi na alimsihi awalee watoto iwapo hatapona.
Kwa mujibu wa mume huyo, alimkuta Ester na watoto wawili naye alikuwa nao saba, kwa kuwa walizaa mmoja pamoja, jumla walikuwa na watoto 10.
“Wakati anaingizwa ICU aliniita na kuniambia, mume wangu naona kama sitarudi lakini nakuomba nisipopona walee watoto wetu na baada ya kusema hivyo aliondoshwa ikawa mwisho wangu na yeye kuongea hadi napewa taarifa ya kifo chake,” amesema.
Kaka wa marehemu, Thomas Mahawe amesema mwili wa marehemu umehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti katika Hospitali ya Rufaa Mount Meru kusubiri taratibu za maziko, yatakayofanyika nyumbani kwake Jumatatu.
“Katika kuepuka usumbufu wa baadaye baada ya kugundua amefariki tuliamua hapo hapo kuuhamisha mwili wa mpendwa wetu hadi Arusha katika Hospitali ya Mount Meru,” amesema.
Amesema shughuli za maziko zitafanyika Jumatatu Januari 20, 2025 katika makaburi ya familia yaliyoko hapohapo nyumbani kwake Ngaramtoni, Arusha.
“Kabla ya kuzikwa tutatoa nafasi ya wageni, ndugu jamaa na marafiki wakiwemo viongozi wa Serikali kutoa heshima za mwisho kwa mpendwa wetu na baadaye itafuatiwa na ibada fupi ya kumuombea itakayoongozwa na Askofu Mkuu wa Kanisa la Wasabato kanda ya kaskazini Mark Walwa alikokuwa anasali marehemu” amesema.
Viongozi wenzake wamlilia
Baada ya taarifa za msiba, Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evansi Mtambi na Wakuu wa Wilaya za Kilwa mkoani Lindi (Mohamed Nyundo), Mkuu wa Wilaya ya Nanyumbu mkoani Mtwara (Christopha Magala) na Mkuu wa Wilaya ya Buhigwa mkoani Kigoma (Michael Ngayalina) walifika nyumbani.
Akizungumza na Mwananchi Digital, Kanali Mtambi amesema alifahamiana na marehemu tangu walipokuwa masomoni pamoja na walionana tena miaka 10 baadaye.
“Ester alikuwa jasiri na mpambanaji akijua nini maana ya maisha na akipambana katika kusaka mafanikio yake, pia alikuwa anaamini katika usawa, kuheshimu na misingi ya ndoa lakini kuheshimu watu wengine” amesema.
Amesema wamekuwa wakikutana mara nyingi kwenye shughuli mbalimbali, hivyo anabaki kuwa alama ya urafiki kwake.
“Nimekuja Arusha jana kwenye vikao vya kikazi nikijua pia nitamuona lakini bahati mbaya nikapata taarifa za msiba huo ambao umekuwa mgumu na mzito kwangu kukubaliana na hali halisi lakini baada ya kuhudhuria msibani hapa leo nimeamini kuwa amefariki, kiukweli inauma lakini nitabaki kumuombea heri huko akhera” amesema.
Akizungumza kwa niaba ya wakuu wa wilaya wenzake, Mkuu wa Wilaya ya Buhigwa, Ngayalina amesema watamkumbuka kwa uchapakazi wake na upendo zaidi kwa watumishi wenzake.
“Tupo hapa kumfariji mume wa marehemu, binafsi nimefanya kazi na Ester akiwa Mkuu wa Wilaya ya Kigoma ambapo alikuwa dada mwema na rafiki lakini pia mchapa kazi hodari na mkweli katika majukumu yake” amesema.
Kanisa nao wamlilia Ester
Akizungumza msiba huo, Askofu Mkuu wa Kanisa la Wasabato Kanda ya kaskazini alikokuwa anasali marehemu, Mark Walwa amesema watamkumbuka Ester kwa mengi, ikiwemo michango yake katika shughuli mbalimbali za maendeleo kwa matawi ya kanisa hilo.
“Ester amekuwa baraka sana tangu namfahamu akiwa muumini mwaminifu na akishiriki ibada ya huduma mbalimbali za kanisa na maendeleo huku akichangia kila penye mahitaji” amesema.
Ester Mahawe amezaliwa Novemba 5, 1973 katika Kijiji cha Isale wilayani Mbulu, Manyara.