Dar es Salaam. Ukimwaga mboga, namwaga ugali. Huu msemo unaweza kuutumia kuelezea kile kinachoendelea ndani ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kwa sasa.
Hali hiyo inatokea katika kuelekea uchaguzi mkuu wa chama hicho, utakaofanyika Jumanne ya Januari 21, 2025 kwenye ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam.
Joto la uchaguzi huo linapanda kila kukicha na sasa imekuwa ‘piga nikupige’ baina ya makundi mawili yanayowania uenyekiti wa chama hicho. Ni timu Freeman Mbowe na Tundu Lissu.
Mbowe anatetea uenyekiti nafasi aliyuhudumu kwa miaka 21 huku Lissu ambaye ni makamu wake-bara anachuana naye. Kwa takribani wiki tatu sasa, imeshuhudiwa minyukano ya kila aina.
Baada ya minyukano ya kambi hizo mbili, kwa sasa viongozi waandamizi wa chama hicho wameanza kushambuliana wao kwa wao kupitia mikutano wanayoitisha na waandishi wa habari.
Januari 5, mjumbe wa Kamati Kuu ambaye ni mgombea makamu mwenyekiti- bara, John Heche anayemuunga mkono Lissu alimtuhumu Ezekiel Wenje kwamba ndiye amesababisha yote yanayoendelea kwa sasa ndani ya Chadema.
Jumanne Januari 14, aliyekuwa mwenyekiti wa kanda ya kaskazini Godbless Lema ambaye pia anamuunga mkono Lissu alieleza kiini za mzozo huo, akimkosoa Wenje kuwa aliwageuka katika mkakati wa kumshauri mwenyekiti mambo mbalimbali yanayoendelea katika chama hicho.
Wenje anayegombea nafasi ya makamu mwenyekiti akimuunga mkono Mbowe, ameibuka na kudai kuwepo kwa mkakati ulivyokuwa umesukwa ili kumpindua mwenyekiti wao Mbowe wakati akiwa gerezani akikabiliwa na kesi ya ugaidi.
Katika maelezo yake, Wenje ambaye ni mwenyekiti wa kanda ya victoria amesema mkakati huo uliratibiwa na Lema.
Wenje akasisitiza, angekuwa na uwezo, Lema hakupaswa kuwa ndani ya chama hicho.
Amedai sababu iliyomfanya kupishana na Lissu na Lema ni kukataa kuhusika na mapinduzi ya Mbowe akiwa gerezani.
Katika mkutano wake na wanahabari leo Alhamisi, Januari 16, 2025 jijini Dar es Salaam, Wenje amesema maswali kuhusu matumizi ya fedha za kampeni ya ‘Join the Chain’ yanapaswa kuelekezwa kwa Lema.
Kauli yake hiyo, inatokana na kile alichofafanua, Lema na wenzake ndio waasisi wa kampeni hiyo iliyokusanya fedha kutoka kwa makundi ya wananchi.
Wenje amesema, awali alikuwa timu Lissu pamoja na Lema, Heche na Mchungaji Peter Msigwa ambaye sasa yuko Chama cha Mapinduzi (CCM), walitaka kumpindua Mbowe lakini baadaye aliona si sahihi na kukimbia kundi hilo.
“Wanasema mimi ndiyo nimewafikisha hapa, basi kama ni hivyo nimefanya uenezi mkubwa sana wa chama chetu. Kila sehemu kinaongelewa basi ni kazi kubwa sana. Lakini Agosti 2024 nilitangaza nia tu nikiwa Mwanza ya kuwania umakamu mwenyekiti naanza kuambiwa nimetumwa na Mbowe.
“Nilipogombea ubunge Nyamagama hawakusema nilitumwa na mtu, nimegombea unyekiti wa kanda hawajasema nimetumwa na mtu, leo nagombea umakamu wanasema nimetumwa,” amesema Wenje katika kipindi hiki ambacho kumekuwa na maswali mengi yaliyokosa majibu kuhusu matumizi ya fedha hizo.
