Nairobi. Hali ya mambo nchini Kenya inaonekana kuendelea kuwa tata, baada ya Waziri wa Utumishi wa Umma, Justin Muturi kufichua hadharani jinsi mwanawe, Leslie Muturi alivyotekwa na namna Rais William Ruto alivyosaidia na kuhakikisha anachiliwa huru.
Kwa mujibu wa Muturi, licha ya kujaribu kuwasiliana na viongozi wa vyombo vya usalama bila mafanikio, alilazimika kumuomba Rais Ruto kuingilia kati na mtoto huyo akaachiwa.
Kauli ya waziri huyo imetolewa siku 17 tu baada ya Rais William Ruto kutoa ahadi kwa taifa la Kenya kwamba serikali yake itahakikisha matukio ya utekaji yanakomeshwa nchini humo. Rais Ruto pia aliwataka wazazi kuwajibika katika malezi ya watoto wao ili kuwasaidia kuwa raia wema na wenye nidhamu.
Rais Ruto alitoa ahadi hiyo Desemba 28, 2024, wakati wa fainali za mashindano ya Cup 2024 zilizofanyika katika uwanja wa Raila Odinga. Alisisitiza kuwa vijana wa Kenya wataishi kwa amani matukio ya utekaji yakidhibitiwa.
“Kuhusu masuala ya utekaji, tutahakikisha tunakomesha ili vijana wa Kenya waweze kuishi kwa amani na pia wawe na nidhamu ili tuijenge Kenya kwa pamoja,” alisema Rais Ruto, akinukuliwa na gazeti la Nation.
Hata hivyo, Waziri mteule wa Habari na Mawasiliano (ICT), William Kabogo, leo Jumatano, Januari 15, 2025, anasema matamshi ya Waziri Muturi ni ishara ya kukosa uwajibikaji, akisisitiza kuwa alipaswa kufuata taratibu sahihi badala ya kutoa madai yake hadharani.
Kabogo anasema hayo alipokuwa akifanyiwa mahojiano ya uteuzi kuthibitisha uwezo wake wa kushikilia wadhifa huo.
Anafafanua, iwapo Muturi hakuridhika na jambo lolote, alipaswa kulifikisha kwa rais au baraza la mawaziri na ikiwa majibu ya mamlaka hizo hayangemridhisha, hatua ya heshima ingekuwa ni kujiuzulu.
“Ningekuwa mimi kwenye nafasi yake, ningewasilisha malalamiko yangu kwa mamlaka ya uteuzi. Kama ningekuwa na hofu ya kumkabili Rais, ningelifikisha suala hilo baraza la mawaziri. Na kama bado nisingeridhika, ningechukua uamuzi wa kujiuzulu,” anasema Kabogo.
Anasisitiza kuwa hatua ya Muturi ni ya kukosa uwajibikaji na kuongeza; “Mimi ni kiongozi kabla ya kuwa mwanasiasa. Kwa mtazamo wangu, alichokifanya Muturi ni kukiuka maadili ya uwajibikaji.”
Muturi alitoa madai hayo kupitia maandishi Januari 14, 2025, aliandika kuwa Rais William Ruto alimwagiza Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa (NIS), Noordin Haji kumwachilia huru mwanawe, ambaye alidai alikuwa anashikiliwa na maofisa wa usalama.
Kwa mujibu wa Muturi, mawasiliano hayo yalifanyika moja kwa moja kati ya Rais na bosi wa NIS, ambaye awali alikana kumshikilia mwanawe lakini hatimaye alikiri kwa Rais na kutekeleza maagizo ya kumuachilia.
Madai hayo yametokea katika kipindi ambapo Kenya inakumbwa na msururu wa matukio ya utekaji nyara na watu kupotea, hali ambayo imezua mjadala mkali nchini humo.
Aidha, madai hayo yamejiri siku chache baada ya mwanahabari na mwanaharakati wa Tanzania, Maria Sarungi, kudai kutekwa nyara nchini humo.
Tukio la Sarungi, Besigye linavyokoleza moto
Sarungi anadaiwa kutekwa Januari 12, 2025 kati ya saa 9:00 na 9:30 mchana katika eneo la Chaka Jijini Nairobi na watu wanne waliokuwa na silaha ambao walimpeleka kusikojulikana huku wakimtesa, kabla ya kumwachia huru baada ya saa nne.
