Musoma. Serikali imeanza mchakato wa kuwalipa fidia wamiliki wa nyumba 50 zilizopo jirani na Uwanja wa Ndege wa Musoma, mkoani Mara, ili kupisha upanuzi wa uwanja huo. Wakazi hao wanatakiwa kuondoka katika maeneo hayo ndani ya siku 90 baada ya kupokea malipo yao.
Malipo haya yanakuja baada ya wakazi hao kusubiri kwa takriban miaka minane.
Imeelezwa kuwa jumla ya Sh3.9 bilioni zitatumika kuwalipa fidia wakazi hao, na malipo hayo yameanza kutolewa leo Alhamisi, Januari 16, 2025.
Akizungumza na wakazi hao mjini Musoma leo, Meneja wa Wakala wa Barabara Nchini (Tanroad) Mkoa wa Mara, Vedastus Maribe amewahimiza wakazi hao wenye migogoro ya umiliki wa mali kutatua changamoto hizo ili waweze kulipwa fidia. “Tayari kuna baadhi ya familia zimeanza migogoro na sisi hatuwezi kulipa pale penye migogoro. Nawasihi mzitatue haraka iwezekanavyo ili muweze kulipwa, kwa sababu fedha hizi ni halali yenu na tayari zimetolewa kwa ajili ya kazi hiyo,” amesema Maribe.
Amesema ujenzi wa uwanja huo unaendelea kwa gharama ya zaidi ya Sh35 bilioni na sasa umefikia asilimia 57 ya utekelezaji wake.
Hii ni awamu ya pili ya malipo ya fidia, baada ya yale ya awamu yaliyofanyika mwaka 2021, jumla ya Sh4.1 bilioni zililipwa kwa wakazi 86.
“Wakazi wa Mtaa wa Nyasho Kati wametakiwa kuondoka katika eneo hili kwa sababu uwepo wao utaathiri shughuli za ujenzi wa uwanja wa ndege, ikiwa ni pamoja na kuzuia ndege kubwa kutua. Tunaomba kila mmoja aondoke baada ya kupokea malipo yake ili kuruhusu shughuli zingine kuendelea,” amesisitiza Maribe.
Mkuu wa Wilaya ya Musoma, Juma Chikoka amewataka wakazi hao kuhama kwa amani baada ya kupokea fidia zao.
“Mko huru kuondoka na vitu vyenu kama mabati, mbao, matofali na vingine ambavyo mngependa kuvichukua. Sisi tunachohitaji ni ardhi tu. Mmepewa muda wa kutosha kabisa, naomba hili jambo tulianze na kulimaliza kwa amani, hakuna sababu ya kutumia nguvu,” amesema Chikoka.
“Watalii na wafanyabiashara wataweza kuanzia shughuli zao hapa Musoma baada ya kutua uwanjani. Hii itachangia maendeleo ya kiuchumi tunayoyataka kwa Musoma,” amesema Chikoka.
Baadhi ya wakazi waliopokea fidia wamemshukuru Mkuu wa Mkoa wa Mara, Evans Mtambi kwa juhudi zake za kusaidia kufanikisha malipo hayo.
“Kwa kweli mkuu wetu wa mkoa ametutendea haki. Tumeanza suala hili miaka mingi na tulipata taabu sana, lakini yeye alituhakikishia kuwa atalishughulikia na kweli ndani ya muda mfupi tumepata fidia zetu kwa amani,” amesema Otieno John.
Naye mkazi mwingine Elizabeth Joliga amesema malipo hayo ni mwanzo wa hatua yao ya kuhama na kuunga mkono utekelezaji wa mradi huo.
Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Nyasho Kati, Biseko Biseko amewahimiza wakazi wake kufuata taratibu za usalama wanapohamisha mali zao.