Katika ukurasa wake wa X, Mchungaji Msigwa aliyewahi kuwa mjumbe wa kamati kuu ameweka picha ya Wenje na kuandika: “Katika maisha yangu ya kufahamiana mpaka tukawa marafiki sikuwahi kujua kuwa Wenje ni muongo.”
“Wakati wa Join the Chain Lema, Wenje na Lissu walikuwa nje ya nchi, Mbowe alikuwa gerezani. Tulibaki mimi na John Heche. Tulihamasisha kukusanya fedha kwa ajili ya Baraza Kuu kwa kuwa, msajili alitishia kukifuta chama.
“Wala sio kufanya mapinduzi. Kwa kuwa umetaja jina langu, nitatoka na ushahidi mzito kuhusu wewe ili Watanzania wajue Siko kwenye chama chenu, lakini nitaweka mambo sawa kuwasaidia watu wakujue.”
Kwa upande wake, akijibu hilo, Lema amesema ataweka mambo hadharani kesho Ijumaa katika mkutano na waandishi wa habari atakaoufanya Dar es Salaam akiambana na watu mbalimbali.
“Niliwaonya wasizungumze kulinda heshima yangu kwa brother (kaka) Freeman Mbowe, lakini kwa kuwa wamekaidi nitaongea kesho kila kitu,” amesema.
Lema amesisitiza katika mazungumzo yake hayo ataeleza ukweli wa mengi aliyoyabeba moyoni, akidokeza dhambi haipaswi kukaliwa kimya.
Katika ukurasa wake wa X Lema aliweka picha zinazomwonesha Mbowe akishiriki kampeni hiyo ya Join the Chain na kuandika: “Mh Mwenyekiti, huyu Wenje anakuharibia sana heshima yako, kesho nitaongea, nitajitahidi tena kulinda heshima yako.”
Kampeni ya Join the Chain ilizinduliwa Machi 25, 2022 na Makamu Mwenyekiti wa Chadema Bara, Tundu Lissu akiwa uhamishoni nchini Ubelgiji.
Mbali na hao, Lissu naye mara kadhaa amekuwa akimshambulia Mbowe kwamba yote yanayofanyika sababu ni yeye akisema Mbowe aliyekwenda gerezani kutokana na kesi ya ugaidi si yule aliyetoka: “amebadilika sana.”
Mjumbe wa Bodi ya Wadhamini wa Chadema, Dk Azaveli Lwaitama akizungumza katika mkutano mkuu wa Baraza la Wanawake la chama hicho (Bawacha) uliohudhuriwa na Mbowe na Lissu amewataka wajumbe wa Bawacha kuhakikisha haki inatendeka katika mchakato huo uaminike kwa kila mtu.
Dk Lwaitama amefafanua kuwa, chama kikuu cha upinzani kitakuwepo lakini siyo lazima kiwe Chadema, lakini kikijichanganya baada ya uchaguzi kitafutwa ingawa siyo rahisi.
“Jiepusheni na ulevi wa ushindi, yeyote atakayeshinda namweleza hivyo hivyo, ndugu yangu Deo (Mahinyila- mwenyekiti wa Bavicha) ogopa ulevi wa ushindi, ogopa wapambe wanaokwambia bado upo kwenye ushindani wakati umeshatangazwa,” amesema.
“Ukishatangazwa wewe ni wa wote, jiepushe na ulevi wa ushindi iwe ni Bawacha, Bavicha au Bazecha, iwe ni Taifa yeyote atakayeshinda mimi hanihusu jiepusheni na ulevi unajua wakati mwingine ushindi una kupa kiburi ambacho ni jambo zuri pale unapopambana na unayeshindana naye siyo baada ya uchaguzi,” amesema.
Mgombea wa nafasi ya uenyekiti Chadema, Odero Odero amewataka Bawacha wasijione wanyonge na katika uchaguzi mkuu wa baraza hilo, wasifanye uamuzi kwa ufuasi wa wagombea watatu wa nafasi ya uenyekiti wa chama hicho.