Tukio hilo lilikuwa ni kama linakoleza moto kwa kuumwagia petroli kwa sababu liliibua mjadala mkubwa kwenye vyombo vya habari vya ndani na nje ya Kenya huku mashirika likiwamo Amnesty International likitoa wito wa kuachiliwa huru kwa wahusika.
Tume ya Haki za Binadamu nchini Kenya ilibainisha kuwa takriban Wakenya 82 walitekwa nyara kati ya Juni 2024 na Januari 12, 2025.
Hadi sasa, Wakenya 20 bado hawajulikani walipo, huku watano wakiachiwa huru wiki iliyopita. Kulingana na tume hiyo, wengi wa waliotekwa walikuwa wakosoaji wa Serikali.
Suala la utekaji nyara nchini Kenya limevutia hisia za kimataifa baada ya mwanasiasa mashuhuri wa Uganda, Dk Kizza Besigye kutekwa nyara na watu wenye silaha jijini Nairobi, Novemba 16, 2024 na kurejeshwa kwa nguvu Uganda.
Simulizi ya waziri Muturi
Katika andiko lake lililosambaa katika mitandao ya kijamii ambalo amethibitisha ndiye ameliandika alipohojiwa na Nation, waziri Muturi ameeleza namna mwanawe alivyotekwa nyara na vyombo vya usalama na namna alivyoshughulikia suala hilo.
Waziri huyo amesimulia Juni 22,2024 saa 3:29 usiku akiwa na kikao na marafiki zake, alipokea simu kutoka kwa mkewe akimjulisha kuwa amepigiwa simu kuwa mtoto wao wa kiume, Leslie Muturi alikuwa ametekwa Jijini Nairobi.
Kulingana na taarifa hizo, mwanawe alikuwa ametekwa katika Mtaa wa Olenguruone na watu wenye silaha zikiwamo bunduki za kivita aina ya AK-47 waliokuwa wakitumia magari mawili, Toyota Prado na Toyota Probox.
“Nilijaribu kumpigia Leslie simu lakini simu yake ilikuwa haipatikani. Baada ya kujadiliana na marafiki zangu niliamua kumpigia simu IGP (inspekta Jenerali), Japhet Koome ambaye aliahidi atasambaza taarifa hiyo vituo vyote vya polisi”
“Baada ya muda kidogo, Mark Mwanje aliyekuwa eneo la tukio alinipigia simu na kunielezea lilivyokuwa kwamba watekaji walikuwa na Prado nyeupe na watu hao walikuwa na bunduki AK-47 na kumwingiza kwa nguvu kwenye gari hiyo,”
Baada ya maelezo hayo, waziri huyo alijaribu kumpigia simu DCI, Mohamed Amin lakini simu yake ilikuwa haijibiwi, na hapo akajaribu kumpigia mkurugenzi mkuu wa NIS, Noordin Haji lakini naye alikuwa hapokei simu yake kabisa.
“Baada ya saa moja, nilimpigia tena IGP, ambaye aliniambia tayari ametoa taarifa kwa barabara zote, lakini akasema tukio hilo linaonekana kama ni la uporaji. Hata hivyo, nilimweleza kwamba, kwa mujibu wa taarifa ya Mwanje, watekaji wanaonekana kama maofisa wa usalama.”
“Ilionekana kama maelezo yangu hayakumshawishi, kwani aliniambia kwamba usiku huo hakukuwa na operesheni yoyote ya polisi. Nilimpigia simu tena, lakini akasema kuwa ameongea na taasisi nyingine na bado linaonekana ni tukio la wizi wa gari.”
“Baadaye niligundua kwamba polisi wa Kilimani walikuwa wameenda Citizen TV kuomba kurekodi kamera za CCTV, lakini walikataliwa. Hata hivyo, baada ya kuzungumza na mkurugenzi, walifanikiwa kupata rekodi hizo, ambazo zilionyesha jinsi utekaji ulivyofanyika kwa kutumia magari mawili.”
Alivyowasiliana na Rais Ruto
Kwa mujibu wa Waziri Muturi, alfajiri ya saa 9:00 siku iliyofuata, akiwa na taharuki bado, aliamua kumtumia Rais Ruto ujumbe WhatsApp akimjulisha juu ya tukio la mtoto wake kutekwa na watu waliokuwa na silaha aina ya AK-47.
