Tanzania imepangwa katika kundi B la mashindano ya mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ndani (Chan) 2024 zitakazofanyika Agosti mwaka huu ambalo litaundwa na timu za Mauritania, Madagascar, Burkina Faso na Jamhuri ya Afrika ya Kati.
Katika droo ya fainali hizo iliyochezeshwa leo, Taifa Stars imejikuta ikiangukia katika kundi hilo ambalo timu zote zilizopo hakuna iliyowahi kufika hatua ya fainali ya mashindano hayo.
Madagascar ndio timu pekee iliyowahi kufanikiwa katika kundi hilo ambapo imewahi kumaliza katika nafasi ya tatu kweye fainali za Chan mwaka 2022.
Mafanikio makubwa ya Mauritania ni kufika robo fainali ya mashindano hayo mwaka 2022 huku Taifa Stars na Burkina Faso zenyewe zikitambia kuwahi kuishia hatua ya makundi tu.
Mnyonge wa kundi hilo ni Jamhuri ya Afrika ya Kati ambayo inashiriki fainali za Chan kwa mara ya kwanza.
Kundi la kifo ni A ambalo waandaaji wenza Kenya wapo kwani watakumbana na timu za Morocco, Angola, DR Congo na Zambia.
Mashindano hayo mwaka huu yatakuwa na makundi manne ambapo makundi matatu ya kwanza ambayo ni A, B, C yatakuwa na timu tano kila moja na kundi D litakuwa na timu nne.
Fainali za Chan 2024 zitakuwa za tatu kwa Taifa Stars kushiriki baada ya kufanya hivyo katika fainali za 2009 na 2020 ambazo zote iliishia hatua ya makundi.
Katika fainali za 2009, Tanzania ilishika nafasi ya tatu kwenye kundi lake baada ya kukusanya pointi nne katika mechi tatu ambapo ilianza kwa kufungwa bao 1-0 na Senegal kisha ikapata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Ivory Coast na mechi ya mwisho ikatoka sare ya bao 1-1 na Zambia.
Fainali za Chan 2020, Tanzania ilimaliza katika nafasi ya tatu tena ikikusanya pointi nne ambapo ilipoteza dhidi ya Zambia kwa mabao 2-0, kisha ikaifunga Namibia kwa bao 1-0 na mechi ya mwisho ikatoka sare ya mabao 2-2 na Guinea.