TAAMULI HURU: 4R zitumike kuponya makovu ya Mapinduzi ya Zanzibar

Jumapili ya Januari 12, 2025 imedondokea siku ileile ya Mapinduzi ya Zanzibar yaliyotokea Jumapili ya Januari 12, 1964. Tanzania imeadhimisha miaka 61 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar.

Wakati Wazanzibari wengi wanashereheka kuyapongeza Mapinduzi hayo na wengine hadi kuyapa utukufu kwa kuyaita Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar, ambapo neno utukufu kwa dini mbili kuu, Wakristu na Waislamu, maana yake ni kwake yeye tu na utukufu ni wake yeye tu, Mwenyezi Mungu, hivyo kuita kitu kingine chochote kitukufu ni kama kufuru.

Kuna Wazanzibari wengine, japo wachache, siku hii ya Mapinduzi ya Zanzibar, kwao ni siku ya kumbukumbu chungu na mbaya kwa kutonesha makovu ya mapinduzi hayo, kwa kuwapoteza wapendwa wao kutokana na umwagaji damu wakati wa Mapinduzi hayo na baada ya Mapinduzi.

Japo hakuna ubishi kabisa kuwa Mapinduzi ya Zanzibar yameleta neema na heri Zanzibar, lakini pia ni ukweli mchungu kuwa mapinduzi hayo yalimwaga damu za watu na pia yalisababisha maumivu makubwa kwa waliopinduliwa ambao wanaishi na makovu ya Mapinduzi hadi leo, hivyo makala ya leo ni kutoa wito, kuzitumia 4R za Rais Samia Suluhu Hassan kutibu makovu ya Mapinduzi hayo na keleta siasa za utengemano Zanzibar.

Katika mtandao wa Jamii Forums, shamra shamra za kuisubiria siku hii ya Mapinduzi ya Zanzibar, zilianza siku nyingi kabla kwa kushamirishwa na taarifa kuwa Sultan aliyepinduliwa angerejea Zanzibar kwa ziara rasmi na angehudhuria maadhimisho ya mwaka huu.

Hilo la Sultani kurejea mimi nikalidaka na kuchangia kwa kulitolea mapendekezo yangu 10 kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Ndipo kaka yangu mmoja kutoka Zanzibar, naomba kumtaja kwa jina moja tu, kaka Chalz, aliyenipokea RTD miaka ya nyuma, akaniuliza una uhakika na chanzo chako cha habari kuwa hii ni habari ya kweli? Nikamjibu kwa vile imetangazwa na Jamii Forums, ambacho ni chombo cha kuaminika, ingekuwa feki, JF inatumia mfumo wa Jamii Check kubaini taarifa za uongo na kuzifuta, hivyo itakuwa kweli.

Ndipo nikaipitia ile habari kwa mara ya pili kuisoma source, nikakuta ni mtu kutoka Oman. Nikamtafuta kaka yangu mwingine Zanzibar, huyu ni Mzee Salim Said Salim, mwandishi wa siku nyingi, tunamuita Mzee SSS, yeye ana nasaba kidogo na ukoo wa Sultan. Salim akawapandia kwa simu Oman, familia ya Sultan wakakanusha kuwa hiyo habari ni fake news (ya uongo). Asante Mzee SSS!

Ndipo nikawasiliana na Mkuu wa JamiiForums, Maxence Mello, kumweleza hiyo habari ya Sultani kurejea ni ya uongo. Nikamrudia Kaka Chalz, nikamshukuru kwa angalizo lake, lakini nikamwambia baadhi ya yale mapendekezo yangu 10 kwa SMZ, mengine bado ni muhimu kwa Zanzibar ya sasa, yafanyiwe kazi.

Baada ya lile jibu la familia ya Sultani kule Oman, kukanusha ile fake news, Sultani alishinda siku moja tu, na kesho yake akatwaliwa kwa Mola wake. Nikamshauri Kaka Chalz, SMZ iseme kitu, haikusema! Ukimya huo wa hata kupeana pole za msiba ukanikumbusha bado Zanzibar kuna fukuto la Mapinduzi.

Huu ni mwaka wa uchaguzi na hakuna ubishi siasa za Zanzibar, licha ya uwepo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK), bado zinaathiriwa na mzimu wa machozi, jasho na damu, zilizomwagika wakati wa mapinduzi na kuna watu bado wana makovu ya mapinduzi, hivyo 4R za Rais Samia zikitumiwa kikamilifu zinaweza kuyatibu.

Hivyo matokeo ya baadhi ya chaguzi za Zanzibar, ni matokeo yaleyale ya ule uchaguzi wa mwaka 1963. Mfano mzuri ni uchaguzi wa mwaka 2015, kuna msemo wa Kiingereza unaosema namba haziongopi.

Matokeo ya Tume ya Uchaguzi wa mwaka 2015 kwa Zanzibar, yamethibitisha pasi na shaka kuwa uchaguzi wa Zanzibar wa mwaka 2015, kama usingefutwa Maalim Seif Shariff Hamad wa Chama cha Wananchi (CUF) ndiye angelikuwa mshindi wa uchaguzi wa Rais wa Zanzibar kwa kutumia kigezo cha matokeo ya uchaguzi wa urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, uliosimamiwa na NEC kule Zanzibar ambao uchaguzi haukuwa na dosari.

Hii maana yake Zanzibar upinzani unaweza kushinda, sasa kwa vile bado kuna uadui wa machungu ya Mapinduzi, siku upinzani ukishinda Zanzibar, kutaibuka kulipiza kisasi.

Nilishauri Zanzibar iitumie R ya maridhiano, ianzishe Tume ya Ukweli na Maridhiano, watu waruhusiwe kutoa machungu yao ya mapinduzi ili kuponya maumivu na machungu ya mapinduzi.

Neno “Matukufu” kwenye Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar lisiendelee kutumika, yaitwe tu Mapinduzi ya Zanzibar na vibwagizo Mapinduzi Daima na Tutayalinda kwa gharama yoyote tuachane nayo ili kuponya wapinduliwa.

Falsafa hii ya 4R za Samia itumike hadi Zanzibar mshindi wa kweli wa uchaguzi wa Zanzibar atangazwe.

Hivyo, nawashauri Rais Samia, na Rais Mwinyi, kubalini kutibu makovu ya Mapinduzi ili kuzimaliza siasa za uadui, ikitokea upinzani umeshinda Zanzibar, hakuna haja kufunika kombe mwanaharamu apite, iwe ni kupokezana kwa amani na upendo.

Related Posts