WHO yatahadharisha uwepo wa Marburg Kagera, wanane wakitajwa kufariki

Dar es Salaam. Shirika la Afya Duniani (WHO) limesema watu wanane wamefariki dunia kutokana na ugonjwa unaoshukiwa kuwa wa virusi vya Marburg (MVD) mkoani Kagera.

Taarifa iliyochapishwa mtandaoni na WHO Januari 13, 2025 imewajulisha nchi wanachama wake na vyombo vya kusimamia Kanuni za Afya za Kimataifa (IHR) kuhusu mlipuko wa ugonjwa unaoshukiwa kuwa Marburg katika wilaya mbili za mkoa huo uliopo Kaskazini mwa Tanzania.

Jitihada za kuwafikia maofisa wa Wizara ya Afya hazijafanikiwa, lakini chanzo cha kuaminika kilithibitisha kuwa wizara inafahamu kuhusu tahadhari ya WHO na inachunguza mlipuko huo.

“Taarifa rasmi itatolewa mara uchunguzi utakapokamilika,” kilisema chanzo hicho ambacho kiliomba kutotajwa jina.

Iwapo itathibitika kwamba kuna mlipuko wa ugonjwa huo nchini, itakuwa mara pili, ya kwanza ilikuwa Machi 16, 2023 Serikali kupitia Wizara ya Afya ilipotangaza uwepo wa ugonjwa usiojulikana katika Halmashauri ya Bukoba Vijijini, Kata ya Maruku na Kanyangereko, vijiji vya Bulinda na Butayaibega ambao uliwapata watu tisa na vifo sita, kabla ya kugundulika kuwa ni Marburg.

WHO katika taarifa imeeleza inatoa tahadhari kuhusu hatari ya afya inayoweza kuwa na athari za kimataifa.

“Januari 10, 2025 WHO ilipokea ripoti za kuaminika kutoka kwa vyanzo vya ndani ya nchi kuhusu wagonjwa wanaoshukiwa kuwa wa Marburg katika Mkoa wa Kagera, nchini Tanzania.

“Watu sita waliripotiwa kuathirika, watano kati yao walifariki dunia. Wagonjwa hao walionyesha dalili zinazofanana kama vile maumivu ya kichwa, homa kali, maumivu ya mgongo, kuhara, kutapika damu, hali ya udhaifu mwilini na katika hatua ya baadaye ya ugonjwa, kutokwa na damu kwenye matundu ya mwili,” imeeleza taarifa ya WHO.

Shirika hilo limesema hadi kufikia Januari 11, wagonjwa tisa walikuwa wameripotiwa na vifo vikiwa vinane katika wilaya za Biharamulo na Muleba.

WHO imesema sampuli kutoka kwa wagonjwa wawili zilikusanywa na kupimwa katika maabara ya kitaifa ya afya ya umma.

“Matokeo bado yanangoja uthibitisho rasmi. Watu waliokuwa karibu na wagonjwa, wakiwemo wahudumu wa afya, wamebainishwa na wanafuatiliwa katika wilaya zote mbili,” limesema shirika hilo.

Kwa mujibu wa WHO, Wilaya ya Bukoba ilikumbwa na mlipuko wa kwanza wa Marburg Machi, 2023 na hifadhi ya wanyama wa asili, kama popo wanaokula matunda, bado ipo katika eneo hilo. Mlipuko wa Machi 2023 uliendelea kwa karibu miezi miwili na kuhusisha na wagonjwa tisa, vikiwemo vifo sita.

Tangu kutokea kwa mlipuko huo, timu za dharura za kitaifa zimepelekwa kusaidia uchunguzi na majibu ya mlipuko, shughuli za ufuatiliaji zimeimarishwa na ufuatiliaji wa watu waliokuwa karibu na wagonjwa unaendelea.

Sampuli za maabara kutoka kwa wagonjwa wa hivi karibuni zimetumwa kwa uthibitisho katika maabara ya kitaifa ya afya ya umma, huku vituo vya matibabu vimeripotiwa kuanzishwa.

