Ukosefu wa umeme kikwazo vifaatiba kufanya kazi Chato

Chato. Vifaatiba vyenye thamani ya Sh210 milioni vilivyopelekwa na Serikali katika Kituo cha Afya Nyabilezi, Kata ya Bukome wilayani Chato havitumiki kwa zaidi ya miezi sita.

Hali hiyo inatokana na ukosefu wa umeme unaotosheleza kuviwezesha kufanya kazi (umeme wa njia tatu).

Kituo hicho kilijengwa kwa gharama ya Sh1.4 bilioni, fedha za Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini (Tasaf) awamu ya tatu na kukamilika mwaka 2023.

Kinatoa huduma za afya kwa wakazi zaidi ya 12,000 wa Kata ya Bukome na zingine za jirani waliolazimika kutembea zaidi ya kilomita 18 kutafuta huduma Hospitali ya Wilaya ya Chato.

Akitoa taarifa ya utekelezaji wa mradi huo kwa wajumbe wa Kamati ya Uongozi ya Tasaf makao makuu waliofika kukagua miradi iliyotekelezwa kwa fedha za mfuko huo, Mganga Mfawidhi wa kituo hicho, Sylivester Bundalah amesema kukosekana umeme wa njia tatu kwenye kituo hicho kumesababisha vifaatiba vilivyopo vishindwe kufanya kazi.

Ametaja vifaa hivyo kuwa taa ya upasuaji yenye thamani ya Sh11 milioni, kitanda cha upasuaji (Sh6 milioni), mashine ya usingizi (Sh80 milioni), mashine ndogo ya kutakasia vifaa vya dharura (Sh3 milioni) na seti sita za kwa ajili ya upasuaji mkubwa zenye thamani ya Sh12 milioni.

Vifaa vingine ni seti sita kwa ajili ya upasuaji wa wajawazito zenye thamani ya Sh12 milioni, jokofu kwa ajili ya kutunzia damu salama (Sh80 milioni) na hadubini inayotumika kwa ajili ya vipimo vya maabara (Sh6 milioni).

Bundalah amesema kutokana na vifaa hivyo kutotumika inawalazimu wagonjwa kufuata huduma hospitali ya wilaya na ya Kanda Chato.

Ameomba wapelekewe umeme ili vifaa hivyo viweze kufanya kazi iliyokusudiwa.

Mjumbe wa kamati ya uongozi, Dk Ruth Lugwisha ameutaka uongozi wa halmashauri kwa kushirikiana na uongozi wa kituo kuona namna ya kufunga umeme mkubwa kwenye kituo hicho ili vifaa hivyo viweze kutumika.

“Vitu vya umeme visipotumika vinaharibika, hivi ni vitu vya gaharama halmashauri na uongozi wa hospitali kaeni chini muone njia ya kuleta umeme mkubwa hapa, mfano kuna wafanyabiashara, kuna watu wakubwa hapa kuna viwanda washirikisheni nina imani hawatakataa ili vifaa hivi viweze kutoa huduma,” amesema.

Mjumbe mwingine, Dk Naftali Ng’ondi ameitaka halmashauri kuangalia uwezekano wa kupata Sh20 milioni hata kutoka kwenye mapato ya ndani kwa ajili ya kufunga umeme mkubwa kwenye kituo hicho ili lengo la Serikali la kutoa vifaatiba kwa ajili ya wagonjwa liwe na tija.

Amesema Tasaf imejenga majengo na Serikali imeleta vifaa, hivyo ni vema uongozi wa halmashauri ukafanya jitihada za kufunga umeme mkubwa ili vifaa hivyo visiharibike na kusababisha hasara.

Mganga Mkuu wa Wilaya hiyo, Aristcles Raphael amesema awali hawakugundua kama umeme uliofungwa ulikuwa mdogo wa njia moja.

Amesema baada ya kugundua halmashauri imejipanga kutafuta bajeti ili kufunga umeme mkubwa utakaoweza vifaa hivyo kufanya kazi.

Katika hatua nyingine, wajumbe wa kamati ya uongozi ya Tasaf wameshauri walengwa wa mfuko huo waelimishwe watambue kuwa umasikini siyo sifa nzuri, hivyo wanapaswa kutumia kidogo wanachopokea kwa malengo ili baada ya muda watoke kwenye lindi la umasikini na kujitegemea.

“Tuwasaidie watambue umasikini siyo sifa, tuwabadilihse mtazamo wao wa akili ili fedha wanazopokea baada ya muda watoke kwenye mpango wengine pia waweze kuingia na kujikwamua kiuchumi, hakuna sifa ya kuitwa masikini. Kuna maeneo mengine hili neno ni aibu wanufaika wasione ni sifa,” amesema Dk Lugwisha.

Awali, Katibu Tawala wa Mkoa wa Geita, Mohamed Gombati akizungumza baada ya kupokea ugeni wa wajumbe hao ofisini kwake, amesema Tasaf inasaidia kusogeza huduma za kijamii karibu, hususani katika sekta ya elimu na afya hivyo kuwaondolea wananchi adha ya kutembea umbali mrefu kutafuta huduma.

Amesema ajira za muda wanazopewa walengwa wa mpango huo zimesaidia waweze kujikimu kimaisha.

Amesema kwa sasa wapo walengwa waliosaidiwa na Tasaf na kufanikiwa kujitegemea na wametoka kwenye mpango baaada ya hali zao kuimarika.

Mpango huo umewezesha watoto wa walengwa wanaosoma shule za msingi na sekondari kumudu kupata mahitaji ya shule na kuendelea na masomo. Pia, umesaidia kuongeza mahudhurio ya kliniki kwa watoto chini ya miaka mitano na wazazi kupata mafunzo na malezi ya watoto.

 “Walengwa wengi wamemudu kupata mahitaji ya msingi katika kaya na kuweza kumudu kupata milo miwili tofauti na awali hali zao zilivyokuwa kabla ya mpango. Baadhi ya walengwa wameanzisha biashara ndogondogo kwa ajili ya kupata kipato na kuimarisha uchumi wa kaya,” amesema.

Mpango wa Tasaf awamu ya tatu mkoani Geita umetumia zaidi ya Sh59 bilioni kutekeleza miradi ya maendeleo na za walengwa katika kipindi cha Julai 2020 hadi Januari 2025.

Related Posts