Dorothy ajitosa kupambana na Samia

Dar es Salaam. Kiongozi wa ACT-Wazalendo, Dorothy Semu ametangaza nia ya kugombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwenye uchaguzi mkuu baadaye mwaka huu, akitaja mambo manne yaliyomsukuma kuitaka nafasi hiyo.

Iwapo atapitishwa na chama chake kuwania nafasi hiyo, atakuwa mgombea wa mwingine mwanamke katika uchaguzi wa mwaka huu. Anatarajiwa kuchuana na Rais Samia Suluhu Hassan wa Chama cha Mapinduzi (CCM).

Semu ametangaza nia kuwania nafasi hiyo leo Januari 16, 2025 ikiwa ni siku moja baada ya chama hicho kuwaalika wanachama kujitokeza kutangaza nia za kuwania nafasi za udiwani, ubunge na urais katika uchaguzi wa Oktoba, mwaka huu.

Amesema katika kipindi cha miaka kadhaa iliyopita, Taifa limekumbwa na changamoto zilizosababisha kudumaa kwa maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

“Pamoja na ujio wa 4R za Rais Samia Suluhu Hassan, kuna upungufu mkubwa unaohitaji uongozi thabiti, wa uwazi na wenye malengo halisi kwa manufaa ya Watanzania wote,” amesema.

Ametaja mambo yanayohitaji uongozi thabiti kuwa ni kushuka kwa kasi ya ukuaji wa uchumi, kupanda kwa gharama za maisha, changamoto za ajira kwa vijana na Serikali ya CCM chini ya Rais Samia kuwa na udhaifu katika usimamizi wa rasilimali za Taifa.

Amesema licha ya Serikali kueleza uchumi unakua, ripoti ya Benki ya Dunia ya mwaka 2024 inaonyesha kasi ya ukuaji wa uchumi imeshuka kutoka asilimia 6.8 mwaka 2019 hadi asilimia 4.6 mwaka 2023, akidai hali hiyo inasababishwa na sera zisizo thabiti za uwekezaji na utekelezaji hafifu wa miradi ya maendeleo.

Amesema takwimu za Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) zinaonyesha kiwango cha mfumuko wa bei kimefikia asilimia 5.6 mwaka 2023, ikilinganishwa na asilimia 3.5 mwaka 2020, hali aliyodai inaendelea kujirudia na inaathiri uwezo wa wananchi kumudu mahitaji ya msingi, hususani vyakula na huduma za afya.

“Kwa mujibu wa ripoti ya Taasisi ya Utafiti na kupunguza Umasikini Tanzania (REPOA) ya 2019, takribani vijana milioni moja wanahitimu kila mwaka huku idadi inayoajiriwa serikalini na sekta binafsi ni 250,000, kwa wastani wa kila mhitimu anatumia wastani miaka 5.5 kupata ajira,” amesema.

Amesema Serikali imeshindwa kuwekeza vya kutosha katika sekta zinazoweza kuzalisha ajira kama kilimo, viwanda, na teknolojia, hivyo akipata ridhaa ya chama chake, atahakikisha anasimamia vyema eneo hilo kuwezesha vijana kujiajiri na kuajiriwa.

Amesema Tanzania inahitaji uongozi mpya utakaolinda masilahi ya Taifa na uchumi imara, jamii yenye fursa sawa na uongozi wa uwazi.

Semu amesema uzoefu alionao kwenye uongozi ni turufu anayoamini itambeba.

“Nipo kwenye uongozi na kwenye siasa kwa miaka 10 naamini nimeiva, pia nipo kwenye chama chenye sera na ilani bora, kinaonyesha tofauti na kujisimamia chenyewe.

“ACT ina miaka 10 tangu kuanzishwa, kinazidi kukua kwa kasi na kutekeleza masuala mbalimbali kama chama makini chenye mikakakati bora na endelevu. Mikakati hii inatuongoza katika hatua ya kwenda kushika dola na itatuletea matokeo bora na kutupa majimbo ya kutosha kuunda Serikali,” amesema.

Mchambuzi wa masuala ya siasa, Dk Richard Mbunda amesema alichofanya Semu ni demokrasia na ni haki ya mtu mwenye vigezo kudhani anaweza kugombea hiyo nafasi.

“Hapo sasa ni jukumu la chama chake kumpitisha ili atimize azma yake hiyo, ukiangalia siasa za Semu na alivyokuwa Anna Mghwira (aliwahi kugombea urais) ni watu ambao wanafanana katika kujenga hoja na masuala mengine ya kisiasa,” amesema.

Amesema Semu kama atapata fursa hiyo bila shaka atatoa changamoto ya kutosha kwenye uchaguzi huo ambao suala la usawa wa kijinsia litapewa kipaumbele.

Mwanasiasa mkongwe, Hashimu Rungwe amesema Semu yuko sahihi kutangaza nia kwa kuwa amejipima na kuona anatosha kugombea.

“Ni haki yake na yupo sahihi, ajaribu aone, chama chake kikimpitisha na uchaguzi mkuu ukawa huru na wa haki anaweza kufanya kitu,” amesema Rungwe.

Semu aliamua kuacha kazi kama mtumishi wa umma katika Wizara ya Afya na kuingia kwenye siasa, akilenga kushiriki michakato itakayochochea mabadiliko yatakayoleta maisha bora kwa wananchi.

Wasifu wake kama mtaalamu wa tiba  mazoezi, ulimfanya anafanikiwe kuajiriwa serikalini na kabla ya kuingia rasmi kwenye siasa, amefanya kazi wizarani kwa miaka 12 mfululizo kama ofisa wa programu ya kifua kikuu na ukoma nchini, ndipo akaamua kuacha kazi.

Dorothy aliyezaliwa mwaka 1975 alipata Shahada ya Uzamili katika tiba ya mazoezi ya mwili (Physiotherapy) kutoka Chuo Kikuu cha Western Cape, Afrika Kusini.

Kazi zake zilihusisha kutibu wagonjwa na kusimamia programu za afya, hasa katika eneo la kudhibiti ulemavu wa ukoma.

Dorothy ndani ya ACT-Wazalendo amefanya kazi akiwa Katibu wa Sera na Utafiti wa chama hicho.

Katibu Mkuu wa ACT- Wazalendo kati ya mwaka 2017 na 2020, kisha alichaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa ACT- Wazalendo (Bara).

Amekuwa Waziri Mkuu Kivuli wa ACT-Wazalendo kuanzia mwaka 2020 mpaka mwaka 2022.

Machi 6, 2024 alichaguliwa kuwa Kiongozi wa ACT-Wazalendo, akichukua nafasi ya Zitto Kabwe aliyemaliza muda wake.

Related Posts