“Asijitokeze mwanamke akapiga kura kwasababu ya Freeman Mbowe au Tundu Lissu, najua ninyi mnajua maana ya wivu kilindeni chama hiki kwa wivu,” amesema Odero.
Katika hatua nyingine, Odero amekemea tabia aliyodai imeanza kujitokeza kwa baadhi ya wanachama wa Chadema kukimbilia kwenye vyombo vya habari na kuzungumza.
“Niseme hili kama mwanachama, tabia hiyo ikiendelea tutahamasisha wanachama wachukue hatua dhidi ya chama chao,” amesema Odero ambaye ni mwanaharakati wa haki za binadamu.
Akifungua mkutano wa Bawacha, Mbowe amewataka viongozi wapya wa mabaraza ya vijana, wanawake na wazee watakaochaguliwa kuhakikisha chama hicho, kinajibu changamoto za kijamii na wananchi, siyo masuala yanayohusu siasa pekee.
Amesema kuna programu ya Chadema Family ambayo haijafanikiwa kwa sababu haikupewa umuhimu mkubwa, hivyo kuanzia sasa ipewe kipaumbele katika uongozi mpya.
“Yeyote atakayeingia kuongoza chama, kwenye chama na mabaraza ahakikishe tunakwenda kuhuisha uwepo wa Chadema Family katika kaya moja moja. Kila mwanachadema atambue kuhusika kuijenga na kuiboresha jamii.
“Kila mwanachama wa Chadema atambue yeye ni bega la kumlilia mwanachadema mwenzake anayefikwa na matatizo katika maeneo yake. Tunataka wanachadema wote mbali na majukumu yenu ya kisiasa, tujipe majukumu ya kuilea jamii,” amesema Mbowe.
Akiendelea na hoja kuhusu umuhimu wa Chadema kuwa karibu na jamii, Mbowe amesema: “Kila mtaa mmoja wenye tawi la Chadema basi, wanachadema wote wanakuwa familia, ikitokea mmoja wetu amefikwa na msiba au ugonjwa, tunapaswa kuungana na kushikana mikono, tukamsaidie kupika, kubeba mahema.”
“Iwe ni marufuku kwa mwanachadema yeyote kuona mwenzake anapata shida, kuona shida hiyo haimuhusu, shida ya mwanachadema ni shida yetu wote. Tusisubiri kuwa chama cha uchaguzi, bali tuwe chama kinachoishi maisha ya kila siku ya wana jamii na ninyi kina mama mkiamua kuchukua wajibu huo, chama hiki kitakuwa cha tofauti,” amesema Mbowe.
Katika mkutano huo wa Bawacha, Lissu amelitaka baraza hilo kupigania mabadiliko ili kupata uwakilishi wa wanawake kwa usawa kwenye vyombo uamuzi.
Amesisitiza Chadema inahitaji viongozi wa kupigania mabadiliko na wanaojua bila mabadiliko hayo idadi ya wanawake bungeni haitoongezeka.
“Kwa hiyo kwenye uchaguzi huu jiulizeni wagombea tulionao wanaweza haya majukumu? Kama wanaweza wape kura, kama unaamini wanaweza majukumu ya kupigania reform (mabadiliko) wape kura, usiwape kwa sababu wamekulaza hoteli fulani,” amesema.
Msimamo wa Lissu kwa Bawacha, ni baraza hilo kutambua viongozi watakaochaguliwa ndio watakaosaidia upatikanaji wa wabunge na madiwani pamoja na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
“Wote mnafahamu wanawake wa Tanzania ni wengi zaidi kwa idadi kuliko wanaume, mnajua wanawake ndio wapigakura wengi kuliko wanaume na wanawake katika nafasi za uongozi ni wachache kuliko wanaume?
“Inakuaje hawa ambao ni wengi zaidi kwa idadi na wapigakura wawe wachache zaidi katika uongozi wa bunge na halmashauri,” amehoji.