Katika tathmini ambayo WHO imefanya, wahudumu wa afya ni miongoni mwa waathirika wa ugonjwa huo, jambo linaloonyesha hatari ya maambukizi zaidi katika vituo vya afya husika, huku chanzo cha mlipuko kikiwa bado hakijajulikana.

Hata hivyo, WHO imesema ripoti inaonyesha uwezekano wa kuenea kijiografia, ugunduzi na kutengwa kwa wagonjwa kulikochelewa, pamoja na ufuatiliaji wa watu waliokuwa karibu, unaonyesha ukosefu wa taarifa kamili kuhusu mlipuko wa sasa na wagonjwa zaidi wanatarajiwa kutambuliwa.

Mkoa wa Kagera, ingawa hauko karibu na mji mkuu wa Tanzania au viwanja vikubwa vya ndege vya kimataifa, umeunganishwa vyema kupitia mtandao wa usafiri na una uwanja wa ndege unaounganisha na Dar es Salaam kwa safari za nje ya Tanzania kwa ndege.

Kwa mujibu wa WHO, virusi vya Marburg ambavyo ni sawa na virusi hatari vya Ebola, viligunduliwa kwa mara ya kwanza baada ya watu 29 kuambukizwa na saba kati yao kufariki dunia mwaka 1967, huko Marburg, Ujerumani.

Hata hivyo, WHO ilisema virusi vya Marburg vilipatikana kwa mara ya kwanza kwa tumbili.

Mlipuko huo ulitokana na tumbili kutoka barani Afrika walioagizwa kutoka Uganda, lakini virusi hivyo vimehusishwa na wanyama wengine tangu wakati huo.

Taarifa ya WHO inaeleza ugonjwa huo pia unaweza kuenezwa na binadamu ambaye amekaa kwa muda mrefu katika mapango na migodi iliyo na popo.

Ugonjwa huo unatajwa kuwa huanza ghafla kwa homa, misuli kuuma na baada ya siku tatu hufuatwa na kuharisha, kuumwa tumbo, kichefuchefu na kutapika. Kisha mgonjwa huanza kutokwa damu kwenye matundu mbalimbali mwilini.

Ugonjwa huo huambukizwa kutoka kwa binadamu mmoja kwenda kwa mwingine hususan kwa njia ya kugusa majimaji mfano mate, mkojo, damu, machozi au kinyesi kutoka kwa maiti au mgonjwa mwenye dalili.

Maambukizi yanaweza kutokea pia kutoka kwa wanyama kwenda kwa binadamu iwapo mtu atakula, kugusa mizoga au wanyama waliambukizwa.

Dalili za ugonjwa huo ni homa, kuumwa kichwa, maumivu ya misuli, kuishiwa nguvu, kutapika na kuharisha, kutoka damu sehemu za wazi za mwili na nyingine zifananazo na hizo. Ni ugonjwa usio na tiba bali hutibiwa kwa dalili za awali.

Jinsi ya kudhibiti ugonjwa huo watu wanapaswa kuepuka kula au kushika nyama ya porini.

Hata hivyo, WHO imesema watu wanapaswa kuepuka kuwa karibu na nguruwe katika maeneo yenye mlipuko.

Kwa mujibu wa WHO, nchi kadhaa za Afrika zimewahi kuripoti mlipiko wa virusi vya ugonjwa huo zikiwamo Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Kenya, Afrika Kusini, Uganda na Zimbabwe. Mlipuko wa mwaka 2005 nchini Angola ulisababisha vifo vya watu zaidi ya 300.

Barani Ulaya ni mtu mmoja tu amefariki katika kipindi cha miaka 40 na mmoja nchini Marekani baada ya kurejea kutoka safari ya kuzuru mapango nchini Uganda.

Mwaka 2017 nchini Uganda wagonjwa watatu waliugua na wote walifariki dunia.

Mwaka 2012 nchini Uganda watu 15 waliugua na kati yao wanne walifariki dunia.

Mwaka 2005 nchini Angola kuliripotiwa wagonjwa 374 na 329 walifariki dunia.

Kati ya mwaka 1998 hadi 2000, DR Congo waliripotiwa wagonjwa 154 na watu 128 walifariki dunia.

Mwaka 1967 nchini Ujerumani waliripotiwa wagonjwa 29 na saba walikufa.

Related Posts