Uchaguzi Bawacha: Mstari wa ushindi Lissu, Mbowe

Dar es Salaam. Uchaguzi wa Baraza la Wanawake la Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Bawacha) unaofanyika kesho Alhamisi Januari 16, 2025 unatajwa kuchora ramani ya matokeo katika uchaguzi wa nafasi ya uenyekiti wa chama hicho taifa.

Mtazamo huo wa wanazuoni wa sayansi ya siasa, unatokana na kile wanachoeleza matokeo ya uchaguzi wa vijana (Bavicha) na wazee (Bazecha), yameweka mizania sawa na sasa yanasubiriwa ya Bawacha ili kuamua ushindi kati ya Freeman Mbowe au Tundu Lissu.

Mbowe na Lissu ni wagombea wa uenyekiti wa Chadema taifa, katika uchaguzi utakaofanyika Januari 21, 2025 kwenye ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam. Ushindani baina yao umesababisha kuwapo kambi mbili zinazounga mkono kila upande.

Kutokana na hilo, wasomi wa sayansi ya siasa wanatabiri huenda katika uchaguzi huo kukashuhudiwa mivutano, sintofahamu na pandashuka nyingi, zitakazochochewa na kambi mbili, kati ya inayomuunga mkono Mbowe na ile ya Lissu.

Mbowe anatetea nafasi hiyo aliyoiongoza kwa miaka 21 huku Makamu wake bara-Lissu akichuana naye.

Kwa mujibu wa wanazuoni hao, hekaheka za wanawake na hulka walizonazo ni jambo lingine litakaloongeza amshaamsha katika uchaguzi huo.

Uchaguzi huo, unafanyika wakati Deogratius Mahinyila akishinda uenyekiti wa Bavicha, huku Suzan Lyimo akishinda kwa upande wa Bazecha.

Mbowe amewapongeza viongozi wa Bazecha na Bavicha walioshinda katika chaguzi zilizofanyika Januari 13 na 14, jijini Dar es Salaam, huku akiwataka viongozi hao kuonyesha njia kwa wengine.

Mbowe amesema hayo leo Jumatano Januari 15, 2025 katika ujumbe aliouweka katika ukurasa wake wa X akisisitiza umoja kupitia kauli mbiu ya ‘We are Stronger Together  katika kufanikisha harakati za kutafuta Tanzania bora.

“Kwa viongozi wote wa Baraza la Wazee na Baraza la Vijana waliochaguliwa, hongereni kwa ushindi wenu! Bidii yenu katika harakati zetu imekuwa msingi wa mafanikio haya, inayowapa fursa ya kuwa viongozi wa kuonyesha njia kwa wengine katika kuongoza Baraza lenu,” ameandika.

Amewatia moyo wale ambao hawakushinda akisema juhudi zao zina thamani kubwa na watabaki kuwa nguzo muhimu ya chama hicho.

Kuhusu uchaguzi wa Bawacha, Mbowe amewatakia heri katika kukamilisha jukumu hilo.

“Kumbukeni, ‘We are Stronger Together’ katika kufanikisha harakati zetu za kutafuta Tanzania bora na sasa zaidi kuliko wakati wowote, tunahitajiana. Tuendelee kujenga chama chetu kwa umoja, upendo na moyo wa ujasiri ili pamoja tuweze kufikia ndoto zetu,” ameandika

Katika uchaguzi wa Bawacha utakaofanyika katika ukumbi wa Ubungo Plaza, Dar es Salaam wanaochuana nafasi ya uenyekiti ni aliyekuwa Spika wa Bunge la Wananchi la Chadema, Celestine Simba.

Wagombea wengine ni anayekaimu nafasi hiyo, Sharifa Suleiman na mbunge wa zamani wa Mlimba mkoani Morogoro, Susan Kiwanga.

Kwa upande wa Makamu Mwenyekiti (Bara), wagombea ni Agnes Chilulumo, Elizabeth Mwakimomo, Marietha Chenyenge, Moza Ally (Makamu Mwenyekiti mstaafu Bavicha -Bara), Naomi Ndigile, Rose Mkonyi na Salma Kasanzu.

Kwa upande wa nafasi hiyo Zanzibar, watakaochuana ni Bahati Haji na Zainabu Bakari, huku wanaogombea nafasi ya naibu katibu mkuu (Bara) ni Glory Tausi, Neema Mhanuzi na Nuru Ndosi.

Asiata Aboubakar ni mgombea pekee wa nafasi ya naibu katibu mkuu wa Bawacha Zanzibar.

Katika uchaguzi huo, Aisha Ame, Ashura Masoud, Husna Said, Sigrada Mligo na Yosepher Komba wanagombea nafasi ya uratibu na uenezi, huku Brenda Jonas na Joyce Mukya wakiutaka uhazini wa baraza hilo.

Wagombea wa ujumbe wa baraza kuu la Chadema kupitia Bawacha ni Amina Kanyama, Anna Ndiwu, Baega Masunga, Elizabeth Umila, Emiliana Kibatala, Hilda Newton, Hosiana Welwel na Irene Lema.

