Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amefanya uteuzi wa wenyeviti wa bodi viongozi mbalimbali akiwemo Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Ramadhan Lwamo.
Uteuzi wa Lwamo umekuja ikiwa ni takribani miezi saba baada ya kuteuliwa kushika wadhifa huo akichukua nafasi ya Yahaya Samamba aliyeteuliwa kuwa Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini.
Mbali na uteuzi wa mtendaji mkuu wa tume ya madini, Rais Samia amewateua pia wenyeviti wa bodi wa taasisi nne za Serikali ambao wote wanahudumu katika nafasi hizo kwa kipindi cha pili.
Walioteuliwa ni Dk Aggrey Mlimuka ambaye ameteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Tume ya Ushindani (FCC).
Profesa Othman Chande Othman naye kuendelea na nafasi ya uenyekiti wa Bodi ya Shirika la Viwango Tanzania (TBS).
Dk Florens Turuka ameteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Kampuni ya Mbolea Tanzania (TFC) na Profesa Valerian Silayo ameteuliwa kuendelea na awamu ya pili ya uongozi katika nafasi ya Mwenyekiti wa Bodi ya Kituo cha Zana za Kilimo na Teknolojia Vijijini (CAMARTEC).