“Ni wakati huohuo kuna mtu alinipa namba ya mkurugenzi wa kitengo cha kupambana na ugaidi (ATPU), Said Mohamed kwa vile tulishatambua yale magari na idara hiyo nayo imekuwa ikitumia magari ya aina hiyo mara kwa mara”
“Simu iliita bila kupokelewa wala kujibiwa kwa SMS niliyokuwa nimemtumia”, alisema na kwa kuwa alikuwa hampati, aliamua kumtafuta naibu wake, James Onyango akasema atafuatilia kwa kuwa kulikuwa na operesheni.”
Aliendelea kueleza katika andiko hilo kuwa, akiwa nyumbani saa 2:15 asubuhi, Onyango alimpigia simu kumueleza kuwa ameangalia kila mahali hakuna tukio kama hilo lililoripotiwa.
Hata hivyo alisema punde Mohamed alimpigia simu akimjulisha kuwa ATPU haihusiki na operesheni hiyo.
Alieleza saa 4:00 asubuhi alipigiwa simu na rafiki yake kutoka NIS akimweleza kuwa mwanawe anashikiliwa na watu wa NIS. Alisema alimpigia simu tena tena Noordin Haji lakini hakupokea.
“Kabla ya saa 7:00 mchana, nilimpigia Waziri wa Mambo ya Ndani, Profesa Kindiki. Baada ya kumweleza tukio lote, aliniambia anahitaji kuzungumza na Noordin. Dakika 15 baadaye alinirudia na kusema Noordin amekana kumshikilia Leslie,” alisimulia katika andiko hilo.
Hata hivyo alisema aliangalia simu yake kuona kama Rais amesoma ujumbe wake, lakini alikuwa bado na muda mfupi helikopta za Rais zikielekea Ikulu akitokea kanisani, akaamua kwenda moja kwa moja Ikulu.
Kwa mujibu wa waziri huyo, alipofika alimkuta Rais akizungumza na kundi la wabunge anaowafahamu akasubiri wamalize akapata fursa ya kumjulisha tukio zima.
“Nikiwa nimesimama pembeni, nilimsikia Rais akimuuliza Noordin Haji kama wao ndio wanamshikilia mtoto wangu. Noordin alimjibu ni kweli. Hapo Rais akaagiza aachiliwe mara moja na Noordin akasema baada ya saa moja watamwachia,” alieleza.
Lakini kauli hiyo ya wazi ya waziri imeibua mijadala mikali nchini Kenya, hususan kupitia mitandao ya kijamii na televisheni. Januari 14, 2025, kulikuwa na malumbano makali kati ya Naibu Spika, Gladys Shollei na Seneta wa Kisii, Richard Onyoka katika kipindi kilichorushwa na televisheni ya Citizen.
Naibu Spika alikataa kuwepo matukio ya utekaji kwa kuegemea uvumi, akisisitiza kuwa ni lazima watu waliotekwa na kuachiwa watoe ushuhuda wazi.
“Huwezi kuniambia kuna utekaji, huo ni mtazamo wako. Mimi ningependa kuona maelezo ya hao watu sita walioachiwa wakisema walikuwa wapi, nani aliwachukua, na ni gari gani lilihusika. Hapo ndipo nitatoa maoni yangu,” alisema Shollei.
Seneta Onyoka alisema; “Nimeshtushwa na kauli ya Naibu Spika. Yaani ni kama ametoka Ulaya leo. Hizi kauli zinazopuuza suala la utekaji si za haki,” alisema Onyoka.
Onyoka aliendelea: “Waziri wa serikali amejitokeza hadharani kueleza namna mtoto wake alivyochukuliwa. Hapa kuna watu sita waliopatikana na nchi yetu inaamini katika utawala wa sheria. Tunapinga matendo haya kwa kuwa yanakiuka sheria na Katiba.”
“Kuna ushahidi wa kutosha kupitia CCTV na magari ya serikali yanayohusika katika matukio haya yanajulikana. Watu wanatekwa, wanauawa, na miili yao inapatikana mortuary (vyumba vya kuhifadhia maiti). Je, tunawezaje kuwa na genge nchini Kenya linalotekeleza utekaji na mauaji kwa sababu ya ukosoaji wa serikali?” alihoji Onyoka.