Dar es Salaam. Viongozi wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Tanzania (JWT), imeridhika na uwekezaji uliofanyika katika Bandari ya Dar es Salaam, ikisema umeleta ufanisi katika uendeshaji wa bandari hiyo katika uboreshaji wa utoaji wa huduma.
Kwa nyakati tofauti Serikali iliingia mikataba na Kampuni za DP World na Kampuni ya Adani Ports ili kuboresha na kuleta ufanisi huduma za bandari hatua itakayowezesha bandari ya Dar es Salaam kuwa na ushindani.
Wakati ziara ya viongozi wa JWTwaliotembelea Bandari ya Dar es Salaam kuangalia namna inavyotekeleza majukumu yake, Mwenyekiti wao, Hamis Livembe alieleza kuwa ufanisi wa bandari ulikuwa moja ya malalamiko yao makubwa.
“Kama mtakumbuka mwaka juzi tulipata changamoto pale Kariakoo akaja Waziri Mkuu (Kassim Majaliwa), katika moja ya mambo aliyoelezwa ni malalamiko ya ucheleweshaji wa utoaji wa mizigo bandarini na ucheleweshaji wa meli kuingia bandarini,” amesema.
Anasema ucheleweshaji wa meli ulisababisha bei ya makontena kupanda, kuna kipindi mwaka 2024, bei ya kontena moja ilifika hadi dola za Marekani 8,000 (Sh20.1 milioni) kutoka 3,000 (Sh7.5 milioni) kutoka na ucheleweshaji wa upakuaji wa mizigo bandarini.
Livembe amefafanua wakati huo, meli ilikuwa inakaa nje kwa siku 30 hadi 40 kabla ya kutia nanga na kuanza kupakua mizigo katika Bandari ya Dar es Salaam. Anasema ikifika bandarini meli hiyo inashusha mzigo kwa siku 10 hadi 15.
“Hapa katikati tumeanza kupata taarifa kutoka kwa wafanyabiashara wanaopitisha mizigo bandarini hapa kwamba hali imebadilika, baada ya kuja kwa DP World na Adani mizigo inashuka kwa haraka, lakini ukaaji wa meli nje umebadilika, ikizidi sana inakaa siku moja kabla ya kuingia bandarini,” anasema.
Ameongeza: “Pamoja na kusikia maelezo haya mazuri tukasema tuje kutembelea kuona hayo mabadiliko ili tuwe mashuhuda. Tumetembelea tumeona kwamba kuna mabadiliko makubwa na uwekezaji bado unaendelea,” amesema.
Livembe anasema wametaarifiwa na uongozi wa bandari ya Dar es Salaam, kwamba meli iliyokuwa ikishusha mzigo kwa siku 10 hivi sasa inashusha kwa siku mbili au moja kisha inaondoka bandarini hapo.
“Haya ni mafanikio makubwa, tunaipongeza TPA (Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania) na Serikali kwa jitihada hizi za kuondoa ucheleweshaji wa utoaji wa mizigo bandarini,” amesema Livembe.
Livembe ameitaka TPA kujipanga zaidi katika kuongeza ufanisi zaidi katika bandari hiyo ili kuvutia wafanyabiashara wa mataifa mengine kupitisha mizigo na kukuza uchumi wa Taifa.
Kaimu Mkurugenzi wa Bandari ya Dar es Salaam, Abed Gallus anasema mafanikio hayo yametokana na uwekezaji uliofanyika katika bandari hiyo.
“Mwaka 2023 Serikali ilishirikisha wawekezaji wawili DP World na Adani Ports wanaofanya kazi kwenye bandari ya Dar es Salaam. Ujio wao umepunguza muda wa meli kusubiria nje, sasa meli za makontena zinakuja moja kwa moja hazisubiri tena.”
Meneja Uhusiano wa Kampuni ya DP World Tanzania, Elitunu Mallamia anasema katika utekelezaji wa majukumu yao wamevuka malengo ya kuhudumia magari, makasha na mizigo mingine.
“Tumejitahidi kuongeza ufanisi, kwa mwezi wa Desemba mwaka 2024 tumevunja rekodi kwa kuhudumia magari zaidi ya 25,000 pamoja na meli 16 za magari ndani ya mwezi mmoja, hiki ni kiwango kikubwa tunajivunia,” anasema Mallamia.