Unguja. Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale, Mudrik Ramadhani Soraga, amesema kuwa kuanzishwa kwa bima maalumu kwa watalii hakujapunguza idadi ya wageni kisiwani Zanzibar, bali kumechangia ongezeko la idadi yao.
Soraga alibainisha kuwa tangu bima hiyo ilipoanza kutumika rasmi mnamo Oktoba 1, 2024, kumekuwa na ongezeko la watalii kwa asilimia 17 kila mwezi.
Amesema kuwa rekodi mpya ilivunjwa mwezi Desemba 2024, ambapo watalii 91,611 walitembelea Zanzibar, idadi ambayo haijawahi kufikiwa. Takwimu za awali zinaonyesha kuwa watalii 60,731 waliingia Septemba, Oktoba walikuwa 69,860 na 67,449 waliingia Novemba.
Bima hiyo ya watalii, inayogharimu Dola za Marekani 44 (takriban Sh111,210), inalenga kuongeza usalama wa wageni na kuimarisha sekta ya utalii.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Waandaaji Misafara ya Watalii Zanzibar (Zato), Khalifa Mohamed Makame amesema hakuna athari hasi za moja kwa moja zilizoonekana kwa wanachama wa jumuiya hiyo.
Amesema viwango vya kukodi, vyumba vya hoteli na nyumba za wenyeji vimeendelea kuwa imara na hakuna dalili ya vyumba kubaki wazi.
Hivyo, Makame amesisitiza kuwa gharama ya bima haionekani kuwa mzigo mkubwa kwa watalii, akitoa mfano wa gharama za usafiri ndani ya kisiwa, kama kutoka Mji Mkongwe hadi Nungwi kwa Dola 50 (takriban Sh126,375). Aidha, amesema watalii wa kawaida hutumia wastani wa Dola 1,500 (Sh3.791 milioni) kwa wiki, hivyo ada ya bima inachukuliwa kuwa ya kawaida.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wawekezaji wa Mahoteli Zanzibar (Zati), Suleiman Mohammed amesema idadi ya watalii kutoka Ulaya imeongezeka na juhudi zinaendelea kuwavutia wageni zaidi kutoka Bara la Asia.
Mohammed amesema hali ya sasa inaendana na viwango vya kimataifa huku akisema nchi nyingi duniani zinahitaji wageni wao kununua bima za usalama wanapozuru.
“Kwa ujumla, wadau wa utalii wameeleza kuwa bima ya watalii imeleta manufaa kwa sekta hiyo, ikiwemo kuimarisha mnyororo wa thamani wa huduma za utalii na kuhakikisha usalama wa wageni wanaotembelea Zanzibar,” amesema Mohammed.