Ulevi watajwa mtendaji wa kijiji kuondolewa kituo cha kazi

Shinyanga. Mkuu wa Wilaya ya  Shinyanga Mjini, Julius Mtatiro ametoa agizo kwa Ofisa utumishi wa Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga, David Rwazo  kumuondoa kwenye eneo la kazi mtendaji wa Kijiji cha Igaganulwa kilichopo Kata ya Usanda, Sebastian Ntungu kwa kosa la kulewa wakati wa kazi kinyume na taratibu za utumishi wa umma.

Agizo hilo amelitoa leo Jumatano, Januari 15, 2025 katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika kijiji hicho baada ya kuanza kusikiliza kero za wananchi na akabaini mtendaji huyu hulewa wakati wa kazi hata muda wa kikao alikuwa amelewa.

“Huyu mtendaji naambiwa kijijini hapa yupo mwaka wa nane sasa, ninasikitika mtendaji wa kata kushindwa kuchukuliwa hatua siku zote kumbe amekuwa mlevi na huduma ya kuwatumikia wananchi inakwama, na hata hapa unavyoongea inaonesha kabisa umelewa, ofisa utumishi mtumishi mtu huyu sitaki kumuona katika kijiji hiki kama mtumishi tafuteni mahali pa kumpeleka,” amesema Mtatiro.

Kwa upande wake, mtendaji wa kijiji hicho Sebastian Tungu amekiri kulewa, lakini amesema huwa analewa baada ya kazi na amekanusha tuhuma za kulewa wakati wa kazi.

“Huwa nakunywa lakini ni baada ya kazi, sijwahi kulewa wakati wa kazi,” amesema Tungu.

Aidha, Kaimu Mtendaji wa Kata ya Usanda, Josiah Dyunyeto amedai kuwa mara nyingi wamemuonya hata kupitia kwenye vikao kuhusu tabia hiyo na mara ya mwisho alionywa mwaka jana mwishoni.

“Mtumishi huyu amekuwa akilewa sana na tulichukua hatua ya kukaa naye na kumuonya, tumekuwa tukimuonya hata kwenye vikao vya utendaji, lakini maonyo yetu hayakufanya kazi na mara ya mwisho kukaa naye na kumuonya ilikuwa Desemba 24, 2024,” amesema Dyunyeto.

Ofisa Utumishi wa Halmashauri hiyo, Davidi Rwazo amesema hana taarifa yoyote juu ya mtendaji huyo kuwa hulewa wakati wa kazi, hivyo hatua itachukuliwa ya kumuondoa eneo hilo na kuleta mtumishi mwingine.

“Sina taarifa yoyote kuhusiana na mtumishi huyu kwenda kinyume na taratibu kwa kulewa wakati wa kazi, lakini kutokana na kinachoendelea, hapa tutamuondoa katika kijiji hiki na kuleta mtumishi atakayeweza kuwatumikia wananchi” amesema Rwazo.

Mkazi wa kijiji hicho, James Sanengo ameeleza sababu ya kukwama kwa mambo mengi kijijini hapo ni kutokana na kukosa mtendaji mzuri kwa sababu kila mara wakimfuata ofisini anakuwa amelewa pombe.

“Wakati wa uchaguzi wa serikali za mitaa alikabidhiwa muhuri na mwenyekiti pia kila ukiwa na uhitaji wa muhuri unakuta amelewa,” amedai Sanengo.

Mwenyekiti wa serikali ya kijiji hicho, Abeli Nkarangi amesema amekabidhiwa muhuri na ofisa mtendaji huyo bila kufuata utaratibu, hata ofisi na nyaraka hajakabidhiwa.

“Tangu nimechaguliwa sijakabidhiwa ofisi na mtendaji huyu, nilikabidhiwa muhuri pekee bila nyaraka zozote kwa ufupi sijakabidhiwa ofisi na mtendaji,” amesema Nkarangi.

Related Posts