WAKATI dirisha dogo la usajili likifungwa usiku wa jana, timu ya Azam imeondoa nyota watano ndani ya kikosi hicho, huku watatu wakitolewa kwa mkopo na wawili wakipewa mkono wa kwaheri.
Nyota walioachwa ni beki wa kati na kiungo, Yannick Bangala aliyeamua kurejea timu yake ya zamani wa AS Vita Club ya DR Congo, huku mwingine akiwa ni beki wa kushoto, Cheikh Sidibe aliyeitumikia Azam FC tangu Julai 2023, akitoka Teungueth ya Senegal.
Waliotolewa kwa mkopo ni kipa Ali Ahamada aliyeenda KMC kwa mkopo wa miezi sawa na Adam Adam aliyetua kwa Tanzania Prisons, wakiungana na beki wa kati, Abdallah Kheri ‘Sebo’, aliyejiunga dirisha hili dogo na kikosi cha Fountain Gate.
Licha ya Azam kuachana na nyota hao ila imesajili wengine wapya ambao ni, Zouzou Landry mwenye uwezo wa kucheza beki wa kushoto na kati aliyejiunga na kikosi hicho cha matajiri wa Jiji la Dar es Salaam akitokea AFAD Djekanou ya kwao Ivory Coast.
Mwingine ni aliyekuwa mshambuliaji kinda wa Dodoma Jiji, Zidane Sereri aliyejiunga na kikosi hicho kwa mkataba wa miaka mitano hadi mwaka 2030.