YANGA ikitinga hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu, itaua ndege wawili kwa jiwe moja.
Jambo hilo linasubiriwa kwa hamu kubwa sana na mashabiki wa timu hiyo ili kuwaziba mdomo watani zao wa jadi, Simba ambao kwa kipindi kirefu wamekuwa wakitamba kwenye mashindano ya Caf.
Wikiendi hii, Yanga ina mechi ya lazima kushinda dhidi ya MC Alger itakayochezwa Uwanja wa Benjamin Mkapa, ili kufuzu robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Yanga yenye pointi saba katika nafasi ya tatu Kundi A, inahitaji ushindi ili kuipiku MC Alger inayoshika nafasi ya pili na pointi nane. Kumbuka MC Alger inahitaji sare tu kufuzu.
Sasa basi, Yanga ikifuzu, kwanza itajiandikia historia yake ya kutinga hatua ya robo fainali ya michuano hiyo mara mbili mfululizo kwani hapo awali haikuwahi kufanya kitu kama hicho.
Pili, itaishusha Simba na kusogea hadi nafasi ya sita katika chati ya ubora wa klabu Afrika kwa muda wa miaka mitano inayotolewa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (Caf).
Kwa sasa Yanga inashika nafasi ya 10 kwa ubora klabu Afrika, ikitinga robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika itapanda hadi nafasi ya sita na kuishusha Simba inayoshika nafasi hiyo kwa sasa.
Ipo hivi; Yanga ikitinga robo fainali, itapata pointi tatu zitakazozidishwa kwa tano na kisha kujumlishwa na pointi 24 ilizozivuna katika misimu minne iliyopita kutegemea na mafanikio iliyoyapata katika mashindano ya kimataifa. Jumla itakuwa nazo 39.
Simba ambayo imeshatinga robo fainali, imejihakikishia pointi 38 kwa vile pointi za hatua ya robo fainali Kombe la Shirikisho Afrika ni mbili, hivyo zikizidishwa kwa tano, Simba inakuwa na pointi 10 kwa msimu huu.
Pointi hizo 10 zinajumlishwa na pointi nyingine 18 ambazo Simba imevuna katika ushiriki wake kwenye mashindano ya klabu Afrika msimu minne iliyopita.
Ikiwa Yanga itasonga mbele zaidi kwenye michuano hiyo, itazidi kuiacha Simba kwenye mataa kwani itapata pointi nyingi zaidi kadri itakavyokuwa inasogea raundi za juu.
Hata hivyo, Simba inaweza kuendelea kuwa juu iwapo Yanga itashindwa kupenya robo fainali au Simba ikivuka hatua za mbele zaidi kulinganisha na watani wao.
Chati ya Caf ya ubora wa klabu hupangwa kwa kuzingatia pointi ambazo klabu imekusanya katika ushiriki wake kwenye mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho Afrika kwa kipindi cha misimu mitano ya nyuma.
Timu huanza kuhesabiwa pointi hizo kuanzia hatua ya makundi hadi ile ya fainali na zinazotolewa katika raundi ya kwanza na ya pili hazipati pointi yoyote.
Kwa mujibu wa muongozo wa sasa, ushiriki wa kuanzia hatua ya makundi hadi fainali Ligi ya Mabingwa Afrika unakuwa na idadi kubwa ya pointi tofauti na Kombe la Shirikisho Afrika.
Katika Ligi ya Mabingwa, bingwa anapata pointi sita (6), mshindi wa pili pointi tano (5), timu mbili zinazoishia nusu fainali kila moja inapata pointi nne, pointi tatu ni kwa timu inayotolewa katika robo fainali, timu inayoshika nafasi ya tatu kwenye kundi inapata pointi mbili na pointi moja hupata timu ambayo inashika mkia kwenye kundi.
Kwenye Kombe la Shirikisho Afrika, timu inayoshika mkia kwenye kundi inapata pointi 0.5, nafasi ya tatu inapata pointi moja, pointi mbili ni kwa inayotolewa robo fainali, timu mbili zinazoishia nusu fainali kila moja inapata pointi tatu, mshindi wa pili anapata pointi nne na bingwa pointi tano.
Kisha pointi hizo zinazidishwa kwa alama ya msimu mmommoja katika mitano iliyopita ambao msimu wa tano nyuma unakuwa ni alama moja, msimu wa nne unakuwa ni alama mbili, msimu wa tatu unakuwa ni alama tatu, msimu wa pili nyuma unakuwa ni alama nne na msimu mmoja nyuma unakuwa ni alama tano.