SHIRIKISHO la Soka Afrika (CAF) limemteua mwamuzi Ahmed Arajiga na wenzake watatu kuchezesha mechi ya Kundi B Kombe la Shirikisho Afrika kati ya RS Berkane ya Morocco na Stellenbosch ya Afrika Kusini itakayopigwa Jumapili ya Januari 19.
Timu zote mbili tayari zimefuzu hatua ya robo fainali, Berkane ikiwa kinara wa kundi hilo baada ya kukusanya pointi 13, Stellenbosch nafasi ya pili na pointi tisa, Stade Malien nafasi ya tatu na pointi nne na Lunda Sul ikimaliza mkiani na alama mbili.
Mchezo huo utachezwa Uwanja wa Stade Municipal de Berkane, mjini Berkane akiwa nyumbani matokeo ya mchezo wa kwanza walipokutana vinara hao wa Ligi ya Morocco waliondoka na ushindi wa mabao 3-1.
Arajiga mara ya mwisho kuchezesha mechi za CAF ilikuwa Septemba 14 mwaka jana kati ya Red Arrows na TP Mazembe kwenye hatua za pili za Ligi ya Mabingwa.
Kwenye mchezo huo, Arajiga atasaidiana na waamuzi wengine wa Tanzania Mohamed Mkono, Kassim Mpanga na Nasir Salum.
Hii si mara ya kwanza kwa waamuzi wa Tanzania kuchezesha kwa pamoja mechi ya kimataifa Novemba 14, Arajiga akiwa kati na wenzake Frank Komba, Hamdani Said na Elly SasiiĀ waliamua mchezo wa kufuzu AFCON kati ya Lesotho na Central African Republic.
Arajiga ambaye tangu akabidhiwe beji ya Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) mwanzoni mwa mwaka 2022 amekuwa bora akipewa mechi mbalimbali za kimataifa.