WAKATI Shirikisho la Soka Afrika (CAF) likiifungia Simba kucheza mechi moja ya nyumbani bila mashabiki huku likiipiga faini ya Dola 40,000, kocha mkuu wa timu hiyo, Fadlu Davids amefichua ukweli akisisitiza kuwa ana mpango tofauti.
Mchezo wa wikiendi iliyopita dhidi ya Bravos do Maquis ya Angola, Simba iliotoka sare ya 1-1, uliwafanya vijana hao wa Fadlu kutinga hatua hiyo baada ya kufikisha pointi 10 katika kundi A nyuma ya CS Constantine wenye pointi 12 huku ikiwa imesalia raundi moja kutamatisha hatua ya makundi na itacheza wikiendi hii nyumbani dhidi ya CS Constantine.
Fadlu amefichua kwamba shauku yake ni Ligi ya Mabingwa msimu ujao, hivyo ikitokea msimu huu wakashinda ubingwa wa Ligi Kuu Bara au hata Shirikisho anaona nafasi ya kushinda taji hilo la Afrika ipo.
“Nilijiunga na timu wakati mgumu mwanzoni mwa msimu, na Simba ilikuwa imemaliza ligi ikiwa ya tatu. Ilikuwa ni fursa nzuri kwangu na Klabu ya Simba kujenga timu upya. Nina wachezaji wengi vijana na nina wachezaji wenye nguvu.
“Bila shaka tungependa kucheza katika Ligi ya Mabingwa kwa sababu hayo ni mashindano ambayo ni makubwa zaidi barani Afrika, lakini kwangu mimi, nilichagua kujenga timu kwanza kwa sababu matokeo hayakuwa mazuri kabla, na sasa nina timu mpya, na ikiwa tutamaliza mashindano haya na kuwa mabingwa wa ligi au tukishinda Kombe la Shirikisho, nadhani tutafanya vizuri zaidi katika Ligi ya Mabingwa baada ya hapo,” alisema Fadlu.
KUKOSA MASHABIKI DHIDI YA CONSTANTINE
CAF imeishushia rungu Simba kufuatia vurugu zilizotokea katika mchezo wa tatu wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya CS Sfaxien uliochezwa Desemba 15, 2024 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam na Simba kushinda 2-1. Vurugu hizo zilisababisha viti 256 kuvunjwa.
Fadlu ambaye alifanya mahojiano maalum na televisheni ya Al Ahly kutoka Misri, alisema: “Ulikuwa ni uamuzi usiokuwa sahihi kwetu. Ukweli ni kwamba kile kilichotokea kilitokea upande wa benchi au Klabu ya Sfaxien. Walianza vurugu dhidi ya wachezaji wetu. Hali hii haikuwa kutoka kwa mashabiki pekee. Huu ni uamuzi usio wa haki kwetu, hasa kwa kuwa kilichotokea kilianza kutoka kwa wachezaji wa Sfaxien na wachezaji wa akiba,” alisema.
Fadlu amebainisha kwamba, jambo hilo limewahuzunisha kwani walitarajia kuujaza uwanja kupitia mashabiki wa Simba waliokuwa na shauku kubwa ya kuishangilia timu yao katika mchezo huo wa mwisho hatua ya makundi ambao wanahitaji kushinda ili kuongoza kundi.
“Tulitarajia uwanja uwe na mashabiki wengi ambao wangeongeza nguvu kwetu na presha kwa wapinzani, lakini ikiwa tunataka kushinda, tutacheza mechi yetu bila kuangalia kutakuwa na mashabiki au hakuna mashabiki,” alisema Fadlu.
Fadlu anatamani kuifunga CS Constantine licha ya kwamba mechi haitakuwa na mashabiki kwani lengo ni kumaliza vinara ili hatua ya robo fainali kuwakwepa vigogo na iwe nafuu zaidi kwao.
Kocha huyo raia wa Afrika Kusini, amebainisha kuwa shauku yake kubwa ni kuichapa Constantine na kuongoza kundi ili robo fainali wasikutane na vigogo kama RS Berkane, Zamalek na USM Alger ingawa anaamini ili timu ifanye vizuri zaidi hutakiwi kumuhofia mpinzani yeyote.
“Tuna shauku kubwa ya kushinda mechi hii na kutinga raundi inayofuata kama vinara wa kundi, ninarudia tena, ni bora kwetu kujaribu kushinda, iwe kuna mashabiki au hakuna mashabiki, kwa mapenzi ya Mungu tutafanikiwa.
“Ni muhimu kwetu kumaliza hatua ya makundi tukiwa vinara, kwa sababu hii itatuepusha na baadhi ya timu kubwa kama Zamalek ambao wana uzoefu mkubwa, lakini hata Al-Masry hivi sasa inafanya vyema na inaonekana ni timu ngumu na yenye nguvu sana, lakini kama unataka kushinda mashindano haya, lazima uwe tayari kujiandaa na kufanya mambo iwe rahisi kwako.
“Kumaliza kundi ukiwa wa kwanza, hii itafanya mambo kuwa rahisi kwetu katika hatua inayofuata. Ukiangalia timu yoyote ambayo Simba itakutana nayo kwa sasa, itapambana kujaribu kushinda, iwe ni timu ya kwanza au ya pili katika kundi, hivyo kuna ugumu.”
Simba inashika nafasi ya pili Kundi A katika Kombe la Shirikisho Afrika ikiwa na pointi 10 nyuma ya vinara Constantine (12) huku zote zikifuzu. Mechi ya Jumapili itazikutanisha timu hizo ambapo Simba inahitaji kushinda ili kumaliza kileleni wakati Constantine inataka sare tu kuzima matumaini ya mpinzani wake.