Wengine ni Jackline Nkunguu, Joyce Mwabamba, Julieth Tillya, Khadija Mwago, Lucia Bwire, Lucy Ngondo, Lucy Magoti, Lucy Kazembe, Mamuu Lolo, Neema Mohamed na Neema Chozaile.

Pia wamo Paulina Narsis, Tatu Mandoa, Tatu Isole, Valentina Rwegoshora na Zainab Ashraff.

Wagombea wa nafasi hiyo kutoka Zanzibar ni Iptisam Abdallah, Maryam Shamata na Mwadua Khamis.

Nafasi ya wajumbe wa mkutano mkuu wanaogombea ni Angela Lima, Asia Msangi, Dailina Gavuma, Dioniz Veneranda, Elda Mbegu, Elizabeth Mollel, Elizabeth Urasa, Esther Fulano, Fidea Komba, Grace Danda na Grace Ngola.

Wamo pia Helga Mchomvu, Imelda Mafuru, Judith Mrangu, Leticia Bwire, Lilian Kimei, Lydia Saliji, Margareth Akilimali, Magreth Lipindi, Maimuna Maluto, Mariam Amri, Nuru Nchimbi na Rehema Masondole.

Wengine ni Rosemary Chumi, Saada Idd, Salma Shariff, Scholastica Sida, Sophia Faraji, Suzana Mgonokulima, Theresia Mboya, Veneranda Martin, Winfrida Mwinula na Zainabu Mohamed.

Wagombea wa nafasi hiyo kutoka Zanzibar ni Ahlam Ali, Khadija Rashid, Khalima Masoud, Maimuna Fakih, Nuru Bakari na Raya Khamis.

Akizungumzia uchaguzi wa Bawacha, Mhadhiri mstaafu wa Sayansi ya Siasa, Profesa Ernest Mallya amesema uchaguzi wa Bawacha unakwenda kuchora mstari wa matokeo ya uchaguzi wa mwisho, Januari 21.

Profesa Mallya amesema uchaguzi wa Bawacha hautakuwa rahisi, kila kambi itafanya kila inaloliweza kujisafishia njia.

Katika mazingira hayo, amesema misukosuko na mivutano ya hapa na pale hushuhudiwa katika chaguzi, hivyo mambo hayo yatarajiwe kuonekana katika uchaguzi wa Bawacha.

“Uchaguzi wa Bawacha utakuwa na vita ya makambi, lakini kama vijana wamekwenda kwa Lissu na wazee kwa Mbowe na wapigakura ni haohao, isipokuwa wataongezeka wachache, ushindi unaweza kwenda upande wowote,” amesema.

Hata hivyo, ametoa angalizo kwa mgombea yeyote kati ya Lissu au Mbowe atakaposhinda ahakikishe anayaweka pamoja makundi katika mabaraza yote ili kuyaunganisha.

“Uchaguzi una ushindani mzuri lakini kazi ya washindi itakuwa ni kuhakikisha anawaunganisha wanachama kwanza kabla ya kutekeleza vipaumbele vyao,” amesema.

Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Frank Mateng’e amesema uchaguzi wa baraza hilo utarajiwe kuwa na taswira ya ushindani mkali kati ya wagombea wanaomuunga mkono Mbowe na Lissu.

Amesema Lissu na Mbowe kwa vyovyote vile ndio wenye nafasi ya kutoa mwelekeo wa chaguzi za vyombo vyote vya chini vya Chadema.

Kwa sababu ya mazingira hayo, amesema uchaguzi wa Bawacha ni kipimo sahihi cha upepo wa uchaguzi wa Januari 21 wa kumpata mwenyekiti wa chama hicho taifa.

“Uchaguzi wa Bawacha unawapa fursa wagombea wa uchaguzi wa Januari 21, kujipima na kuona jinsi wanavyoungwa mkono au wasivyoungwa mkono,” amesema.

Kwa mujibu wa Dk Mateng’e, iwapo uchaguzi wa Januari 21 utafanyika katika mazingira huru na haki, kitakachotokea Bawacha na kilichotokea Bavicha na Bazecha kitaakisi matokeo ya Lissu na Mbowe.

Hata hivyo, amesisitiza kwa sababu ya ushindani mkali wa wagombea wawili wa nafasi za juu, hali kama hiyo lazima ishuhudiwe pia kwenye uchaguzi wa Bawacha.

“Uchaguzi wa Bawacha hautakuwa lelemama, ndiyo uchaguzi utakaotoa taswira ya matokeo ya uchaguzi wa Januari 21 baada ya Bavicha na Bazecha kumaliza chaguzi zao. Huenda kukawa na ushindani mkubwa zaidi kwa Bawacha kwa sababu ni kipimo cha mwisho cha wagombea wa uenyekiti wa chama taifa,” amesema.

Hata hivyo, amesema ushindani unaoendelea unaweza kuleta athari kwa chama hicho, iwapo hakijakomaa katika kuhimili hali ngumu za kisiasa.

“Misukosuko kama hiyo wakati mwingine kuna hofu kwamba Chadema itasambaratika, lakini ikipita salama kwenye hii misukosuko wataonyesha kipimo cha ukomavu wa kuhimili nyakati ngumu,” amesema.

Related Posts