JAMII YATAKIWA KUPIMA AFYA MAPEMA KUCHUKUA TAHADHARI ONGEZEKO LA MARADHI YA SARATANI NCHINI

Na Khadija Khamis, WHVUM

Msaidizi Meneja Kitengo cha Maradhi yasioambukiza (NCDs UNIT) kutoka Wizara ya Afya Zanzibar, Zuhura Saleh Amour amewataka Wananchi kuchukuwa tahadhari kutokana na ongezeko la maradhi ya saratani Nchini.

Ameyasema hayo wakati wa Mafunzo kwa Maafisa Mipango wa Wizara mbali mbali za Serikali, yaliofanyika hivi karibuni katika kituo cha Afya ya uzazi na Mtoto Kidongo Chekundu Wilaya ya Mjini.

Amesema Hospitali ya Oceon road Jijini Dar-es-salaam imesema inapokea wateja wengi kutoka Zanzibar hivyo ni vyema jamii kupima afya mapema ili kujuwa matatizo walionayo mapema na kuyapatia ufumbuzi wa haraka.

“Kadri umri unavyokwenda kuna hatari ya kupata saratani na baadhi ya wenzetu akinababa wanachelewa kupima afya zao na kupelekea kukosa huduma mapema jambo ambalo linachangia ongezeko la maradhi hayo” amesema Bi Zuhura.

Aidha amesema iwapo maradhi ya saratani yatagundulika katika hatua za awali, inaweza kutibika na kuokoa maisha ya mtu.

Mbali na hayo amesema tatizo la Saratani linapoanza huwa halionyeshi dalili hivyo ni vyema jamii kuhamasika kufanya mazowezi ili kupunguza uzito na kupaki salama.

Hata hivyo ameishauri jamii kupunguza matumizi ya mafuta kwa wingi ili kuzuia kuganda katika mifupa na kusababisha maradhi yasioambukiza.

Nae Mkufunzi wa Maradhi yasioambukiza kutoka Hospitali ya Rufaa Mnazimmoja Dkt. Salum Saleh Mwinyi ameitaka jamii kuchukuwa hatua kwa Watoto na Vijana wao, wanaojishughulisha na utumiaji wa Sigara, Shisha, electroninic sigaret, Tumbaku, Bangi kwani vinachangia kwa kiasi kikubwa kuiathiri jamii.

Amesema vifo vinavyotokana na Tumbaku ni zaidi kuliko Ukimwi, Malaria na Kifua kikuu huku akibainisha kuwa katika Nchi zenye maendeleo, matumizi ya Tumbaku yamepunguwa ikilinganishwa na Nchi zisizokuwa na maendeleo.

Kwa Upande wa Meneja wa Jumuiya ya Watu wanaoishi na Maradhi yasioambukiza Haji Khamis Fundi amesema lengo la kuanzishwa Jumuiya hiyo ni kuwasaidia Wagonjwa kuwaunganisha pamoja na kupaza sauti zao.

Amesema wamekuwa wakifanya kazi mbalimbali ikiwemo kujenga uwezo wa kutoa elimu kwa jamii kupitia njia mbalimbali kama vile kusambaza vipeperushi,Vijarida pamoja na Fulana, zenye ujumbe makhsus unaohusiana na maradhi yasioambukiza.

Aidha amesema pia Jumuiya hiyo inatoa utetezi ushauri nasihi kwa waathirika wa maradhi hayo sambamba na kupima afya zao ili waweze kuishi katika hali ya amani na kufuata maelekezo wanayopewa na Wataalamu wa Afya.

Jumuiya ya Maradhi yasioambukiza, imeanzishwa tarehe 01.07.2012 na inahusisha Muungano wa Watu wanaoishi na maradhi mbalimbali ikiwemo Kisukari, Saratani, Moyo, Mifupa pamoja na kukauka damu.

Msaidizi
Meneja Kitengo cha Maradhi yasioambukiza (NCDs UNIT) kutoka Wizara ya Afya
Zanzibar, Zuhura Saleh Amour akitoa Mafunzo kwa Maafisa Mipango wa Wizara mbali
mbali za Serikali, yaliofanyika hivi karibuni katika kituo cha Afya ya uzazi na
Mtoto Kidongo Chekundu Wilaya ya Mjini.

Mkufunzi wa Maradhi yasioambukiza kutoka
Hospitali ya Rufaa Mnazimmoja Dkt. Salum Saleh Mwinyi akitoa elimu ya madhara
ya Tumbaku wakati wa Mafunzo kwa Maafisa Mipango wa Wizara mbali mbali za
Serikali, yaliofanyika hivi karibuni katika kituo cha Afya ya uzazi na Mtoto
Kidongo Chekundu Wilaya ya Mjini.

Meneja wa Jumuiya ya Watu wanaoishi na Maradhi yasioambukiza Haji Khamis Fundi akitoa
historia ya jumuiya kwa Maafisa Mipango wa Wizara mbali mbali za
Serikali, yaliofanyika hivi karibuni katika kituo cha Afya ya uzazi na
Mtoto Kidongo Chekundu Wilaya ya Mjini.

 

Related Posts

en English sw Swahili