Yanga yapewa mwamuzi wa sare

NYOTA wa Yanga wanatakiwa kuongeza umakini wakati wakipambania ushindi, Jumamosi katika mchezo wao wa mwisho wa hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya MC Alger kutokana na rekodi ya ajabu ya mwamuzi, Patrice Milazare kutoka Mauritius ambaye anatarajiwa kuamua mchezo huo.

Katika michezo mitatu aliyoamua msimu huu, rekodi ya Milazare ni ya kutisha, hakuna timu yoyote iliyofunga bao, hivyo kocha wa Yanga, Sead Ramovic na vijana wake wanatakiwa kufanya kazi ya ziada kuhakikisha wanabadilisha rekodi hiyo kwani uhitaji wao wa kushinda ni mkubwa kulinganisha na wapinzani wao MC Alger hata sare inawabeba.

Kama hiyo haitoshi, Milazare pia ni mtaalamu wa kutoa kadi. Hadi sasa, ameonyesha ni mwepesi wa kutoa kadi, akitoa 15 katika michezo mitatu ya msimu huu wa mashindano ya 2024/25.

Kadi hizi za njano, ambazo anazitoa kama njugu, zinaonyesha ni mwamuzi mwenye mkono mrefu wa kutoa adhabu na hili linaweza kuwa changamoto kubwa kwa Yanga, ambayo itahitaji umakini wa ziada ili kuepuka adhabu kutoka kwa mwamuzi huyu mkali.

Katika michezo aliyochezesha msimu huu, Milazare aliongoza mechi mbili muhimu za kuwania kufuzu kwa fainali za Mataifa ya Afrika, huku akiwadhibiti wachezaji kwa kiwango cha juu.

Mchezo wa kwanza ulifanyika Oktoba 10, 2024, Ghana walikuwa wenyeji wa Sudan kwenye Uwanja wa Michezo wa Accra. Katika mchezo huo, Milazare alitoa kadi tatu za njano, na matokeo yalikuwa 0-0.

Mwezi mmoja baadaye, Novemba 18, 2024, Milazare alichezesha mechi nyingine ya kuwania kufuzu fainali za Afcon, hii ikiwa ni ya kundi D kati ya Libya na Benin kwenye Uwanja wa Kimataifa wa Michezo wa Tripoli. Aliendelea na mtindo wake wa kutoa kadi nyingi na alitoa kadi tisa za njano na matokeo yalikuwa 0-0.

Hii ni dalili Milazare ni mfalme wa michezo isiyo na magoli, pia ni changamoto kubwa kwa wachezaji wa Yanga ambao wanahitaji kufunga ili kusonga mbele.

Mchezo wa tatu wa msimu huu kwa Milazare ulikuwa wa Ligi ya Mabingwa Afrika, na MC Alger walicheza ugenini dhidi ya TP Mazembe huko DR Congo. Katika mechi hiyo, hakuna timu iliyofunga bao na mechi hiyo ilimalizika 0-0. Alitoa kadi tatu za njano.

Kulingana na rekodi za mwamuzi huyo, kila hatua itahitaji umakini wa ziada ili kupambana na si tu wapinzani wao MC Alger, bali pia na mwamuzi huyu ambaye ni kama vile  ‘mfalme wa suluhu’.

Related Posts